Dk Mwakyembe: Wanahabari, michezo, burudani hawatamsahau Mengi

Tuesday May 7 2019

Waombolezaji wakiwa ndani ya Ukumbi wa Karimjee

Waombolezaji wakiwa ndani ya Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho kwa marehemu Reginald Mengi 

By Elizabeth Edward, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amesema mchango wa aliyekuwa mwenyekiti mtendaji wa kampuni za IPP, Reginald Mengi hauwezi kusahaulika kwenye tasnia ya habari, michezo na burudani.

Amesema Mengi alikuwa na mchango mkubwa kwenye michezo na kujitolea mara kadhaa kwenye timu ya taifa na vijana kwa kusaidia na kuwa mlezi.

Amemtaja Mengi kama mzalendo aliyeamini katika maendeleo ya taifa lake na alikuwa akifanya kila linalowezekana kuhakikisha maendeleo hayo yanapatikana kwenye taifa lake lenye upendo na amani.

Akitoa salamu za Serikali, Waziri wa Mambo ya Nje, Profesa Palamaganda Kabudi naye alisema kifo cha mfanyabiashara huyo ni pigo kubwa kwa taifa.

“Tumepokea kwa mshtuko taarifa za kifo chake na hali hiyo imetokana na kwamba aliondoka nchini akiwa nzima lakini akiwa kule Dubai akaugua na Mungu akamchukua.”

“Kwa muda wote Serikali kwa kushirikiana na familia ilikuwa ikifuatilia taratibu za mwili wa mpendwa wetu kurejea nchini na hilo limefanikiwa.”

Advertisement

Amesema katika uhai wake, Mengi amekuwa na mchango mkubwa kwa taifa katika masuala mbalimbali aliyoyafanya kwenye elimu, afya, kilimo, madini na sekta ya uchumi kwa ujumla.

“Alishiriki kuinua uwekezaji na kuboresha mazingira ya uwekezaji bila kusita kuwasaidia wawekezaji wazawa kuwekeza nchini,”

“Alitumia muda mwingi kuishauri Serikali jinsi ya kuwashirikisha wazawa na juu ya sera za kiuchumi za nchi yetu,  alikuwa mzawa na mzalendo wa kweli aliyeishi kwenye dhana ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda,” amesema Profesa Kabudi.

Advertisement