Prime
Huyu hapa ‘mchawi’ Bajeti ya Serikali
Muktasari:
- Maoni hayo yametolewa siku moja baada ya Serikali kuwasilisha bajeti yake ya mwaka wa fedha 2026/27 ikisubiri mjadala wa siku saba utakaoanza Jumatatu.
Dar es Salaam. Wadau wa biashara na uchumi wamesema Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/27 inaonyesha matumaini kwa Tanzania kuianza safari ya uchumi wa kujitegemea, lakini changamoto kubwa inayoweza kuathiri mafanikio yake ni utekelezaji.
Kwa mujibu wa wadau hao, mafanikio ya mipango ya kuongeza mapato ya ndani, uwekezaji katika uzalishaji na mageuzi yanayolenga kuchochea biashara, yatategemea utekelezaji wa vitendo.
Wamesema bajeti hiyo ya Sh62.3 trilioni imeweka msingi wa kujenga uchumi unaotegemea zaidi rasilimali za ndani kuliko misaada na mikopo ya nje, lakini mafanikio yake yatatokana na namna mipango hiyo itakavyofanyiwa kazi.
Wamesema bajeti hiyo inaweza kuwa mwanzo wa sura mpya ya maendeleo iwapo malengo yaliyowekwa yatasimamiwa kwa karibu, kwa kuwa mafanikio ya bajeti yatapimwa kwa kiwango ambacho ahadi na mikakati iliyowekwa itageuzwa kuwa matendo yatakayochochea ukuaji wa uchumi na kuwanufaisha wananchi.
Maoni hayo yametolewa siku moja baada ya Serikali kuwasilisha bajeti yake ya mwaka wa fedha 2026/27 ikisubiri mjadala wa siku saba utakaoanza Jumatatu.
Utekelezaji
Akizungumza na Mwananchi, Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo cha Serikali za Mitaa Dodoma, Dk Nanzia Mmbaga amesema mafanikio ya Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/27 yatategemea utekelezaji wake.
Amesema msisitizo wa kuongeza mapato kupitia kodi, tozo na ada unaweza kugeuka kuwa mzigo kwa wananchi na wafanyabiashara wadogo ikiwa hautasimamiwa kwa usawa.
Kwa mujibu wa Dk Mmbaga, kinachotakiwa ni kuhakikisha ukusanyaji wa mapato hauathiri uwezo wa wananchi kumudu gharama za maisha na kuendesha shughuli za kiuchumi.
Hata hivyo, amesema bajeti hiyo inaonyesha mwelekeo wa kujenga uchumi unaojitegemea kupitia kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, kuongeza uzalishaji na kuchochea uwekezaji.
“Serikali inalenga kupunguza utegemezi wa misaada na mikopo ya nje kwa kuongeza mapato ya ndani. Kiuchumi, hatua hii ni muhimu kwa sababu inaongeza uwezo wa nchi kupanga na kugharamia vipaumbele vyake vya maendeleo kwa uhuru zaidi,” amesema.
Amesema bajeti hiyo pia imehusishwa na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na inaweka msingi wa uchumi unaojitegemea, lakini mafanikio yake yatategemea nidhamu ya utekelezaji, usimamizi wa matumizi na uwezo wa kulinda wananchi dhidi ya ongezeko la gharama za maisha.
Akizungumzia maeneo yatakayosaidia kufanikisha malengo ya uchumi unaojitegemea, Mtaalamu wa Fedha na Uhasibu wa Chuo cha Serikali za Mitaa, Charles Matekele amesema Serikali imeonyesha utayari wa kuendana na mwelekeo wa dunia katika matumizi ya nishati safi kupitia misamaha ya kodi kwa teknolojia mbalimbali, ikiwemo magari ya umeme.
Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na utegemezi wa mafuta, ambayo bei zake zimekuwa zikibadilika mara kwa mara.
