Dunia inapomtaka Mobetto kuliko Mama Rwakatare...

Saturday November 17 2018

 

By Dk Levy

CHIBUDI CHIBUDEE. Kachafua hali ya hewa. Kila kitu kimesimama. Akiwa kando ya bwana mdogo Rayvanny. Wamedondosha ngoma iitwayo “Mwanza” iliyovuruga vichwa vya watu kitaa. Na kutikisa bongo za wazee pale Ilala Sharifu Shamba.

Asikuambie mtu. Ngoma ni kali kinoma. Imesambaa na wapo walioielewa na wale wasioielewa. Kifupi ni kwamba mambo ya korosho. Na upuuzi mwingi umesahaulika. Kitaa chote kinaongea juu ya ngoma hiyo. Wimbo umebamba zaidi kwa ukakasi wa maneno yake waliyotumia madogo.

Kwenye daladala ikigongwa huoni kiumbe kiitwacho binadamu kikikaa kimya. Wale wa mikunjo usoni na wale wa tabasamu. Idadi ya wanaoufurahia ni sawa na ya wasioukubali. Picha hiyo utaisikia baada ya wimbo. Wale wa kulalamika na wale wa kutetea.

Sihitaji kuambiwa na mtu kuwa kwenye wimbo kuna kitu cha ajabu. Nimejiridhisha kuwa hakuna cha ajabu. Kama mtu anaona kuna kitu cha ajabu. Basi huyo hana simu janja ‘smartphone’. Mwenye simu ya kisasa akisema ule wimbo haufai ujue ni mnafki mkubwa.

Kama una simu janja naamini utakuwepo kwenye ‘magrupu’ ya whatsApp. Lugha inayotumika kwenye mawasiliano huko tunaijua. Hakuna sehemu watu wanajiachia kama kwenye ‘magrupu’ hayo. Watu ‘wanachati’ kwa lugha chafu na matusi matupu.

Kule watu wako huru kwa sababu ni watu wazima watupu. Na si hivyo tu pia kule siyo hadharani ni muunganiko wa watu walio pamoja. Wimbo huo upo ‘kilokole’ sana ukifananisha na kile kinachoendelea kwenye ‘magrupu’ ya WhatsApp. Watu hawaoni cha ajabu.

Hizi simu unapata kila kitu. Kitu chochote cha hadharani, uchochoroni mpaka gizani unakipata kwenye simu za kisasa. Kupitia simu hizi ndipo unakutana na kitu kinaitwa instagram. Matusi ya instagram, utafananisha na wimbo wa hawa madogo?

Kama hakuna kitu cha ajabu basi Basata walitakiwa wajifikirie adhabu ya kutoa. Wangekataza wimbo kupigwa redioni na runingani. Waache kwingine ngoma igongwe kama kawa. Au wangewataka madogo wafute baadhi ya maneno. Hukumu imekuwa ya kikatili sana.

Wangeishia huko kwingine wangeacha jamii ijiongoze. Kama ni wimbo usiostahili kupigwa hadharani jamii ingejiongeza. Naanzaje kupiga wimbo wa matusi hadharani? Au wanataka kumaanisha kuwa Watanzania wote hawajui baya na jema kasoro ‘stafu’ ya Basata tu?

Ina maana wimbo wote utaharibu watoto? Watoto gani? Hawa wanaokesha kuangalia BET, TRACE, YouTube na chanel nyingi zinazopiga nyimbo za Wamarekani? Kilatini na Kijamaika zenye uchafu zaidi? Wanaoona kaka na dada zao wakifanya ujinga mchana kweupe mitaani?

Hatutaki kukubali kuwa tupo katika vita ya maadili. Kama tumeamua tuamue tu. Kwa kwenda mbali zaidi tufunge na ‘pub’ pamoja na baa za uchochoroni. Kama kweli tunahitaji kulinda maadili ya watoto wetu. Maana huko kuna ujinga wa wazi mwingi, ikiwemo walevi kutongoza vitoto vinavyoishi jirani na vibaa hivi.

Tufute na matangazo ya kondomu. Matangazo ambayo yanasifia kondomu kuwa ina ladha nzuri wakati wa tendo la kujamiiana.

Vita ya maadili

Kila kitu kinachopendwa na ulimwengu wa vijana kinapingwa. Ni kweli kama taifa hatuwezi kukubaliana na kila kinachopendwa na vijana. Lakini hali halisi mtaani inataka nini? Inapenda nini? Jamii yenyewe matendo yake yakoje? Angalia mijadala mitandaoni. Hii ni dunia ya vita ya kimaadili.

Dunia ya sasa inamuhitaji zaidi Hamisa Mobetto kuliko Mchungaji Mama Rwakatare. Lazima tukubali kwamba upepo wa mambo yaliyokuwa ya kijinga siku za nyuma umekuwa mkali sana. Unatusukuma na kutupeleka unakotaka wenyewe na sisi tunaenda kama maboya.

Rostam na “Kibamia”, unadhani wehu? Weusi na “Unanifanya nicum”, ulifikiri hawana akili? Na “Iokote”, ya Maua Sama? Alipitiwa na shetani? “Aibu” ya Nandy ni kichaa? “Katika” ya Navy Kenzo? Hizi nyimbo zote si kwamba watu hawaelewi kinachomaanishwa. Jamii inajua na ndiyo mambo inayoyataka.

Vipi kuhusu “Jibebe” na “Kwangaru” za Wasafi? Utasema hawajielewi? Na unayesema hawajielewi huna lolote zaidi ya kumhifadhi msichana wa kazi “beki tatu” na mshahara wa masimango kibao. Hao unaosema hawajielewi wameajiri mamia ya watu mitaani. Wanafanya jamii inachotaka.

Wimbo haufai ni kweli. Lakini usihalalishe kuupinga kwa kigezo kuwa siwezi kuusikiliza mbele ya wazazi. Kwa sababu hata vipindi vya redio na runinga ni vingi ambavyo siwezi kusikiliza na kutazama mbele ya wazazi. Lugha inayotumika ni ya kipuuzi tu. Lakini jamii ya sasa ndo inataka.

Watangazaji wanajisifia kwa ulevi kwenye vipindi vyao naanzaje kusikiliza mbele ya mzazi? Kuna mengi yanatendeka ambayo siwezi kutazama au kusikiliza si tu mbele ya wazazi bali hata mbele ya wadogo zangu, kuliko huo wimbo wa WCB.

Tupo kwenye dunia ya vita ya maadili.

Sitaki kuhalalisha kuwa wimbo hauna tatizo. Hapana, mimi natatizwa na adhabu iliyotolewa. Kwani wimbo ukiachwa YouTube kuna tatizo gani? Kule ndiko zipo nyimbo chafu zaidi ya hiyo. Sasa utawazuiaje watoto wasiharibiwe na hizo zingine ila ya Rayvanny na Diamond tu?

Basata wamekataza wimbo usichezwe mpaka jukwaani. Shoo nyingi zinafanyika usiku watoto wataharibiwa vipi muda ambao wamelala majumbani? Hivi maneno yale ni hatari kuliko matukio ya kishenzi yanayofanywa na mashabiki kwenye shoo za usiku? Shoo nyingi usiku hutawaliwa na uzinzi.

Dunia inaenda kasi ikiwaacha wazee nyuma mno. Badala ya kupinga kinachofanywa na vijana wa dunia ya sasa. Ni vyema tukawashika mkono wazee wetu. Mwana FA waambie wazee hao, kuwa dunia ya sasa inamuhitaji zaidi Hamisa Mobetto kuliko Mama Rwakatare. Ni vita ya maadili.

Advertisement