Mapya siku moja baada ya Nassari kuvuliwa ubunge

Muktasari:

  • Baada ya uamuzi huo, Mbowe alisema amemuagiza Nassari kuzungumza na wananchi na wanachama wa jimbo lake kuwaeleza kilichotokea kazi ambayo imeelezwa kwamba ataifanya leo.

Katika mkutano huo, Mbowe alizungumzia suala la Joshua Nassari kupoteza sifa za kuwa mbunge wa Arumeru Mashariki akisema akiwa kiongozi wa shughuli za upinzani bungeni, anatambua kwamba alikuwa anahudhuria vikao.

Juzi, Nassari alipoteza sifa za kuwa mbunge na Spika Job Ndugai kuiandikia barua Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) akiieleza kuwa jimbo hilo lipo wazi hivyo iendelee na mchakato wa kuitisha uchaguzi.

Spika Ndugai aliitaja mikutano hiyo kuwa ni wa 12 ulioanza Septemba 4 hadi 14; Novemba 6 had 16, 2018 na wa Januari 29 hadi 9.

Baada ya uamuzi huo, Mbowe alisema amemuagiza Nassari kuzungumza na wananchi na wanachama wa jimbo lake kuwaeleza kilichotokea kazi ambayo imeelezwa kwamba ataifanya leo.

Wananchi wazungumza

Hatua hiyo ya Nassari imepokewa kwa hisia tofauti mkoani Arusha. Wakati wanaCCM wakipongeza, Chadema wameeleza kushtushwa wakitaka ukweli wa jambo hilo kuwekwa wazi.

Katibu mwenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Shabani Mdoe alisema Nassari amevuna alichopanda kwani alitaka ubunge ili kutekeleza masilahi yake badala ya kuwatumikia wananchi.

Wakati Mdoe akisema hayo, mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Arumeru Mashariki, Gadiel Mwanda licha ya kueleza kusikitishwa na uamuzi wa Spika, aliwataka wapigakura wake kuwa watulivu kwa kuwa suala hilo linashughulikiwa.

Baadhi ya wakazi wa wakazi wa Arumeru Mashariki waliohojiwa kuhusiana na hatua hiyo, walitaka ukweli wa jambo hilo ujulikane.

Jeremiah Kaaya, mkazi wa Usa River wameupokea uamuzi wa Spika kwa sura mbili. Kwanza, kutaka wabunge wawajibike lakini pia huenda kuna mambo ya kisiasa.

Elias Pallangyo wa Kikatiti, alisema Nassari amekuwa kimya kwa muda mrefu, hivyo kama alikuwa na matatizo ya kifamilia alipaswa pia kuwaeleza wananchi na Bunge.

Sio Bunge tu

Licha ya kutohudhuria mikutano mitatu ya Bunge na hivyo kupoteza kiti chake, imeelezwa pia kwamba katika Nassari hakuwa na mahudhurio mazuri katika vikao vya kamati ya ushauri Mkoa wa Arusha (RCC) na na vingine muhimu.

Ofisa habari katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Alice Mapunda alisema katika vikao vya mwisho wa mwaka huu, Mbunge huyo hakuonekana.

Nyongeza na Mussa Juma Arusha