“Sasa ndio mwelekeo wa dunia wa kukabiliana na uchafuzi wa mazingira na ongezeko la bei ya mafuta isiyotabirika. Ukitumia nishati mbadala ya gesi asilia, ya kawaida na umeme, itasaidia kupunguza matumizi ya Serikali,” amesema.
Aidha, amesema bajeti hiyo imeleta nafuu kwa wafanyabiashara kupitia pendekezo la msamaha wa kodi ya mapato kwa mwaka mmoja kwa wafanyabiashara wapya.
Pia amepongeza ongezeko la kodi kwenye michezo ya kubahatisha, akisema hatua hiyo inaweza kusaidia kuwaelekeza vijana kwenye shughuli za uzalishaji badala ya kutegemea njia za mkato za kupata kipato. Hata hivyo, amesisitiza kilichobaki ni utekelezaji.
“Nilitamani kodi ipande zaidi kidogo, kwa sababu vijana wengi ni kama vile wameathirika na ‘betting’ ili kupata fedha za chapu chapu badala ya kujishulisha na shughuli za kiuchumi na maendeleo,” amesema.
Mfumuko wa bei
Katika hilo, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Dk Felix Nandonde, amesema pamoja na bajeti kubeba hatua zitakazochochea ukuaji wa uchumi na kusaidia kudhibiti mfumuko wa bei, bado kuna haja ya kuangalia baadhi ya changamoto zinazoweza kuathiri utekelezaji wake.
Moja ya maeneo hayo amesema ni utegemezi wa mbolea kutoka nje ya nchi.
“Hangaiko tunalokwenda kukabiliana nalo ni hatua ya Tanzania kutegemea asilimia 80 ya mbolea yake inayoagizwa nje. Kwa namna ulimwengu unavyoyumba hivi sasa ni wazi, ili kukabiliana na mfumuko wa bei ni lazima tupunguze uagizaji wa mbolea nje ya nchi,” amesema.
Dk Nandonde amesema kwa siku za karibuni mbolea imekuwa ikipanda bei na mfumuko wa bei katika mataifa yanayoendelea unachangiwa kwa kiasi kikubwa na kupanda kwa gharama za chakula, hivyo kuna kazi kubwa ya kufanya.
Hata hivyo, amesema moja ya maeneo ya kupongezwa ni msisitizo uliowekwa katika matumizi ya mifumo ya kidijitali kwenye malipo na hatua za kubana matumizi ya Serikali.
“Kwa muda mrefu limekuwa likizungumzwa, hata Rais (Samia Suluhu Hassan) amekuwa akilisema ni matumizi ya mitandao katika malipo, katika bajeti hii lipo, ni hatua nzuri itakayoleta mabadiliko makubwa,” amesema.
Dk Nandonde, amesema bajeti hiyo imeleta ahueni kwa wananchi wa kipato cha chini, hususan vijana, wanawake na wenye ulemavu kupitia fursa za mikopo.
Bado kuna shida
Kwa upande wake, Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), Dk Rogers Andrew amesema bajeti hiyo ni ya kwanza katika utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050, lakini haijaakisi malengo ya dira hiyo.
“Bado haijaakisi malengo, kwa mfano sekta ya kilimo bajeti imepungua asilimia 10, wakati kilimo ndio mhimili mkubwa wa kufikisha dola 7,000 kwa kila Mtanzania. Sasa tukianza kwa kulegalega, tutakuwa tunalegalega kila mwaka na kushindwa kufikia malengo,” amesema.
Kutokana na hilo, mtaalamu huyo wa uchumi, amesema wabunge katika michango yao wanatakiwa kuboresha sekta za uwekezaji na uzalishaji si katika matumizi, ili bajeti hiyo iakisi malengo yaliyokusudiwa.
Wafanyabiashara
Akizungumzia bajeti hiyo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Severini Mushi amesema hatua zilizochukuliwa ni njema kwa wafanyabiashara, hasa wanaotamani kuanzisha biashara mpya, ambao wamekuwa wakikwamishwa na kodi mwanzo wa biashara.
