Aweso: Sitaki ‘kutumbuliwa’ na Rais Magufuli

Muktasari:

  • Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akataa 'kutumbuliwa' na Rais John Magufuli. Azipa kazi ya kufanya mamlaka za maji Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani kushughulikia changamoto za maji.

Pwani. Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema hayupo tayari  kutimuliwa na Rais John Magufuli kwa kushindwa kupeleka huduma za maji kwa wananchi.

Kauli ya Aweso imetokana na kusuasua kwa utekelezaji wa miradi ya maji katika wilayani Kisarawe mkoani Pwani licha ya bajeti iliyopo.

Akizungumza leo Jumanne Januari 22, 2019 wakati wa ziara ya kikazi katika wilaya hiyo, Aweso amesema Rais Magufuli alipomteua alimpa jukumu la kuhakikisha maji safi na salama yanawafikia wananchi wote.

Kauli hiyo ya Aweso imetokana na kusuasua kwa miradi ya maji wilayani humo huku mkuu wa wilaya hiyo, Jokate Mwegelo akisema imeshindwa kuendelea kwa kukosa huduma ya maji.

"Tulipoteuliwa katika nafasi hizi Rais alisema anatupa wizara hii ili wananchi wapate maji na wasipopata basi atatumbua na mimi sipo tayari kutumbuliwa," amesema Aweso.

Naibu waziri huyo ameonyesha kutoridhishwa na maendeleo ya miradi ya maji wilayani humo huku bajeti iliyotengwa kutotumika kabisa.

Amemtaka mhandisi wa maji wa wilaya hiyo, Majid Mtili  na Mamlaka ya Maji Safi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa) kuhakikisha wanaongeza kasi ya usanifu wa miradi na kuhakikisha wanatafuta makandarasi wenye vigezo ili kuboresha miradi hiyo.

Naye Jokate amesema wilaya hiyo ipo nyuma kwa maendeleo kutokana na kukosa maji, hali inayowafanya watu kushindwa kuwekeza  eneo hilo licha ya kuwa na rasilimali nyingi.

"Kisarawe kuna potential (fursa) kubwa sana lakini wanauliza kuna maji? Kuna mwekezaji anataka kufungua kiwanda kikubwa cha mihogo lakini anataka maji kwa hiyo maendeleo yanakwamishwa kwa sababu tunakosa hii huduma muhimu ya maji," amesema Jokate.

Wilaya hiyo inatarajia kunufaika baada ya kukamilika kwa mradi wa maji wa Kibamba hadi Kisarawe unaozalisha maji kutoka mtambo wa Ruvu Juu ambao utasaidia kuzalisha mita za ujazo  4080.