Hawa bado hawajapatikana

Muktasari:

  • Licha ya kupatikana Mohamed Dewji 'Mo' bado Watanzania kadhaa hawajapatikana ingawa muda waliopotea au kutekwa umekuwa mrefu zaidi

Dar es Salaam. Wakati jana Watanzania waliamka na habari njema za kupatikana kwa mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji ‘Mo’, bado kuna maswali kuhusu walipo watu wengine waliotekwa na kupotea.

Mo Dewji aliyetekwa Oktoba 11 katika Hoteli ya Colosseum, Oysterbay jijini Dar es Salaam alipatikana jana saa 7:30 usiku baada ya kutelekezwa na watekaji maeneo ya viwanja vya Gymkhana.

Oktoba 13, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam alisema watu 75 walitekwa katika miaka mitatu iliyopita, ingawa wengi wao walipatikana.

Lugola alisema Serikali itahakikisha watu ambao hawajapatikana wanapatikana na waliohusika wanachukuliwa hatua kali.

Hata hivyo juzi, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro akijibu swali la waandishi wa habari kuhusu kupotea kwa watu katika mkutano wake na wanahabari alisema si kila anayepotea huwa anakuwa ametekwa.

Alisema wakati mwingine mtoto akipotea wiki mbili, mzazi hujitokeza na kusema katekwa na watu wengine huwaaga wake zao na wasiporudi nyumbani hudaiwa wametekwa.

Mwananchi linakuchambulia watu ambao wamekuwa wakitajwa zaidi na jamii kutokana na mazingira yao ya kupotea.

Watu hao ni pamoja na Simoni Kanguye, Ben Saanane, Azory Gwanda, Idrissa Ally na Dewji, ambaye tayari amepatikana.

Ben Saanane aliyekuwa msaidizi wa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alipotea katika mazingira ya kutatanisha Novemba 18, 2016 na hadi jana haijafahamika kama alitekwa au kupotea.

Ben Saanane ametimiza siku 701 sawa na mwaka mmoja na miezi 11 tangu alipotoweka katika mazingira ya kutatanisha.

Novemba 14, 2016 ndiyo ilikuwa siku ya mwisho kwa Ben kuonekana ofisi za makao makuu ya Chadema yaliyopo Ufipa wilayani Kinondoni, Dar es Salaam ambako alitumia muda wake mwingi.

Siku hiyo alisaini kitabu cha mahudhurio ya watumishi wa ofisi hiyo na kufanya shughuli zake za kichama. Hiyo ikawa siku yake ya mwisho kuonekana.

Mwingine ni Kanguye, ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibondo mkoani Kigoma aliyetoweka katika mazingira ya kutatanisha Julai 20, 2017.

Hadi jana, Kanguye alikuwa ametimiza siku 457 sawa na mwaka mmoja na miezi miwili tangu alipotoweka machoni mwa ndugu, jamaa na marafiki zake.

Mei 4, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), Zitto Kabwe akichangia bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa 2018/19, alizungumzia matukio ya utekaji na kupotea kwa watu.

Kuhusu Kanguye, alisema aliitwa ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Kibondo kukutana na DSO na tangu hapo hajaonekana tena.

Zitto, ambaye ni kiongozi wa ACT Wazalendo alilieleza Bunge kuwa kama mhimili huo ungekubali kuchunguza kupotea kwa Ben Saanane, labda Kanguye ambaye ni diwani wa CCM asingepotea.

“Sisi wabunge hatukutimiza wajibu wakati wa suala la Ben Saanane, tuutimize sasa kwa kuchunguza matukio haya ya watu kupotezwa huku vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vikihusishwa.”

Mwandishi alivyotekwa

Azory Gwanda, ambaye ni mwandishi wa kujitegemea wa Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL) mkoani Pwani alitekwa na watu wasiojulikana Novemba 21, 2017.

Hadi jana, Azory alikuwa ametimiza siku 333 sawa na miezi 10 na siku 29 tangu alipochukuliwa na watu hao ambao hawajulikani.