Amesema miongoni mwa mambo yaliyokuwa yakilalamikiwa kwa muda mrefu ni gharama za leseni na baadhi ya tozo za mamlaka za serikali za mitaa, ambazo ziliwakatisha tamaa wafanyabiashara wadogo kuingia kwenye mfumo rasmi.
“Kwa upande wetu tunaona huu ni mwanzo mzuri, tumekuwa tukishauri kwa muda mrefu kuhusu baadhi ya changamoto zinazowakabili wafanyabiashara.
“Kuna maeneo ambayo tayari yamefanyiwa kazi na tunashukuru, lakini bado yapo mambo ambayo tuliyawasilisha na hayajapatiwa ufumbuzi wa mwisho,” amesema Mushi.
Wananchi wanasemaje
Mmiliki wa duka la bidhaa mchanganyiko katika eneo la Mbagala jijini Dar es Salaam, Hassan Mussa amesema kupungua kwa misaada kutoka nje ni changamoto inayopaswa kufanyiwa Tanzania kujitegemea zaidi.
“Kwa miaka mingi tumekuwa tukisikia kuhusu misaada na mikopo. Kama Serikali sasa inaamua kuongeza mapato ya ndani, hilo ni jambo zuri. Lakini kinachotakiwa ni kuhakikisha mzigo hauhamishiwi kwa wafanyabiashara wadogo kupitia kodi nyingi zaidi,” amesema.
Amesema hatua ya kutumia teknolojia za kisasa kama Akili Unde (AI) na Big Data katika ukusanyaji wa mapato inaweza kusaidia kudhibiti ukwepaji kodi kwa wafanyabiashara wakubwa badala ya kuwabana wale wadogo ambao tayari wanakabiliwa na changamoto za mtaji.
Kwa upande wa muuza nguo Kariakoo, Judica Mwaipopo, amesema mpango wa kutoa msamaha wa kodi kwa wafanyabiashara wapya kwa mwaka mmoja itawavutia vijana wengi kuanzisha biashara rasmi.
“Vijana wengi wanaogopa kusajili biashara kwa sababu wanaona wakisajiliwa tu wanaanza kufuatwa na kodi. Hii ya mwaka mmoja bila kodi inaweza kuwapa nafasi ya kujijenga kwanza,” amesema.
Hata hivyo, amesema Serikali inapaswa kuandaa utaratibu rahisi wa usajili wa biashara ili watu wengi zaidi waweze kunufaika na mpango huo.
Akizungumzia malipo ya mtandao, mwendesha teksi mtandao jijini Dar es Salaam, Rajabu Salum, amesema matumizi hayo yanaweza kuongeza usalama na kurahisisha biashara lakini ipo haja ya kupunguza gharama za miamala ili isiwaumize wananchi.
“Kwa upande wa teksi mtandao tayari wengi tunatumia malipo ya simu na benki. Hii itasaidia kupunguza hatari ya kubeba fedha taslimu, lakini wasisahau kuna gharama za miamala wakati mwingine mtu anakwepa kulipa kidijitali kukwepa hizo gharama hivyo ziangaliwe,” amesema Salumu.
Hilo limeelezwa pia na Lucy Lupogo: “Hili suala la malipo kimtandao ni jambo zuri ila tatizo linakuja pale yanapoongeza gharama,” amesema.
Kuhusu matumizi ya magari yanayotumia umeme na gesi, Salum Omary ambaye ni dereva wa daladala amesema hatua hiyo inaweza kusaidia kupunguza gharama za mafuta ambazo zimekuwa zikiongezeka mara kwa mara.
Hata hivyo, amesema bado gharama za kununua magari hayo ni kubwa kwa wananchi wa kawaida.
“Gharama kubwa tunayokutana nayo ni mafuta. Kama magari ya umeme yatakuwa nafuu kuendesha, yatatusaidia sana. Kinachotakiwa ni kuwe na mikopo au ruzuku zitakazowezesha watu wengi kuyanunua,” amesema Omary.
