Uganda yataka kumhifadhi al Bashir

Muktasari:

  • Umoja wa Afrika (AU) watishia  kuisimamisha uanachama Sudan ikiwa jeshi litashindwa kukabidhi madaraka kwa raia ndani ya siku 15

Kampala,Uganda. Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda imesema nchi hiyo iko tayari kumpa hifadhi ya kisiasa aliyekuwa Rais wa Sudan, Omar al-Bashir kama akiomba.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Henry Okello Aryem ameiambia kamati ya bunge ya masuala ya kimataifa ya nchi hiyo kuwa, Rais huyo aliyeondolewa madarakani ni mdhamini wa makubaliano ya amani ya Sudan Kusini.

Amesema mamlaka nchini Uganda zinafuatilia kwa karibu hali inayoendelea nchini Sudan ambako maandamano yanaendelea baada ya jeshi kumwondoa al-Bashir madarakani wiki iliyopita.

Rais Yoweri Museveni wa Uganda na al-Bashir ni wadhamini wa makubaliano ya amani ya Sudan Kusini.

Jana Umoja wa Afrika (AU) ulitishia  kuisimamisha uanachama Sudan ikiwa jeshi litashindwa kukabidhi madaraka kwa raia ndani ya siku 15.

Katika taarifa yake, Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika limesema AU itasitisha ushiriki wa Sudan katika shughuli zote hadi pale amri ya kikatiba itakaporejeshwa.

Wito huo wa AU unafuatia mapinduzi ya wiki iliyopita yaliyoshuhudia Bashir akiondolewa madarakani na jeshi.

Bashir ameitawala Sudan kwa miaka 30 kabla hajaondolewa wiki iliyopita kufuatia maandamano ya nchi nzima yaliyoanza mwezi Desemba. Hata hivyo, AU imesifu  madai ya waandamanaji na kuita uingiliaji wa jeshi kuwa ni mapinduzi ambayo imeyalaani.

Umoja wa Afrika ulio na wanachama 55 umeongeza kuwa, Serikali ya mpito ya kijeshi ni tofauti na matakwa ya watu wa Sudan. Umoja huo umekuwa na msimamo mkali kuhusiana na mapinduzi na uliwahi kuzisimamisha Misri na Jamhuri ya Afrika ya Kati mwaka 2013 kufuatia mapinduzi katika nchi hizo mbili.

Shirika la habari la Sudan (Suna) limearifu kuwa kiongozi wa baraza la kijeshi, Abdel Fattah al-Burhan amepokea simu kutoka kwa mfalme wa Saudi Arabia, viongozi kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu, Qatar, Waziri Mkuu wa Ethiopia na Rais wa Sudan Kusini wakionyesha kuunga mkono hatua hiyo ingawa wameelezea wasiwasi wao kwa mustakabali wa taifa hilo.