‘Fountain garden ndio itakayonitoa’

Wakati mwingine sanaa za mikono zinaweza kumuinua na kumpa mtu kipato cha ziada. Hilo hujitokeza kwa watu wengi kwani kipaji hakipatikani darasani bali kukiendeleza.

Licha ya taaluma yake ya ufundi rangi wa kupendezesha nyumba, Gullam Rajpar (57) ameiona fursa katika utengenezaji wa fountain garden na kuitumia.

Fountain garden ni urembo wa bustani za nyumbani au hotelini zikiwa na nakshi ya kumwaga maji yanayotokea katika mdomo wake maalumu kuelekea chini.

Rajpar ambaye ni mkazi wa Bagamoyo alianza kazi hiyo kwa kukusanya vitu kidogo kidogo kila anapovipata kisha kutengeneza fountain garden moja.

“Kuna wakati nilianza natengeneza lakini kwa sababu sikuwa na masoko ya uhakika na mtaji nikaacha kabla ya kuanza tena mwaka huu kwa sababu niligundua kukata tamaa ni kuua kipaji na ndoto,” anasema Rajpar.

Bustani moja ya aina hiyo, anasema hutengenezwa kuanzia Sh200,000 kutegemea ukubwa na aina anayoipenda mteja.

“Kwa wiki nina uwezo wa kutengeneza mbili zenye ukubwa tofauti na kuzipaka rangi kulingana na mahitaji ya mteja na zipo za kuanzia futi 4 hadi 6,” anasema Rajpar.

Rajpar anasema nguvu nyingi ameziweka katika kutangaza bidhaa hizo katika mitandao ya kijamii ili kuhakikisha anapata wateja wa kutosha.

“Japo bado soko sio kubwa sana lakini moja ya ndoto zangu ni kuhakikisha biashara hii inakua kubwa ili niweze kufika mbali na kuajiri vijana wengi,” anasema.

Wakati akiendelea kuimarisha soko la biashara hiyo mpya, Rajpar anaamini akielekeza juhudi za kutosha, itamuingia kipato cha kutosha kufanikisha mipango yake ya muda mfupi hata mrefu.

“Nahitaji kuongeza umakini na ubora wa bidhaa ili kuwavuta wateja wengi zaidi. Naamini mambo yatakuwa sawa huko mbele,” anasema.