Wananchi wa Msumbiji waanza kupata msaada

Muktasari:

  • Idadi ya watu waliokufa kutokana na kimbunga Idai mpaka sasa imefika 446 nchini Msumbiji, 259 Zimbabwe na 56 nchini Malawi

Beira.Msumbiji. Serikali ya Msumbiji imesema hali katika maeneo yaliyokumbwa na kimbunga Idai imeanza kuwa nzuri kuwezesha kupelekwa misaada ya haraka.

Aidha, imesema barabara muhimu inayoelekea katika mji wa Beira imefunguliwa.

Jeshi la Marekani limesema litaungana na mashirika ya kimataifa ya wahisani katika shughuli za kugawa dawa na chakula kwa watu walioathiriwa na kimbunga hicho kilichosababisha maafa makubwa ambayo hayajawahi kutokea eneo la Kusini mwa Afrika.

Waziri wa mazingira wa Msumbiji, Celso Correia amesema watu 228,000 wamehifadhiwa kwenye kambi za muda baada ya kukumbwa na mafuriko.

 Pia kuna taarifa juu ya kuzuka magonjwa ya kuendesha, lakini Correia amesema bado ni mapema kujua iwapo ugonjwa huo ni kipindupindu.