Dawa ya mbunge kuhutubia tu katika jimbo lake

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Chidilo Kata ya Chipanga wilayani Bahi mkoani Dodoma juzi ambapo wakazi hao walimsimika kuwa Chifu wa Kabila la Wagogo na kupewa jina la Mazengo. Na Mpigapicha Maalum

Rais John Magufuli amesisitiza kwamba mbunge wa haruhusiwi kwenda kuhutubia mikutano ya kisiasa nje ya jimbo lake. Ukiacha ukakasi katika agizo hilo, jambo linalopaswa kutazamwa kwa maslahi ya nchi ni nafasi ya mbunge katika taifa.

Mwalimu Nyerere kwenye miaka ya 70 alisema kwamba wabunge wa Tanzania si wa majimbo; ni wa kitaifa. Hivyo jimbo linawezesha tu mchakato wa uchaguzi kufanyika.

Kutokana na ukweli huo, chama cha UDP tunaamini kwa dhati mfumo wa uwakilishi wa uwiano, tofauti na mfuno wa sasa.

Kwa mfumo wa sasa mshindi anachukua vyote. Maana yake ni kwamba mshindi wa uchaguzi hata kama ni kwa tofauti ya kura moja anachukua kila kitu. Watanzania wameshuhudia mara nyingi ugomvi unaozuka kutokana na tofauti finyu sana ya kura.

Na mfano muhimu ni uchaguzi wa Zanzibar mwaka 1964 ambao ulisababisha Mapinduzi. Utaratibu wa uchaguzi haukuakisi mgawanyo wa kura nchi nzima, hivyo kupelekea ASP kufanya Mapinduzi. Baada ya miaka 50 ya uhuru ni wakati wa kutazama mambo upya kutokana na matatizo mengi tunayokumbana nayo. Mfumo wa uwakilishi wa uwiano ambao kwa Afrika unatumika Afrika Kusini na Namibia ndilo suluhisho.

Katika mfumo huu ni kuwa wananchi wanapigia orodha ya wagombea wa chama kitaifa na si kwenye majimbo kama tulivyozoea. Kinachotokea hapo ni kwamba kila chama kitakuwa na wagombea ambao kinaona wanafaa kukiwakilisha kulingana na matokeo ya kura, hao wanakuwa wabunge.

Mfumo huu unakuwa na faida ya kuvisaidia vyama vingi vidogo, kupunguza rushwa na matumizi makubwa ya fedha kwenye kampeni, kupunguza hisia za ukabila na udini, kuongeza idadi ya wanawake bungeni na kadhalika.

Kutokana na ukweli huu, UDP tunaamini kama ambavyo msomi mmoja alivyopata kutamka miaka ya tisini: “Inaingia akilini kuvipigia kura vyama vya siasa kulingana na sera zao nzuri pamoja na wagombea wabunge wanaofaa kunadiwa kwenye ngazi ya taifa.”