Ufaransa yaahidi kushirikiana na Magufuli

Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Frederick Clavier

Muktasari:

  • Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Frederick Clavier amesema Serikali yake itaendelea kushirikiana na Rais John Magufuli katika uongozi wake wa Sadc baada ya kukabidhiwa uenyekiti wa jumuiya hiyo kwenye mkutano wa Agosti 17 na 18 mwaka huu utakaofanyika hapa nchini.

Dar es Salaam. Serikali ya Ufaransa imeahidi kushirikiana na Rais wa Tanzania, John Magufuli katika kipindi chote cha uenyekiti wake wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Africa (Sadc).

Hayo yalibainishwa jana Jumamosi Julai 13, 2019  jijini Dar es Salaam na balozi wa Ufaransa, Frederick Clavier katika hafla ya maadhimisho ya mapinduzi ya Ufaransa ya mwaka 1789.

Clavier amesema uhusiano kati ya Tanzania na Ufaransa umedumu kwa sababu ya ushirikiano uliopo uliochangiwa zaidi na ziara za viongozi wa mataifa hayo.

“Ufaransa na Tanzania tumeamua kuboresha uhusiano wetu wa kidiplomasia na kuupeleka mbali zaidi hasa katika kuwaletea wananchi maendeleo kupitia miradi mbalimbali,” amesema balozi huyo.

Tanzania imedhamiria kufanya biashara zaidi ya Ufaransa na kupata wawekezaji wengi kutoka Ufaransa, “Tunakaribisha kampuni kutoka Ufaransa kuja kuwekeza hapa nchini.”