IST, Volkswagen ni usafiri wa wanyonge?

Thursday June 6 2019

 

By Padri Privatus Karugendo

Baada ya kusikiliza kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda akiponda usafiri wa gari la IST kwamba ni wa watu baki au wanyonge, nimeshangaa sana na kujiuliza maswali mengi.

Huyu ni kiongozi kwenye serikali inayojitambulisha ya wanyonge, hivi kauli yake inawalenga wanyonge? Ya kuwatetea na kusimama nao. Kusema kwamba IST ni gari la watu wa kuhongwa maana yake ni nini?

Ina maana ameteleza au ndio hivyo ilivyo? Wakoloni walipoleta elimu yao, walileta inayowasaidia kututawala, inayotufanya tusijitambue nafsi zetu badala yake tujitambue kama watumishi. Ndiyo maana kuna mapendekezo kwamba kama tunataka kujenga Tanzania ya watu wanaowajibika kama raia, tunatakiwa kubadili mtaala wetu na kuongeza somo linalowafundisha wanafunzi kujitambua. Mambo ya kufundishwa yangekuwa kama vile haiba. Hapo wanafunzi wajifunze kutambua upekee wa kila mmoja, ukuaji wao kimwili, kimaono, kijamii na nafasi ya familia katika ukuaji wao.

Wafundishwe uzalendo, kulipenda taifa, kuipenda lugha yao, kulinda rasilimali za taifa na viwanda.

Mfano nchi zinazotuzunguka za Kenya na Uganda, watu wanajua kulinda bidhaa za nchi yao. Wana tofauti za kisiasa, lakini katika kujenga uchumi wanakuwa na lugha moja.

Somo kama hili lilimsukuma mtu kama Hitler kufikiria kutengeneza Volkswagen. Alitambua umuhimu wa kila Mjerumani kuwa na usafiri. Uchumi haukuwa mzuri na watu hawakuwa na fedha, hivyo alifikiria gari ambalo kila Mjerumani angeweza kulimudu. Volkswagen, neno la Kijerumani – linalounganisha maneno mawili. Volk (watu) na Wagen (gari) – yaani gari la watu, ambalo kila mtu anaweza kulinunua.

Advertisement

Kwa uvumbuzi huu, Ujerumani ilipona kutumia pesa za kigeni kuagiza magari ya bei kubwa kutoka nchi za nje.

Wakati Makonda anabeza IST na kushabikia magari ya kifahari, Hitler alifikiria kuwa na gari la watu wote. Wakati serikali ya awamu ya tano inajitangaza kuwa ni wanyonge, kiongozi wa ngazi ya juu anapoubeza unyonge, ni dalili za usaliti au kuteleza?

India inawalazimisha watu wake kutumia magari yaliyotengenezwa India. Serikali ya India, inazuia nchi hiyo kutumia fedha za kigeni kununulia magari ya kifahari kutoka Japan na kwingineko. Kwa kufanya hivyo India, inalinda viwanda vyake na kutunza pesa za kigeni kwa mambo mengine muhimu.

Nchi nyingi duniani, zilizoendelea na zinazoendelea, zinajitahidi kuuza vitu nje kuliko zinavyonunua. Hata zikinunua, zinanunua vitu vya lazima na nafuu.

Huwezi kukuta nchi hizi zinaagiza magari ya kifahari au simu za bei mbaya kutoka nchi za nje.

Sisi kwa vile tunafuata elimu ya kikoloni, inayotuandaa kuwa watumishi na soko la wakoloni, bado tumeshindwa kutengeneza volkswagen yetu. Tunashabikia magari ya bei kubwa na kuyatukana ya bei nafuu.

Tunaendelea kutumia pesa za kigeni kuagiza magari ya kifahari. Serikali inanunua magari ya kifahari kutoka nchi za nje. Ina maana gani nchi inayojiita masikini kununua gari moja

Suluhisho si kubadilisha mitaala tu bali hata na wale waliosoma zamani, kuna haja ya kuwarudisha shule.

Maana kuna mambo yanayochanganya mpaka mtu ukaanza kujiuliza elimu tunayopata inatusaidia nini.

Advertisement