Washtakiwa kwa kuendelea kumshikilia mlinzi wa Bobi Wine

Monday September 10 2018

 

Kampala, Uganda. Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Uganda, Grace Akullo anashtakiwa kwa madai ya kuendelea kumshikilia kinyume cha sheria mlinzi binafsi wa Mbunge wa Kyadondo Mashariki, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine.
Mlinzi huyo Edward Ssebuufu maarufu kama Eddie Mutwe kupitia kwa wanasheria wake wa kampuni ya Kiiza & Mugisha Advocates, walifungua kesi Mahakama Kuu jijini Kampala Ijumaa akiomba aachiwe bila masharti yoyote kwa kuwa anazuiwa kinyume cha katiba inayoruhusu saa 48 tu mtu kushikiliwa.
Wengine walioshtakiwa pamoja na Akullo ni ofisa mfawidhi wa upelelezi wa uhalifu wa kituo cha Kibuli, Eliao Moses ambaye ni naibu kamanda wa polisi kituo cha Jinja na mwanasheria mkuu.
“Hili ni tangazo kwamba vitendo vya wajibu mashtaka (Akullo na wenzake) vya kuendelea kumshikilia mlalamikaji (Mutwe) nje ya muda was aa 48 uliowekwa kikatiba, tangu Agosti 25, 2018 ni ukiukwaji wa misingi ya haki za binadamu na haki kwa uhuru wa mtu binafsi, heshima na utawala wa haki kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Uganda ya mwaka,” inasema sehemu ya nyaraka zilizoko mahakamani.
Mutwe pia anataka Akullo na wenzake kumlipa kwa madhara aliyopata kwa kumweka kizuizini kinyume cha sheria jumuisha na athari za mateso ya kisaikolojia na akili.
Kwa mujibu wa nyaraka za Mahakamani ambazo gazeti la The Monitor limefanikiwa kuziona, Mutwe alikamatwa na vikosi vya usalama Agosti 25 kutoka Semakokiro Plaza kitongoji cha Kamwokya jijini Kampala na baadaye alipelekwa na kuwekwa katika kizuizi cha makao makuu ya Idara ya Upelelezi wa Kijeshi (CMI) Mbuya.
Baadaye alisafirishwa hadi kizuizi cha polisi Agosti 31 mwaka huu ikidaiwa kutokana na amri iliyotolewa na Akullo na wenzake.
Agosti 30, Jaji Musa Sekaana wa Mahakama Kuu jijini Kampala, alitoa amri akitaka jeshi na mwanasheria mkuu kumfikisha Mutwe mahakamani akiwa “mfu” au “hai” ifikapo Septemba 4.
“Amri hiyo ilipuuzwa na wajibu mashtaka (Akullo na wenzake) na mlalamikiwa wa pili (Womanya), alifikia kuidanganya mahakama Septemba 4 kwamba mlalamikaji (Mutwe) alikuwa anatarajiwa kusafirishwa hadi Mahakama ya Hakimu Mkazi Gulu,” hati ya mashataka ya shauri hilo inasema.

Advertisement