Kuna zaidi ya aliyoeleza Bashiru kwa Makonda

Thursday June 6 2019

 

By Luqman Maloto

Hakijapita kitambo kirefu tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aibue kauli tata kuhusu kabila la Wachaga na moyo wao wa kujitolea. Ameibua jingine kuhusu watu wenye kumiliki magari aina ya Toyota IST.

Wakati wa mazishi ya Reginald Mengi, Makonda alisema Mengi alikuwa Mchaga wa kipekee, kwani alisaidia walemavu. Namna ambavyo Makonda alifanya uwasilishaji, ilijenga tafsiri kwamba Wachaga ni watu bahili, hivyo Mengi alijipambanua kuwa wa tofauti.

Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally, alimwombea msamaha Makonda kanisani kwa matamshi yake, akasema ni matokeo ya nchi kujiweka kando na ufundaji wa viongozi. Hitimisho la Bashiru likawa “Makonda ni mfano wa kiongozi ambaye hajafundwa”.

Kwa sehemu ndogo, nakubaliana na Dk Bashiru kuwa Makonda ana shida ya malezi ya uongozi. Hata hivyo, ukiupima mwenendo wa matamshi yake, unaona zaidi ya ukosefu wa malezi ya uongozi.

Tuanze na kauli mpya ya Makonda, kwamba aliombwa na askari kuwanunulia gari aina Toyota IST kwa sababu linatumia mafuta kidogo, akajibu yeye hawezi kuwapa askari wenye kiapo magari ya watu wanaohongwa.

Siku ambayo Dk Bashiru alimwombea radhi. Makonda alisema haoni kosa.

Advertisement

Kwamba pamoja na wote waliozungumza mpaka katibu mkuu akaona amwombee radhi, bado alisisitiza hakuwa na kosa. Hapa tatizo si kukosa malezi ya kiuongozi, bali ubishi na kutotambua nidhamu ya umri.

Dk Bashiru ni katibu mkuu wa CCM. Mwenyekiti wa sekretarieti na ndiye oksijeni ya CCM. Kiumri anatosha kuwa baba wa Makonda. Zaidi, ni msomi ngazi ya shahada ya uzamivu.

Kwa sifa zote hizo, inakuwaje Bashiru aseme Makonda amekosea na kumwombea msamaha, yeye aendelee waziwazi kusema hajakosea? Utaona kwamba ana tatizo lingine zaidi.

Januari 31, mwaka huu, Makonda alifanya kikao na wasanii mbalimbali kusikiliza kero zao, hoja mbili zilimkwaza. Ya kwanza kutoka kwa msanii wa maigizo, Jacob Stephen’ ‘JB’, aliyeomba mkutano uwe wa siri, maana changamoto nyingine si za kujadili waziwazi na kurekodiwa na waandishi wa habari.

Mwanamuziki Nikki wa Pili, aliilaumu Serikali kwa matatizo ya sanaa, kwamba hutokea wakati wa kuchukua sifa kwa wasanii na matokeo yake huharibu badala ya kutengeneza. Majibu ya Makonda yalikuwa makali mno. Alimjibu JB kuwa kama anataka mkutano wa siri akakae na mkewe. Kiumri JB ni mtu mzima kuliko Makonda. Umaarufu wa JB ulichanua miaka ya 1990 wakati Makonda ni mwanafunzi wa sekondari. Unawezaje kumjibu mtu mzima bila angalizo?

Wakati akimjibu Nikki wa Pili, Makonda alisema kuna watu wanajidanganya wanalingana naye, akasema wanaweza kuwa sawa kiumri lakini kwa cheo amewazidi sana. Hapa Makonda alitoa tambo za madaraka.

Kuhusu IST

Kwa mujibu wa ripoti iliyoelezwa na kipindi cha Amplifier, Clouds FM, mwishoni mwa mwaka jana, magari aina Toyota IST ndiyo yenye kutumiwa na Watanzania wengi zaidi.

Sababu ya magari hayo kukimbiliwa na wengi ni matumizi yake ya mafuta. Makonda kwa mtazamo wake ni kwamba hayo magari yanamilikiwa na watu wenye kuhongwa.

Watu wamechukua mikopo, wanakimbilia magari hayo kwa unafuu wa kuyahudumia. Kiongozi badala ya kuheshimu watu hao na vipato vyao, anadiriki kutamka magari wanayomiliki ni ya watu wanaohongwa. Wake kwa waume wakiendesha waonekane wamehongwa

Hali ya biashara imekuwa ngumu. Taasisi nyingi zinafunga biashara, nyingine zinapunguza wafanyakazi. Kuna kundi kubwa limejikuta halina ajira. Wengi wamechukua mikopo na wengine wametumia akiba zao kununua IST na kuziingiza kwenye biashara ya usafiri wa Uber, Bolt na kadhalika. Wewe unasema hayo magari watu wamehongwa.

Namna ambavyo Makonda aliyaelezea magari aina ya IST ni kuwa hayana hadhi. Wanaoyamiliki ni sampuli ya wenye kuhongwa. Eti, ukipanda IST huwezi kuketi nyuma na kufunga mkanda.

Matamshi haya ni kielezo cha aliyejisahau, anashindwa kutambua kuwa nchi ina watu wa vipato tofauti.

Advertisement