Bila ushiriki wa Tanzania jumuiya ya SADC isingekuwapo

Katibu mkuu mstaafu, Uledi Mussa. Picha na Idara ya habari Maelezo

“Bila ya umoja, Afrika haitakuwa na mafanikio ya baadaye.” Kauli hii iliyotolewa na Rais wa Tanzania kwa wakati huo, Mwalimu Nyerere ndiyo zinayoiishi nchi 16 wanachama wa Jumuiya ya maendeleo ya kusini mwa Afrika (SADC) wanaotarajiwa kukutana jijini Dar es Salaam katika mkutano wa 39 wa wakuu wa nchi na serikali.

Kuwapo kwa SADC ambayo awali ilikuwa inaitwa jukwaa la kuratibu harakati za maendeleo (SADCC) kikiwa chombo cha nchi za mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi na utawala usiozingatia demokrasia kusini mwa Afrika, kulitokana na mchango wa Tanzania katika kuziunga mkono nchi hizo.

Akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu SADC, aliyewahi kuwa katibu mkuu katika wizara kadhaa nchini Tanzania, Uledi Mussa anasema bila ushiriki wa Tanzania iliyochangia kwa hali na mali katika harakati za ukombozi wa Kusini mwa Afrika, huenda SADC ya sasa isingekuwapo.

Uledi anasema hali hiyo inatokana na ukweli kwamba, nchi nyingi zilizounda kundi la nchi za mstari wa mbele, kijiografia, kiuchumi na kijeshi hazingeweza kuhimili vishindo vya serikali ya kibaguzi na mabavu ya Afrika Kusini bila ushiriki wa dhati wa Tanzania.

Kwa mujibu wa Uledi, kundi hilo la nchi za mstari wa mbele baadaye lilijizatiti zaidi kwa kuanzisha jukwaa la kuratibu harakati hizo (SADCC), hususan kujenga uwezo wa kujitegemea kiuchumi na hatimaye kujigeuza na kuwa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Anasema uundwaji wa SADC umepitia nyakati za machungu makubwa enzi za kundi la nchi za mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi na utawala usiozingatia demokrasia kusini mwa Afrika.

Uledi anaeleza kuwa ushirikiano huo wa kikanda ulianza kama kundi la mstari wa mbele mwaka 1980 huko Lusaka nchini Zambia ambako viongozi wa nchi tisa walikutana wakiwamo Mwalimu Nyerere, Samora Machel (Msumbiji), Robert Mugabe (Zimbabwe) na mwenyeji wao Kenneth Kaunda.

Baada ya Namibia kupata uhuru, viongozi hao walikutana mjini Windihoek nchini humo Agosti 17, 1992 walikoamua kuunda upya umoja wao kutoka SADCC na kuanzishwa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika (SADC) ikiwa na malengo kadhaa ya kimaendeleo kuhusu ukanda huo.

SADC ambayo makao makuu yake yako Gaborone, Botswana, malengo yake ni kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi, mtangamano, siasa na ulinzi na usalama na una jumla ya nchi wanachama 16.

Kuthibitisha umuhimu wa Tanzania katika SADC, Desemba 2013 wakati wa mazishi ya Rais mstaafu wa Afrika Kusini na mpigania uhuru wa taifa hilo, Nelson Mandela, Rais wa Tanzania kwa wakati huo Jakaya Kikwete alizungumza namna Tanzania ilivyokuwa na mchango mkubwa kwa ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika.

Alitoa mfano kwamba Januari, 1962 Mandela alifika Tanganyika bila kuwa na hati ya kusafiria na kwamba katika mazungumzo na Mwalimu Nyerere alieleza mpango wake wa kudai uhuru kwa njia ya mapambano.

Kikwete alisema Nyerere aliamua kuwapa sehemu ya kuweka kambi za kuendeshea shughuli zao katika maeneo kama vile Kongwa (Dodoma), Mgagao (Iringa), Mazimbu na Dakawa (Morogoro).

Eneo la Mgagao liko Kijiji cha Kihesa mkoani Iringa lilitolewa na wananchi kwa ushawishi wa Mwalimu Nyerere, kwa ajili ya kuhifadhi wapigania uhuru hao.

Miongoni mwa wapigania uhuru walioishi hapo ni Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela na mkewe, Winnie na Rais wa sasa wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, ambao waliongoza mapambano kutokea Kihesa Mgagao.

Kikwete pia alisema wakati huo vita ya ukombozi haikuwa rahisi kwani wakati mwingine Tanzania mbali na kuwasaidia wapigania uhuru hati za kusafiria, ililazimika pia kuwapa majina ya bandia ili waweze kutekeleza majukumu yao vizuri.

Jitihada za Tanzania katika kuwasaidia wapigania uhuru hazikuishia kwa Afrika Kusini pekee, pia Msumbiji ilinufaika na msaada wa Tanzania hadi ilipopata uhuru wake Juni 25, 1975 kutoka kwa watawala wa Kireno walioupata kwa kupigana vita wakiongozwa Samora Machel.