Kwa mujibu wa mkewe Anna Pinoni (35), siku hiyo asubuhi watu wanaokadiriwa kuwa wanne wakiwa katika gari aina ya Toyota Land Cruiser nyeupe, walifika katikati ya mji wa Kibiti sehemu ambayo Azory hupatikana mara kwa mara na kumchukua.

Katika taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Francis Nanai kuelezea tukio la mwandishi huyo alisema baada ya kumchukua, gari hilo lilielekea shambani kwake saa nne asubuhi na kumkuta mkewe Anna akiwa huko.

Alieleza kuwa Azory aliyekuwa amekaa kiti cha nyuma alimuita mkewe kutokea upande huo wa gari na kumuuliza alikokuwa ameuweka ufunguo wa nyumba yao.

Nanai alisema mkewe alilisogelea gari na kuzungumza naye kutokea dirishani na kumweleza alipouficha ufunguo, huku Azory akimwambia amepata safari ya dharura na kama asingerudi siku hiyo ya Novemba 21 basi angerudi siku inayofuata.

Alisema gari hilo liliondoka na kwenda nyumbani ambako mkewe alieleza kuwa aliporudi alikuta kuna upekuzi umefanyika kwa sababu alikuta vitu viko shaghalabaghala.

Mtoto atekwa ‘kimafia’

Septemba 26, mtoto Idrisa Ally (13) alichukuliwa ‘kimafia’ na mtu asiyejulikana akiwa anacheza nyumbani kwao eneo la Tegeta Masaiti jijini Dar es Salaam.

Idrissa, ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Princes Gate alichukuliwa saa 11 jioni eneo la Tegeta Masaiti akiwa anacheza na wenzake na hadi jana alikuwa ametimiza siku 24.

Mtoto huyo alichukuliwa na dereva mwanaume aliyekuwa katika gari aina ya Toyota IST, ambaye baada ya kuwafukuza marafiki wa Idrissa, alitoa kichupa kidogo kinachodhaniwa ni ‘spray’ na kumpulizia mtoto huyo na kumuingiza mlango wa nyuma wa gari lake.

Bilionea Mo Dewji

Habari nzuri ni kuwa zikiwa zimepita siku tisa tangu atekwe mfanyabiashara maarufu nchini, Mo Dewji amepatikana.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa katika taarifa za awali alidai waliomteka Mo Dewji walikuwa ni raia wa kigeni. Kutekwa kwake kuliifanya familia ya Mo Dewji ambaye ni bilionea kijana Afrika, itangaze donge la Sh1 bilioni kwa yeyote ambaye angefanikisha kupatikana kwa mfanyabiashara huyo.

Juzi, IGP Sirro alisema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na kubainisha gari iliyotumika kumteka Dewji.

Takwimu za miaka mitatu

Oktoba 13, Waziri Lugola aliyewahi kuwa askari polisi akizungumzia takwimu na matukio ya watu kupotea alisema mwaka 2016 kulikuwa na matukio ya watu tisa kutekwa, lakini watano walipatikana wakiwa hai kwa ushirikiano na wananchi huku wanne wakiwa hawajulikani walipo.

Alisema katika kipindi hicho watuhumiwa sita walikamatwa, watano walifikishwa mahakamani na mmoja aliuawa na wananchi.

Alisema mwaka 2017, watu 27 walitekwa, polisi walifanikiwa kuwapata 22 wakiwa hai na wawili wakiwa wamekufa na watatu hawakupatikana.

Waziri Lugola alisema kuanzia Januari hadi Oktoba 11, watu 21 walitekwa na kati yao, 17 walipatikana wakiwa hai na wanne hawakupatikana hadi siku hiyo alipozungumza na waandishi wa habari.

Alisema watuhumiwa 10 walikamatwa na kufikishwa mahakamani.

Kuhusu utekaji wa watoto, Lugola alisema tangu mwaka 2016 watoto 18, wa kiume sita na wa kike 12 walitekwa.

“Watoto 15 walipatikana wakiwa hai, wawili walikutwa wamekufa na mmoja hajapatikana,” alisema Lugola.

Alitaja sababu za utekaji huo kuwa ni za kisiasa, kiuchumi, kulipiza visasi, wivu wa mapenzi na ushirikina.