Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lissu: Niko tayari kuwania urais 2020

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu

Dar es Salaam. Wakati vuguvugu la Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 likianza chini kwa chini, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amesema yupo tayari kugombea urais ikiwa vyama vya upinzani vitampa ridhaa hiyo.

Lissu ambaye yupo nchini Ubelgiji akipatiwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30, Septemba 7 mwaka jana akiwa Dodoma na watu wasiojulikana, amesema hayo jana wakati akizungumza na Mwananchi kuhusu maendeleo ya afya yake.

Mwanasiasa huyo alisema yeye ni mwanachama wa Chadema na hawezi kufanya jambo pasi na kuridhiwa na chama chake au vyama washirika wa Chadema kwani kufanya hivyo ni kinyume cha taratibu na maadili.

Kauli ya Lissu kuhusu kugombea urais mwaka 2020 imetokana na swali aliloulizwa kutokana na kuwa miongoni mwa wanasiasa wa upinzani wanaotajwatajwa, “Wakikaa katika vikao na kunipa bendera, nitakubali kubeba msalaba huo mzito kwa mikono miwili.”

Pia aliulizwa, ikiwa hataombwa na chama atajitosa mwenyewe kuwania nafasi hiyo? Rais huyo wa zamani wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) alisema, “Maadili yangu, unaambiwa ukiwa katika chama lazima upewe fursa kwa hiyo nitasubiri fursa hiyo.”

Katika Uchaguzi Mkuu uliopita wa 2015, vyama vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya Chadema, NCCR-Mageuzi, NLD na CUF vilimsimamisha Edward Lowassa kuwania nafasi ya urais na licha ya kushindwa Dk John Magufuli wa CCM, alipata kura nyingi ambazo hazijawahi kufikiwa na mgombea yeyote wa upinzani.

Katika uchaguzi huo, ilishuhudiwa kwa mara ya kwanza tangu uchaguzi wa vyama vingi ulipoanza mwaka 1995, upinzani ukipata kura zaidi ya milioni sita ikiwa ni tofauti ya kura milioni mbili dhidi ya mshindi wa nafasi hiyo.

Lowassa alipata kura milioni 6.01 sawa na asilimia 39.97 huku Dk Magufuli akiibuka mshindi kwa kupata kura milioni 8.9 sawa na asilimia 58.46.

Kuhitimisha matibabu Desemba 31

Kuhusu afya yake, Lissu ambaye ni mnadhimu mkuu wa kambi rasmi ya upinzani bungeni alisema anatarajia kuanza mwaka akiwa hana vyuma alivyowekewa Julai 9 katika mguu wake wa kulia ili kuunganisha mifupa.

“Desemba 31 nitafanyiwa upasuaji wa mwisho wa kuondoa hii antena ambayo nimekaa nayo kwa miezi sita tangu Julai 9 na nimeelezwa na madaktari kuwa mfupa uliokuwa uunge umeunga na mfupa uliotakiwa kuota unaendelea vizuri,” alisema Lissu na kuongeza:

“Yaani Jumatatu (Desemba 31) nitahitimisha kazi ya kitabibu na nitaanza mwaka mpya (2019) na mguu mpya ambao hauna chuma.”

Lissu alisema baada ya kuondolewa kwa vyuma, kitakachofuata ni mazoezi ya kutembea na taratibu ataachana na magongo.

Baada ya hapo, Lissu alisema ataanza kuhudhuria vikao mbalimbali ambayo amealikwa katika mataifa ya Ulaya.

Alisema Januari 14 amealikwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) na Umoja wa Ulaya (EU) Brussels, Ubelgiji na Februari mwakani amepata mwaliko wa wiki moja huko Washington Marekani.

“Huko kote nakwenda kuzungumzia kile kilichonitokea Septemba 7 (mwaka jana) lakini kile ambacho kinaendelea nyumbani (Tanzania) na mambo mengine,” alisema.

Kurudi Tanzania badobado kwanza

Alipoulizwa kwamba kuanza wake kusafiri nchi mbalimbali bila shaka ni wakati wake wa kurejea nyumbani, mwanasheria mkuu huyo wa Chadema alisema, “Katikati ya mwakani naweza kurejea. Kuanza mazoezi hakutanizuia kurejea kwani naweza kurudi nyumbani na nikawa nakuja huku (Ubelgiji) kwa madaktari.”

Hata hivyo, Lissu alisema hilo la kurejea nchini litafanikiwa baada ya kufanya mazungumzo na watu mbalimbali ikiwamo viongozi wenzake wa kisiasa pamoja na Serikali.

“Serikali itapaswa kunieleza usalama wangu utakuwaje baada ya kurejea, ingawa jukumu la Serikali ni kulinda raia wake na mimi ni miongoni mwao hasa ukizingatia kile kilichonitokea,” alisema.

Akigusia harakati zake za kupigania demokrasia, Lissu alisema , “Kama nilivyowahi kusema, sitarudi nyuma na mapambano ya kupigania demokrasia si ya wanasiasa pekee, bali makundi mbalimbali kama madaktari, waandishi wa habari, wakulima, wavuvi, bodaboda na wengine.”

Aliunga mkono hatua ya vyama vya Chaumma na ACT- Wazalendo kushirikiana na vyama vya Ukawa vya Chadema, CUF, NLD na NCCR-Mageuzi kutoa tamko la pamoja kuhusu mwaka 2019.

“Umoja ni nguvu utengano ni dhaifu, katika mapambano ya demokrasia kushirikiana ni muhimu zaidi na hicho walichokubaliana mwaka 2019 ni mwaka wa kupigania demokrasia nami nakiunga mkono asilimia 100,” alisema.