Kiongozi wa wapigania uhuru wa Msumbiji, Samora Machel alihudhuria mafunzo ya kijeshi ya kujitolea

mjini Dar es Salaam na baadaye alikuwa ni miongoni mwa wapiganaji wa chama cha Frelimo waliopelekwa nchini Algeria kwa ajili ya mafunzo zaidi.

Aliporejea Tanzania kutoka Algeria, Machel aliteuliwa kuongoza kambi ya mafunzo ya wapigania uhuru wa Frelimo iliyokuwa Kongwa mkoani Dodoma.

Machel na wanajeshi wenzake wapigania uhuru waliweka kambi Tanzania na muda mwingine Mwalimu Nyerere alifika katika eneo hilo na kupanga mikakati mbalimbali ya kupata uhuru huo.

Dk Ayoub Rioba ambaye alikuwa mwezeshaji kwenye mafunzo ya hayo, anasema viongozi wa nchi tisa waliokutana Lusaka nchini Zambia mwaka 1980 walikuwa na falsafa muhimu katika kuanzisha SADCC.

Anazitaja falsafa hizo kuwa ni uhuru, usawa, haki, umoja, kujitegemea na maisha mazuri kwa jamii.

Rioba ambaye ni mkurugenzi mkuu wa TBC, anasema umuhimu mwingine wa mtangamano huo ni kulinda utamaduni wa ukanda wa nchi za SADC ambao kwa kiasi fulani unafanana, mfano chakula cha ugali unaoliwa na karibu na mataifa yote, tofauti yake ikiwa ni majina.

Msingi wa SADC

Kanali Wilbert Ibuge kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambaye amefanya kazi kwa muda mrefu makao makuu ya SADC, Botswana anasema msingi wa SADC ni kusimamia malengo yake ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii na yale ya ulinzi na usalama kikanda unabainishwa katika Ibara ya 2 ya mkataba wa SADC.

Anasema katika mkataba huo nchi wanachama waliazimia, kusimamia maendeleo ya kiuchumi ya Kanda kwa kuzingatia baadhi ya malengo ambayo ni kutafuta maendeleo na kukuza uchumi, kuondoa umaskini, kuboresha hali ya maisha ya watu wa kusini mwa Afrika na kuwapa msaada wale waliotengwa kijamii kupitia ushirikiano wa kikanda.

Kanali Ibuge anasema pia nchi wanachama zinatakiwa kuhakikisha ujenzi wa demokrasia inayofuata kanuni zilizokubalika na kuhakikisha maendeleo endelevu.

Anasema mkutano wa viongozi wa nchi na serikali uliofanyika Machi 9, 2001 huko Windhoek, Namibia uliamua kurekebisha muundo wa SADC na hivyo kuidhinisha na kusaini nyaraka mbili zinazoendelea kuziongoza nchi za SADC hadi sasa katika ushirikiano wao wa kikanda.

Marekebisho yaliyofanyika ni kuongeza taasisi za SADC kutoka tano za wakati ule hadi nane na walitia saini mipango miwili.

“Ule uitwao Mpango wa Maendeleo wa Muda Mrefu (RISDP) na Mpango Mkakati wa Taasisi ya Siasa, Ulinzi na Usalama (SIPO),” anasema Kanali Ibuge.

Anasema uhusiano wa mipango mikakati hiyo miwili RISDP na SIPO ni sawa na nyumba, ambayo bila msingi au bila kuwapo kuta na paa, nyumba haiwezi kusimama.

Historia ya mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) inaonesha kuwa kulikuwepo vipindi vya faraja na wakati mwingine machungu. Kuna wakati, EAC ilifikia kiwango kikubwa cha mtangamano wa kiuchumi kiasi cha nchi wanachama wa jumuiya hiyo kuwa na sarafu moja na huduma za pamoja lakini ikavunjika mwaka 1977.

Jumuiya hiyo ya awali ilidumu kwa miaka 10 tu kwa sababu ilivunjika mwaka 1977 kutokana na tofauti za kiitikadi. Kila nchi ilitaka ifaidike zaidi ya nyingine kiuchumi; na mtazamo usio wa kimataifa ambao mara nyingi hudumaza maendeleo ya nchi au kanda husika.

Pamoja na kuvunjika huko kwa Jumuiya ya awali, Tanzania ilichagiza ufufuaji wa Jumuiya hiyo na hatimaye kuanzishwa tena mwaka 1999, Tanzania ikijitolea majengo ya Makao Makuu ya Jijini Arusha.

Vivyo hivyo, uundwaji wa SADC umepitia nyakati za machungu makubwa enzi za kundi la nchi za mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi na utawala usiozingatia demokrasia katika eneo hilo, lakini tanzania ilisimamama kidete zikakombolewa na kuwa pamoja.