Bodaboda Kilimanjaro watangaza kuiunga mkono CCM 2020

Muktasari:

  • Chama cha Wamiliki na Waendesha Bajaji na Bodaboda Mkoa wa Kilimanjaro (CWBK), kimetangaza kumuunga mkono Rais wa Tanzania  John Magufuli katika uchaguzi mkuu utakaofanyia 2020

Moshi. Chama cha Wamiliki na Waendesha Bajaji na Bodaboda Mkoa wa Kilimanjaro (CWBK), kimetangaza kumuunga mkono Rais wa Tanzania  John Magufuli katika uchaguzi mkuu utakaofanyia 2020.

Hata hivyo, chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimedai kushtushwa na msimamo huo na kueleza kuwa ndani ya kundi kuna ambao ni wana CCM, wafuasi wa upinzani na wasio na vyama.

Chama hicho chenye wanachama 4,500 kimetangaza msimamo huo mwishoni mwa wiki katika mkutano wa wamiliki na waendesha bajaji na pikipiki, uliofanyika ofisi za CCM mkoa Kilimanjaro.

Msimamo huo ulitolewa kupitia risala yao kwa mgeni rasmi wa mkutano huo ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola ambaye pia ni Mbunge wa Mwibara kupitia CCM.

Awali risala hiyo ilikuwa isomwe na mwenyekiti wa chama hicho, Bahati Nyakiraria lakini baadhi ya wanachama wakapaza sauti wakipinga, ndipo iliposomwa na Katibu wa UVCCM mkoa, Asia Halamga.

“Tunaomba umpelekee Rais Magufuli salamu zetu za dhati kuwa tunamuunga mkono kwa kazi kubwa anayofanya ya kuwaletea watanzania maendeleo,” inaeleza sehemu ya risala hiyo.

 “Sisi wasafirishaji tunafurahi kwa kutuletea treni ya mizigo na abiria kwani kwetu itakuwa fursa ya kuongeza kipato kwa kutoa huduma za usafiri pale kituoni. Mtoe wasiwasi (Rais) kuhusu chaguzi zinazokuja za Serikali za Mitaa na uchaguzi mkuu. Tutakiunga mkono CCM  kwani kinatetea wananchi wake.”

katika mkutano huo ulihudhuriwa pia na mwenyekiti wa CCM Mkoa Kilimanjaro, Patrick Boisafi na Katibu wa mkoa, Jonathan Mabhia, Lugola alitatua papo kwa hapo, kero mbalimbali za kundi hilo.

Miongoni mwa kero alizoelezwa Lugola ni pamoja na madereva wa Bajaji na Bodaboda kukamatwa  na kupigwa faini ya kuanzia Sh30,000 kwa makosa yanayohitaji kupewa tu elimu.

Kero nyingine ni madereva kukamatwa na kuwekwa mahabusu kwa kushindwa kulipa faini papo hapo, kero ambayo Waziri aliitolea maamuzi kuwa wanapaswa kuandikiwa faini na kulipa ndani ya siku saba.

Mojawapo ya kero aliyoitatua papo hapo ni kuagiza kurejeshwa kwa vituo viwili vya Bajaji vya Kwa Sharifu soko la Mbuyuni na Agakhan karibu na kituo kikuu cha mabasi vilivyofutwa kinyemela.

Pia,  alimwagiza kamanda wa Polisi mkoa Kilimanjaro, Hamis Issah aliyekuwepo katika mkutano huo, kufanyia kazi malalamiko ya rushwa kwa trafiki watatu waliotajwa katika mkutano huo kuwa vinara.

“Matatizo mengi mliyowasilisha kwangu ni yale yanayosababishwa na Halmashauri zenu mbili. Kama ni matatizo ya maegesho viongozi wako hapa kuanzia mstahiki Meya na madiwani,” amesema Lugola.

“Hawa ndio wamewafanya watumwa ndani ya nchi yenu. Fanyeni matengenezo sasa na ni CCM pekee ndio kuna hewa ya Oksijeni. Acheni kutumia hewa ya ukaa mtakufa,”alisisitiza Waziri Lugola.

Waziri Lugola aliwaonya watendaji wa taasisi za Serikali wanaowawekea vikwazo wamili na waendesha Bodaboda na Bajaji, akisema dawa yao inachemka kwani Rais Magufuli hataki mambo hayo.

Chadema Kilimanjaro wanena

Katibu wa Chadema mkoa Kilimanjaro, Basil Lema amesema watamuandikia barua msajili wa Asasi za Kiraia kuhoji uhalali wa CWBK kutoa matamko ya kisiasa ambayo si malengo ya chama hicho.

“Kiukweli tumeshtushwa sana na msimamo ulitolewa Ijumaa. Hatuamini kulikuwa na consensus (makubaliano) katika kuandika hotuba hiyo. Humo ndani kuna wana CCM na upinzani,” amesema.

Lema amedai CCM kimeishiwa mbinu ndio maana kimeamua kucheza rafu kwa kumuita Waziri Lugola kwenda Kilimanjaro kwa kodi ya watanzania, lakini akaenda kufanya kazi za kukiimarisha CCM.

Kwa mujibu wa Katibu hiyo, wanafahamu sababu za CCM kuamua kushika kundi hilo ni kutokana na kuzidiwa na upinzani na kufananisha na mtu anayezama hivyo hata akiona unyoya anaushika.