Jinsi kero 11 za madini zinavyoshughulikiwa

Thursday May 30 2019

 

By Tumaini Msowoya, Mwananchi [email protected]

Suala la Joseph Temba, mchimbaji mdogo wa madini mkoani Shinyanga kuuza almasi ya Sh3.2 bilioni ni habari iliyopokelewa kwa furaha na wengi.

Licha ya kwamba taarifa hiyo inamuweka Temba kwenye orodha y amabilionea kuanzia sasa nchini, Serikali imekusanya kodi kutokana na mauzo hayo yaliyofanyika katika soko la madini la Mkoa wa Shinyanga.

Temba ni miongoni mwa mamilioni ya Watanzania wanaonufaika na uchimbaji mdogo wa madini wakati Serikali, kwa muda mrefu, ikiyategemea kuiingizia fedha za kigeni.

Kwa mwaka ulioishia Machi 2019, taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaonyesha uuzaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi uliongezeka na Dola 8.54 bilioni zikilinganishwa na Dola 8.48 bilioni zilizopatikana kipindi kama hicho mwaka 2018. Uuzaji wa madini hasa dhahabu uliokua kwa asilimia 9.8 ulichangia Dola 1.68 bilioni katika kipindi hicho.

Madini ni kati ya sekta nyeti inayotegemewa kukuza uchumi wa Tanzania. Licha ya umuhimu wa sekta hiyo, Sheria ya Madini ya mwaka 1979 na 1998 zilitoa manufaa zaidi kwa wawekezaji.

Kutokana na hali hiyo, wananchi walipiga kelele kupokwa urithi wao hivyo kuilazimu Serikali kuchukua hatua.

Advertisement

Katibu mtendaji wa tume ya kurekebisha sheria nchini, Casmir Kyuki anasema malalamiko hayo yalichangia kuundwa kwa kamati mbalimbali ikiwamo ya Jaji mstaafu Mark Bomani na maboresho ya sheria yaliyofanyika mwaka 2017 yakilenga kuirejesha raslimali hiyo mikononi mwa mwanchi.

Katika hoja zilizokuwa zinatolewa, Kyuki anasema kulikuwa na maeneo 11 yaliyolalamikiwa zaidi. Maeneo hayo ni pamoja na Taifa kutokuwa na umiliki wa madini yake, masharti magumu kwenye mikataba, unafuu wa kodi kwa wawekezaji na, wizi na utoroshaji wa madini nje ya nchi.

Mengine ni uhamishaji wa faida, utoroshaji wa fedha na udhibiti hafifu wa maeneo ya machimbo uliorahisisha utoroshaji madini. Vilevile, kulikuwa na ukwepaji kodi kutokana na mikopo kutoka nje, mchango mdogo wa sekta hiyo katika uchumi wa nchi, usimamizi hafifu wa matumizi ya bidhaa zinazopatikana nchini na kutowasilisha taarifa za kijiolojia serikalini.

Wananchi pia walilalamikia leseni zinazotoa haki ya kuhodhi maeneo yenye madini bila kuendelezwa pamoja na uharibifu wa mazingira.

Hatua zilizochukuliwa

Mtendaji Mkuu Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya anasema hatua tofauti zimechukuliwa na zinaendelea kuchukuliwa kumilikisha raslimali hizo kwa Watanzania.

Kutungwa kwa sheria ya madini ya mwaka 2010 na maboresho yaliyofanywa mwaka 2017, ilikuwa ni miongoni mwa hatua za msingi kushughulikia malalamiko hayo.

“Uchunguzi wa kisayansi pia ulifanyika ili kubaini wizi na utoroshaji madini. Sheria inalenga kuwalinda na kuwahamasisha wachimbaji wadogo,” anasema profesa Manya.

Kutokana na mabadiliko yaliyofanywa, mwaka 2017, Serikali ilizuia usafirishaji wa mchanga wa madini kutoka Buzwagi na Bulyanhulu katika Bandari ya Dar es Salaam.

“Madini haya yalikuwa yakisafirishwa bila kulipiwa mrabaha na kodi nyingine,” anasema.