Naye, John Mrema, muuzaji wa vipuri vya pikipiki amesema msamaha huo unaweza kuwa kichocheo kikubwa kwa vijana wanaomaliza vyuo lakini wanakosa ajira rasmi.
"Vijana wengi wanataka kuanzisha biashara lakini mtaji ni mdogo. Ukiondoa mzigo wa kodi kwa mwaka wa kwanza unawapa nafasi ya kuelekeza fedha hizo kwenye kukuza biashara. Hilo linaweza kusaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa kiasi kikubwa," amesema Mrema.
Bima ya afya
Suala jingine lililovutia maoni ya wadau ni la bima ya afya, ambapo Rais wa Chama Cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko, amesema Serikali tozo za kuigharimia ni hatua muhimu ya kupongezwa.
"Afya ni uwekezaji, afya ni haki ya msingi, ni wajibu wa Serikali, ni usalama wa Taifa, si anasa wala hiari, hivyo bado tunaomba vikwazo vyote vinavyofanya wananchi wasipate huduma za afya bora na salama viondolewe, vikiwemo vikwazo vya kiuchumi miundombinu na kadhalika," amesema.
Amesema kunahitaji kasi katika utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote kwa viongozi kufanya uamuzi ili kuwanausuru wananchi wanaohangaika kupata huduma za afya
Amesema afya haina awamu, haisubiri miongozo kwani huo ni uhai ambao hausubiri mijadala.
"Bajeti hii tunaomba ikidhi haja za wananchi, iimarishe huduma za afya, iboreshe maisha ya wananchi, ikazie usalama na ubora wa huduma za afya, Ijenge mifumo imara ya afya, idhibiti maradhi. Iwahakikishie wananchi wote upatikanaji wa huduma za afya," amesema.
Dk Nkoronko, amesema bajeti ya Serikali iimarishe ushirikiano wa taasisi za uma na binafsi, iweke mkazo kwenye uwekezaji wa uzalishaji wa dawa na vifaa vya kutolea huduma.
Pia, amesema ilete tija na siha njema kwa makundi yote, ushirikiano imara na wadau na kuhakikisha usalama dhidi ya magonjwa ya milipuko.
Hata hivyo, amesema: "Magonjwa yasiyoambukizwa yanahitaji makati wa pekee, sheria imetaja kutakuwa na mfuko maalumu wa kugharimia tiba za magonjwa haya. Mpaka sasa mfuko huo bado haujatengewa fedha,nina imani Bunge litatimiza wajibu wake kikamilifu kwa kuipa afya nafasi na kipaumbele inachostahili," amesema.
Mchango katika sekta hiyo pia unatolewa na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Chama cha Wamiliki wa Vituo Binafsi vya Afya Tanzania (APHFTA), Dk Samwel Ogillo aliyesema ni hatua nzuri imechukuliwa na Serikali kuongeza kodi katika bidhaa ambazo zinaathiri afya ya binadamu.
"Sisi watoa huduma za afya binafsi tunapongeza hatua hizi kwa sababu bidhaa hizi ndio zinaleta changamoto kwenye afya. Sukari ni chanzo kikuu cha magonjwa yasiyo ya kuambukiza na yale ya kuambukiza, watu hawapaswi kutumia sukari kwa wingi, sigara inafahamika kuwa ni tatizo kwa afya zetu," amesema.
Dk Ogillo, amesema sigara ni kichocheo kikubwa ya maradhi ya saratani kwenye mwili wa binadamu, hivyo ushuru wake unapaswa kuongezwa zaidi ili watu waziepuke.
Amesema hata bajeti inayofuata Serikali inapaswa kuangalia zaidi ongezeko la ushuru kwenye pombe ili kusaidia afya za wananchi.
"Fedha hizi zote zitakwenda kugharamia huduma za afya kwa makundi yasiyo na uwezo hata mataifa mengine yanafanya hivyo, ni Serikali tu ilitumia busara ikatoa fedha," amesema.