Kimei aomba kasi Brela

Muktasari:

Ni katika mkutano wa 11 wa TNBC

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk Charles Kimei ameuomba Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) uendelee kuingiza taarifa ya mali za wateja.

Amesema benki haiwezi kukopesha bila kuwa na taarifa za kampuni kutoka Brela.

Kauli hiyo ameitoa leo Machi 19, 2018 wakati wa Mkutano wa 11 wa Baraza la Taifa la Biashara, uliobeba maudhui ya ‘Tanzania ya Viwanda na Ushiriki wa Sekta binafsi nchini.

“Kwa upande wa Brela waendelee kuharakisha kuingiza taarifa ya mali za wateja hasa kampuni, hatuwezi kukopesha bila kuwa na taarifa hasa benki za nje zinavyofanya biashara na sisi,”amesema.

 

Hata hivyo, Dk Kimei ameishukuru Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) hususani wizara ya fedha kwa mambo yaliyotekelezwa hadi sasa hivi ikiwamo kushusha viwango vya riba.

Amesema hatua hiyo inasababisha pia mabenki nayo kulazimika kushusha riba zake.

“Serikali inaweza kukopa sasa kwa riba ya asilimia kati ya sita na nane kwa hiyo mabenki nayo yanalazimika kushusha riba zake, nimezungumza na wenzangu hapa riba za mabenki zitashuka, naamini mtaanza kuona riba zinashuka polepole,”amesema.