VIDEO: Kinana atoa neno kwa wabunge CCM

Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Abdulrahman Kinana akizhutubia wabunge katika hafla aliyoandaliwa na wabunge wa CCM ya kumuaga  na kumkaribisha Katibu Mkuu mpya, Dk Bashiru Ally, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Kinana asema hana shaka na mrithi wake Dk Bashiru Ally


Dodoma. Aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana amewaaga wabunge wa chama hicho akiwahusia wanachopaswa kufanya ili kuendelea kujenga imani kwa wananchi.

Kinana amesema hayo Juni 19, 2018 katika halfa iliyoandaliwa na wabunge wa CCM ya kumuaga na kumkaribisha Katibu Mkuu, Dk Bashiru Ally iliyofanyika katika hoteli ya Morena jijini Dodoma.

Amesema chama hicho kimekuwa na makatibu wakuu kadhaa na kila mmoja aliondoka kama yeye.

"Nilijitahidi kujitolea, kufanya kazi, kujituma kwa maarifa yangu yote na ninyi ndio mtakaonihukumu kama nilifanya kazi ipasavyo," amesema.

Kinana amesema kama kuna upungufu uliojitokeza anakiri kwamba ni wake binafsi na kama kuna mafanikio hayakuwa na maarifa na juhudi zake bali ni matokeo ya juhudi za wana CCM na wabunge wote.

“CCM si chama cha viongozi ni chama cha wanachama wote, chama chetu bado ni imara na kinakubalika na kuheshimika ndani na nje ya nchi, chama ambacho ni bora kwa muundo wake,” amesema Kinana.

Amesema chama hicho kimekamilisha chaguzi za jumuiya na kazi iliyo mbele ni kuhakikisha inatekeleza mambo matatu.

Ameyataja kuwa ni kutimiza ahadi kwa Watanzania kama zilivyo katika ilani; kujiandaa na uchaguzi wa serikali za mitaa mwakani; na kujiandaa na uchaguzi mkuu ujao.

Kinana amesema, “Serikali ikitimiza ahadi zake kwa wananchi, itaendelea kuaminika na serikali ikipokea matatizo ya wananchi na kutimiza yale wanayoyataka, watafarijika na mtaendelea kuchaguliwa kwa idadi kubwa na mwisho wa siku CCM itapata ridhaa ya kuendelea kuongoza.”

Amesema ili kuendelea kupata ushindi inapaswa kuendeleza sera kwa kuwasikiliza wananchi, kuwa karibu nao na kuchukua hatua kutatua matatizo yanayowakabili, yanayowasumbua na yanayowaudhi ili wasipoteze mapenzi kwa chama chao na viongozi wao.

“Kuna wakati wa kuchukua dhamana na kukubali kuondoka, kuna wakati wa kukubali kazi moja na kwenda kufanya nyingine, kuna wakati wa kufanya kazi na kuna wakati wa kupumzika. Nimeamua kwenda kupumzika,” amesema.

“Nampongeza Bashiru Ally kwa kuteuliwa na ninamtakia kila la kheri katika dhamana hii, sina shaka hata kidogo ndugu Bashiru atapata ushirikiano mkubwa,” amesema.

Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema alichozungumza Kinana ni funzo.

"Katika uongozi wa kisiasa, hakuna heshima kubwa kama itafika mahali wewe mwenyewe, tena katika wakati uko juu unafanya vizuri kabisa unasema inatosha, hili ni funzo zuri ambalo Komredi Kinana amelifanya na sisi viongozi tujifunze hilo,” amesema.

“Wabunge wengi tunaondoka kinyemela, tunasubiri hadi mageziti yaandike Ndugai chali, sasa hayo yasitufike, tufanye kama ndugu yetu Kinana. Hii ni historia kubwa na utaingia katika vitabu vya kihistoria,” amesema.