Dk Bashiru amwandikia barua Waziri Mkuu Tanzania, makatibu wa CCM

Monday August 5 2019

 

By Elias Msuya, Mwananchi [email protected]

Mwanza. Katibu Mkuu wa chama tawala nchini Tanzania cha (CCM), Dk Bashiru Ally amemwandikia barua Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Kassim Majaliwa akimtaka afuatilie utekelezaji wa ilani ya chama hicho ya mwaka 2015/20 kwa watendaji wa Serikali.

Mbali na barua hiyo, Dk Bashiru pia amewaadikia barua makatibu wakuu wa mikoa wa CCM akiwataka kufuatilia utekelezaji wa ahadi za chama hicho katika mikoa yao.

Akizungumza jana Jumapili Agosti 4, 2019 katka kipindi na Tuongee Asubuhi kinachorushwa na televisheni ya Star TV, Dk Bashiru ambaye yuko mkoani Mwanza akifuatilia utekelezaji wa ilani ya CCM alisema suala hilo limekuja baada ya kuona mikutano mingi ya Rais wa Tanzania John Magufuli kusimamishwa na wananchi wakimweleza kero zao.

“Aliwaagiza viongozi wake wote kutenga muda kusikiliza kero za wananchi, zinazoweza kubebwa na ngazi ya chini zitatuliwe na zinazotakiwa kupanda kutokana na uzito wake ziende juu,” alisema Dk Bashiru.  

Aliongeza, “Baada ya maagizo yale niliandika barua mbili moja ofisi ya Waziri Mkuu ambaye ni msimamizi wa shughuli za Serikali na ya pili kwa makatibu wote wa chama kusisitiza. Kweli sasa tunaanza kuona mabadiliko.”

Alisema kwa sasa CCM inawashindanisha watendaji wa Serikali kupita na kuangalia hali  ya utekelezaji wa ahadi za Serkali kupitia vikao vya chama na viongozi waliochaguliwa kupitia chama hicho.

Advertisement

Huku akitoa mfano wa baadhi ya wakurugenzi, Dk Bashiru alisema ametoa maagizo kwa mabaraza ya madiwani kuwabana wakurugenzi hao kutoa taarifa za fedha.

“Kwa mfano Segerema (mkoani Mwanza) tuna mkurugenzi pale, Mheshimiwa Rais alitaka kujua bajeti ya Sengerema halmashauri, mkurugenzi ameshindwa,” alisema.

Aliongeza suala hilo lilileta mgogoro miongoni wa madiwani wa halmashauri hiyo.

“Nimeacha maagizo pale waitishe kikao cha madiwani Mkurugenzi aeleze. Hiyo inaleta migogoro kwenye halmashauri, unakuta mkurugenzi anazo taarifa lakini hajaona kama ni za wananchi maana madiwani ndiyo wawakilishi wa wananchi.”

“Pale Shinyanga kulikuwa na mgogoro pale wanasema hata mhutasari wa vikao vyao mkurugenzi anavyoandika sivyo walivyojadili. Pale Shinyanga pia nimeacha maelekezo wambane Mkurugenzi,” aliongeza.  

Aliwataka viongozi wa chama na Serikali kutekeleza maagizo anayotoa Rais Magufuli mikutano anayoifanya au tukuio lolote linalohusu maendeleo.

“Kama Rais anatoa taarifa kwa umma mambo anayofanya, kwa nini anayafanya, yana faida gani, sisi wenzake lazima tumsaidie.

“Wakati anazindua terminal 3 (uwanja wa ndege) ile hotuba inaeleza siyo tu inaleleza anayofanya, lakini pia kwa nchi nzima na faida ya kulipa kodi. Popote kila tukio iwe katika Stiegler’s inakuwa muda wa kueleza nini kinafanywa na Serikali, kina faida gani na kwa nini kinafanywa? Pia ni wasaa wa kuwaomba wananchi watuunge mkono,” alisema.

Advertisement