Bajeti Madini 2019/20 ni Sh49bilioni

Waziri wa Madini, Doto Biteko akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2019/2020 bungeni jijini Dodoma jana. Picha na Ericky Boniphace

Dodoma. Bajeti ya Wizara ya Madini kwa mwaka 2019/20 ya Sh49.46 bilioni imewasilishwa bungeni jijini Dodoma ikiwa na zaidi ya vipaumbele 10, huku waziri wake, Doto Biteko akitoa maagizo kwa wakuu wa mikoa ambao mikoa yao haijafunguliwa masoko ya madini, kufanya hivyo hilo mara moja.

Wakati Biteko akieleza hayo, Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini iliwasilisha maoni yake ikieleza kusikitishwa na utolewaji wa fedha za miradi ya maendeleo ya wizara hiyo usioridhisha baada ya kupokea chini ya asilimia moja ya fedha zilizotengwa kwenye bajeti ya 2018/2019.

Akisoma maoni hayo ya kamati, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mariam Ditopile alisema kiasi cha fedha za miradi ya maendeleo kilichopokelewa katika kipindi cha kati ya Julai 2018 hadi Februari mwaka huu ni Sh100milioni sawa na asilimia 0.5 ya bajeti yote ya miradi ya maendeleo kwa mwaka 2018/2019 ambayo ni Sh 19.6bilioni.

Wakati fedha za maendeleo mwaka 2018/19 zikitolewa Sh100 milioni pekee, katika bajeti ya 2019/2020 fedha zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo zimepungua kwa Sh12.5 bilioni ikilinganishwa na mwaka 2018/19.

Akielezea mchanganuo wa bajeti, Waziri Biteko aliliomba Bunge kuidhinisha Sh49.46 bilioni ambazo ni pungufu ya Sh9.44 bilioni ya bajeti ya mwaka 2018/19 ya Sh58.9 bilioni.

Alisema kati ya Sh49.46 bilioni, bajeti ya maendeleo ni Sh7.03 bilioni ambazo zote ni fedha za ndani na Sh42.42 bilioni ni za matumizi ya kawaida ambapo Sh16.47 bilioni ni za mishahara na Sh25.95 bilioni ni matumizi mengineyo.

Katika bajeti ya mwaka 2018/19 ya Sh58.9 bilioni ilikuwa na ongezeko la Sh6.5 bilioni ikilinganishwa na ya mwaka 2017/18 ya Sh52.4 bilioni.

Kati ya Sh58.9 bilioni, fedha za maendeleo zilikuwa Sh19.6 bilioni na matumizi ya kawaida ni Sh39.2 bilioni.

Akielezea utekelezaji wa bajeti hiyo ya mwaka 2018/19, Biteko alisema hadi kufikia Machi 31 wizara ilikuwa imepokea Sh26.02 bilioni kutoka Wizara ya Fedha na Mipango.

Alisema kati ya fedha hizo Sh25.92 bilioni zilipokelewa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh100 milioni ambazo ni fedha za ndani zilipokelewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Alisema kati ya fedha za matumizi ya kawaida zilizopokelewa, Sh15.4 bilioni zilikuwa kwa ajili ya matumizi mengineyo na Sh10.51 bilioni kwa ajili ya matumizi ya mishahara kwa watumishi wa wizara na taasisi zake.

Ilichokisema kamati

Katika maelezo yake Mariam alisema kutotolewa kwa fedha za maendeleo kumesababisha ucheleweshwaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na miradi mingine kutotekelezwa kabisa.

“Kamati inafahamu kiasi cha Sh 8.6 bilioni kilitengwa kwa ajili ya uchenguaji wa visusu vya dhahabu katika mgodi wa Buhemba na kwamba sasa kiasi hicho kinakusudiwa kutumika kama mtaji wa Stamico pindi mazungumzo na majadiliano ya ubia kati ya mwekezaji na Stamico yatakapokamilika,” alisema.

Alisema kamati hiyo inaona kuwa mazungumzo hayo yamechukua muda mrefu na jambo ambalo linaweza kuleta athari katika uwekezaji huo. Alisema wanaishauri Serikali izingatie utoaji wa fedha za miradi ya maendeleo kama zinavyoidhinishwa na Bunge, ili kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa wakati kama ilivyokusudiwa.

Kutotolewa kwa fedha za maendeleo, miradi ya 2018/19

Katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali ilipanga kufanya mambo 11 ikiwemo kuimarisha ukusanyaji wa mapato yatokanayo na shughuli za madini, kuwaendeleza wachimbaji wadogo na kuhamasisha shughuli za uongezaji wa thamani madini .

Nyingine ni kuimarisha ukaguzi wa usalama, afya, mazingira na uzalishaji wa madini migodini, kuendeleza kuboresha mazingira ya kuwawezesha wananchi kunufaika na shughuli za madini, kuelimisha umma na kuboresha mawasiliano baina ya wizara na wadau wa sekta ya madini. Shughuli nyingine ni kusimamia na kuboresha sera, sheria, kanuni, mikakati na miongozo, kuwaendelea kuvutia wawekezaji wakubwa kwenye sekta ya madini, kuboresha utoaji na usimamizi wa leseni za madini.

Masoko ya madini

Waziri Biteko alisema wakuu wa mikoa waliagizwa kuhakikisha wanafungua masoko ya madini kwenye maeneo yao, lakini bado kuna mikoa haijafungua masoko hayo.

Aliyataja masoko yaliyofunguliwa ni Geita, Kahama, Namanga, Singida, Chunya, Ruvuma, Shinyanga, Katavi, Dodoma, Kigoma, Tabora, Mara, Mbeya, Kagera, Iringa, Mwanza, Songwe, Tanga, Manyara na Singida (Sekenke).

“Nitoe wito kwa viongozi wa mikoa mingine na wilaya ambazo bado hawajatekeleza maagizo na maelekezo hayo ya Serikali kuharakisha taratibu za uanzishwaji wa masoko katika maeneo yao mapema iwezekanavyo,” alisema Biteko.

Wapinzani na mchanga wa madini

Sakata la mchanga wa madini ya dhahabu liliibuka bungeni baada ya upinzani kuhoji kwa nini kampuni ya Accacia hadi sasa inaendelea na shughuli za uchimbaji wa madini nchini, licha ya Serikali kuituhumu kupora rasilimali za nchi.

Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani upande wa Madini John Heche alisema: “Na ikiwa Serikali iliwadanganya Watanzania ni lini itajitokeza hadharani kufafanua jambo hili ambalo limegubikwa na sintofahamu wakati Watanzania wakiendelea kusubiri magari ya Noah nchi nzima kama ilivyoahidiwa na Serikali?”alihoji.