BoT kuongeza kibano maduka ya dola

Muktasari:

  • Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeahidi kusimamia kwa uimara maduka ya kubadilishia fedha na kutoa upya leseni kwa maduka wa lengo la kudhibiti utakatishaji wa fedha.

Dodoma. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inakusudia kupitia kanuni inayohusu maduka ya kubadilishia fedha ya mwaka 2015 ili kuimarisha usimamizi wake.

Juni mwaka jana, BoT ilipitia mitaji inayohitajika kwa ajili ya kufungua maduka na iliyataka maduka hayo kuomba upya leseni zao.

Katika masharti hayo, BoT ilipandisha kiwango cha chini cha mtaji kutoka Sh100 milioni hadi kufikia Sh300milioni kwa wenye leseni daraja A na Sh250 milioni hadi Sh1 bilioni kwa wenye daraja B.

Hata hivyo, meneja wa kurugenzi ya sekta ya usimamizi wa Fedha, Nassor Omary aliwaambia waandishi wa habari waliokuwa wakihudhuria semina ya uchumi na biashara jijini Dodoma kuwa kanuni ya mwaka 2015 inayoratibu shughuli za utoaji wa leseni ina upungufu.

Alieleza kuwa katika ukaguzi wa leseni uliofanywa mwaka jana, maduka 107 yalifungiwa kati ya maduka yote 297 yaliyokuwa yakifanya kazi.

“Tumetoa upya leseni kwa maduka hayo kwa lengo la kudhibiti utakatishaji wa fedha na kuhakikisha wale waliopewa leseni hizo wanafanya shughuli zao kwa umakini,” alisema Omary.

Alisema hatua ya hivi karibuni ambayo hata hivyo alikataa kuitaja imethibitisha kuwepo kwa upungufu ambao unatoa mwanya kwa baadhi ya maduka kujihusisha na biashara ya utakatishaji wa fedha na usafirishaji wa dawa za kulevya.

Alisema kutokana na hali hiyo imeonyesha ulazima wa kuipitia upya kanuni ya 2015 ili kudhibiti zaidi.

Meneja huyo alisema BoT ilipitia kanuni ya viwango vya ubadilishaji wa fedha katika maduka, lakini kutokana na matukio ya hivi karibuni, imepanga kufanyia mapitio mengine ili kuongeza udhibiti zaidi.

Alibainisha kuwa BoT inapanga kushirikiana na vyombo vya ulinzi kuchukua hatua zaidi ili tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi.