Lipumba ashinda tena CUF, kina Maalim waisubiri Mahakama

Mwanachama wa Chama cha CUF akikusanya kura za wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho walipokuwa wakimchaguwa mwenyekiti wao katika uchaguzi uliofanyika jana jijini Dar es Salaam. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Wakati Chama cha Wananchi CUF kikiwa katika mgogoro, chama hicho upande wa Profesa Ibrahim Lipumba walifanya uchaguzi ambako Profesa Lipumba alichaguliwa mwenyekiti akipata kura 516 akiwashinda Zubeit Mwinyi na Diana Daud ambao kwa pamoja walipata kura 52.

Dar es Salaam. Mkutano mkuu wa CUF umemchagua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyeki wa chama hicho, huku nafasi ya Maalim Seif Sharif Hamad ikiwekwa kiporo.

Maalim Seif, katibu mkuu wa chama hicho amewekwa kiporo kutokana na mabadiliko ya katiba yaliyofanyika juzi ambayo yamempa nguvu mwenyekiti kuteua majina matatu ya wanachama kwa kushauriana na makamu wenyeviti wa Bara na Zanzibar.

Baada ya hatua hiyo, majina hayo yatapelekwa katika kikao cha Baraza la Uongozi ambalo litakuwa na jukumu la kumpigia kura mmoja.

Mabadiliko hayo yaliyofanywa na mkutano huo yamefuta utaratibu wa awali ambao katibu mkuu alikuwa akichaguliwa na mkutano mkuu na sasa Profesa Lipumba atakuwa ameshikilia hatima ya Maalim Seif.

Uchaguzi huo umefanyika kipindi ambacho CUF iko katika mgogoro mkubwa wa kiuongozi ulioigawa katika pande mbili - mmoja ukiwa wa Profesa Lipumba na ule wa Maalim Seif.

Mgogoro huo umekifikisha chama hicho mahakamani ambako kuna kesi kadhaa ikiwamo ya kumpinga Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti na Machi 17, hukumu ya ama ni mwenyekiti au la itatolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Katika mkutano huo ulioanza juzi ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iliubariki kwa kuufungua kupitia naibu msajili wa vyama, Sisty Nyahoza, hatimaye jana ulimchangua Profesa Lipumba.

Baada ya kupewa nafasi ya kuzungumza, Profesa Lipumba alisema jambo la kwanza wanalokwenda kufanya ni kutibu majeraha yaliyotokana na mgogoro uliopo ndani ya chama hicho. “Atakayeendeleza migogoro iliyopita wakati tunatibu majeraha hatua kali zitachukuliwa dhidi yake,” alisema.

Hata hivyo, baada ya Profesa Lipumba kutangazwa kuwa mshindi, Nassoro Mazrui ambaye ni naibu katibu mkuu wa CUF (Zanzibar), upande wa Maalim Seif, aliliambia Mwananchi kuwa chaguzi zote zilizofanywa ni batili kwa kuwa kuna zuio la Mahakama Kuu.

“Sisi tunaamini lipo zuio la Mahakama, kwa hiyo mchakato wote ni batili na tutaupinga mahakamani,” alisema Mazrui.

Katika hotuba yake, Profesa Lipumba ambaye alianza kuongoza CUF tangu 1995 hadi 2015 alipojiuzulu kabla ya kurejea tena na kuibua mgogoro unaoendelea, aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kutoka Tanzania Bara kuwa wanakwenda kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na hataki kusikia mtaa au kijiji hakina mgombea wao.

Alisema kwa upande wa Zanzibar waende wakajenge chama na Uchaguzi Mkuu wa 2020 washiriki ipasavyo. Katika uchaguzi huo, Profesa Lipumba alipata kura 516 akiwashinda Zueit Mwinyi aliyepata kura 36 na Diana Daudi kura 16.

Nafasi ya makamu mwenyekiti Zanzibar ilichukuliwa na Abbas Juma Muhunzi aliyepata kura 349 akiwashinda wenzake watatu.

Maftaha Nachuma alishinda kwa upande wa Bara akipata kura 231 sawa na asilimia 40.9. Nachuma pia ni mbunge wa Mtwara Mjini.