Kuongezea, Kyuki anasema mabadiliko ya mwaka 2017 yaliweka masharti yatakayowawezesha wananchi na Taifa kunufaika zaidi na madini, petroli na gesi asilia.

“Kutokana na mabadilikohayo, makinikia hayatauzwa nje ya nchi bali yataelekezwa kwa wachenjuaji wa ndani na yatatozwa kodi,” anasema Kyuki.

Sheria hiyo pia inalipa Bunge mamlaka ya kupitia, kujadili na kuridhia mikataba ya utafutaji na uendeleaji wa mafuta ya gesi asilia.

Wananchi

Mkurugenzi wa sheria wa Wizara ya Madini, Edwin Igenge anasema mabadiliko ya sheria yamewapa uwezo wananchiwanaozunguka migodi kuchukua hatua za kisheria endapo wataathirika na uchimbaji usiozingatia utunzaji mazingira. “Wachimbaji wanatakiwa kula kiapo cha uadilifu kwamba watafuata sheria za kulinda mazingira na wakikiuka wanaweza kushtakiwa kuanzia na wananchi watakaoathirika,” anasema Igenge.

Pamoja na uwezeshajiwa wananchi wa kawaida, wizara pia inawajengea uwezo wachimbaji wadogo ili waweze kukuza mtaji na kuongeza tija ya shughuli zao.

Miongoni mwa juhudi zinazofanywa ni kuwaunganisha kwenye vikundi ili wakopesheke na taasisi za fedha suala litakaloboresha uchimbaji wao.

Utekelezaji wa sheria

Mtendaji mkuu tume ya madini, Profesa Manya udhibiti utoroshaji na wizi wa raslimali hiyo umeongezeka na mikakati zaidiinaendelea kuwekwa kuhakikisha biashara hiyo inafanywa kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa.

Kwa miezi 10, mpaka Agosti 2013, uliokuwa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) ulikamata watoroshaji 23 wa madini mbalimbali yenye thamani ya Sh13.17 bilioni katika viwanja vya ndege Dar es Salaam, Arusha na Mwanza wakiwamo raia wa kigeni 20.

Miaka miwili baadaye, Februari 2015 wakala huo ulitangaza dau nono kwa atakayewezesha kukamatwa kwa mfanyabiashara yeyote anayesafirisha madini kwa njia za magendo ukisema umezibaini njia za panya zaidi ya 400 zinazotumika.

Aliyekuwa mkurugenzi wa fedha na utawala wa TMAA, Bruno Mteta alisema: “Kuanzia Januari mpaka Desemba mwaka 2014, wakala umekamata watoroshaji wa madini 27. Tunawaomba Watanzania wazalendo kushirikiana nasi kuendelea kuwabaini watu wanaojishughulisha na magendo haya. Zawadi ya asilimia tano ya thamani ya madini yatakayokamatwa itatolewa.”

Profesa Manya anasema ujenzi wa ukuta wa Mirerani umesaidia kuongeza makusanyo ya ushuru na kodi ya Tanzanite. Kati ya Aprili hadi Disemba mwaka 2018, anasema Serikali imekusanya Sh1.43 bilioni.

Tangu umakini uongezwe kwenye usimamizi wa sekta hiyo, anasema madini tofauti yenye thamani ya zaidi ya Sh30 bilioni yaliyokuwa yanatoroshwa, yamekamatwa.

Ndani ya kipindi hicho, anasema Dar es Salaam kumekamtwa vito vya Sh4 bilioni wakati mkoani Geita ikikamatwa dhahabu ya Sh389.7 bilioni, Mwanza dhahabu ya Sh26 bilioni na Tabora ya Sh6 milioni.

“Kwa hiyo ujenzi wa ukuta umesaidia kuongeza mapato na kudhibiti madini yaliyokuwa yakipotea, haya ni mafanikio. Na, mwaka huu 2019 tunatarajia kuongeza mapato zaidi,” anasema Profesa Manya.

Kuongeza udhibiti wa sekta hiyo, wizara inaendelea kuongeza wataalamu wa uthaminishaji madini na udhibiti wa uharibifu uliopo.

Advertisement