VIDEO: Jenerali Mabeyo atoa onyo kwa wanaotoa kauli tata

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Venance Mabeyo akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Mji wa Serikali uliopo Mtumba, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Mkuu wa Majeshi, Jenerali Venance Mabeyo ameonya kuwa jeshi linafuatilia kauli tata za uchochezi zinazolenga kuibua machafuko ndani ya nchi

Dar es Salaam. Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Tanzania, Jenerali  Venance Mabeyo amesema jeshi la Wananchi wa Tanzania linafuatilia  kauli tata zinazoashiria uchochezi na kuhatarisha kuibua machafuko ndani ya nchi.

Amesema jeshi hilo pia lipo tayari kukabiliana na machafuko ambayo yanaweza kujitokeza kutokana na uchochezi huo.

Jenerali Mabeyo ameeleza hayo leo wakati wa hafla ya  uzinduzi wa mji wa kiserikali uliojengwa Ihumwe mkoani Dodoman ambao utazinduliwa na Rais wa Tanzania, John  Magufuli.

Amesema hali ya nchi ni shwari ila jeshi linaendelea kuimarisha ulinzi wa wananchi na mali zao kuhakikisha amani inaendelea kutawala.

“Hali ya usalama kwenye mipaka yetu ni shwari, ndani ya nchi yetu JWTZ kwa kushirikiana na vyombo vya wengine liko tayari kuwalinda wananchi na mali zao, wakati wote tupo tayari kukabiliana na matishio yoyote yanayojitokeza," amesema.

Kuhusu ujenzi wa nyumba na ofisi za Serikali, Jenerali Mabeyo amesema kwa kiasi kikubwa kazi hiyo imefanywa na vijana wa JKT na imefanyika kwa miezi mitano.

Amesema kwa kuwatumia vijana hao, Serikali imeokoa takribani Sh2.1 bilioni,  huku akieleza kazi yote hiyo imefanyika kwa Sh5 bilioni.

“Mheshimiwa Rais vijana hawa wamefanya kazi kubwa sana, naomba kwa ridhaa yako utoe neno lolote la kuwafariji ila kwa upande wa maofisa nitaomba ruksa yako niwafanyie kitu na askari ambao wameajiriwa hao nitajua cha kuwafanyia,” amesema.

Awali, Waziri Mkuu Mstaafu, Samuel Malecela alimpongeza Rais Magufuli kwa kufanya uamuzi wa kuhamishia makao makuu ya Serikali katika mji wa Dodoma.

Amesema kwa uamuzi huo watu wa Dodoma hawawezi kumsahau Rais Magufuli kwa kuwapelekea heshima hiyo kubwa.

“Najua hupendi kusifiwa lakini kwa hili nakwambia watu wa Dodoma kila siku tutakukumbuka maana ukitaja makao makuu ya Serikali tutakutaja Magufuli,” amesema.

Kwa upande wake, Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema Serikali kuhamia Dodoma imerahisisha utendaji wa Bunge.

“Kazi ya Bunge imekuwa rahisi maana kila anapohitajika kiongozi wa Serikali inakuwa rahisi kumpata kwa wakati, tunaahidi kuendelea kufanya kazi na Serikali na hata inapotekea tunarusha mawe msijisikie vibaya ndio kazi tuliyopewa na wananchi,” amesema.