Lissu: Nitarejea nyumbani asubuhi au mchana kweupe

Thursday August 1 2019

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Tundu Lissu sasa amehitimisha safari ya siku 691 za matumizi ya dawa kutibu majeraha ya risasi na urekebishaji wake na sasa anasema atarudi nchini “mchana kweupe; si usiku wala alfajiri”.

Lissu, aliyevuliwa ubunge wa Singida Mashariki kutokana na kutohudhuria vikao vya Bunge tangu ashambuliwe kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana Septemba 7, 2017 akiwa nje ya makazi yake mjini Dodoma, alitibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na usiku wa siku hiyo akahamishiwa Jijini Nairobi, Kenya na Januari 6, 2018 akahamishiwa Ubelgiji.

Katika salamu alizozitoa jana kwenda kwa marafiki zake, Lissu alizungumzia masuala kadhaa ya hali yake ya kiafya pamoja na hatua alizofikia kwenda mahakamani kupigania ubunge wake pamoja na tarehe atakayorejea nchini.

Mwanasheria huyo mkuu wa Chadema alisema tangu alipoanza matibabu, juzi alihitimisha matumizi ya dawa ikiwa ni siku 691 sawa na mwaka mmoja, miezi 10 na siku 23.

“Leo (jana) ni siku ya kwanza tangu niliposhambuliwa Septemba 7, 2017, situmii dawa ya aina yoyote,” alisema wakili huyo wa kujitegemea.

“Kwa maelekezo ya madaktari wangu, jana (juzi) ilikuwa siku ya mwisho ya mimi kutumia dawa ambazo nimezitumia tangu siku niliposhambuliwa.

Advertisement

“Na jana (juzi) hiyohiyo nilitimiza mwezi mzima tangu niache kutumia magongo. Ijapokuwa bado nachechemea kwa sababu ya goti kutokunja sawasawa. Sasa natembea bila msaada wa magongo.”

Katika salamu hizo, Lissu alisema matibabu yake yatakamilika rasmi Agosti 20 atakapokutana na timu ya madaktari wake kwa ajili ya vipimo vya mwisho na ushauri.

“Baada ya hapo itakuwa ni maandalizi ya kurudi kwetu. Hakutakuwa na sababu tena ya kitabibu ya mimi kuendelea kukaa Ulaya,” alisema Lissu na kuongeza kuwa atarejea “mchana kweupe na si alfajiri wala usiku” na ikiwa ratiba ya ndege ikiwa ni usiku atabadilisha.

Awali, alisema angerejea Septemba 7 siku ambayo alishambuliwa lakini jana alisema tarehe ya kurudi itatangazwa baadaye.

“Kwa vile tumekuwa pamoja kwenye safari hii ndefu, hatuna budi kupongezana na kumshukuru Mungu kwa hatua hii nzuri nilikofikia,” alisema Lissu.

Alisema yeye pamoja na familia yake hawatachoka kuwashukuru wananchi kwa kuwa pamoja nao katika kipindi chote kigumu.

Kuhusu kuvuliwa ubunge, Lissu alisema wakati wowote kuanzia jana wangeenda mahakamani kufungua kesi ya kupinga uamuzi wa Spika.

Spika alimtaarifu mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC) Juni 28 kuwa Lissu amepoteza sifa ya kuwa mbunge kwa kuwa ni mtoro na hakujaza fomu za maadili ya uongozi ambazo huelezea mali anazomiliki.

“Kesi za ubunge, kama zilivyo kesi zote za uchaguzi wa kisiasa, ni kesi za kisiasa,” alisema Lissu,“ni mwendelezo wa mapambano ya kisiasa katika uwanja tofauti. Kwa sababu hiyo, ni kesi nyeti na za kipekee sana. Zinahitaji umakini mkubwa katika kuziandaa na kuziendesha. Nina uzoefu mkubwa nazo, kwa sababu nimezifanya sana tangu 2005.

“Sasa ninaweza kuwafahamisha kwamba mimi na timu ya mawakili wangu tuko tayari kuingia Mahakama Kuu ya Tanzania. Tutafanya hivyo muda wowote kuanzia leo. Maandalizi yote yanayohitajika yamekamilika.”

“Nitawajulisheni mara moja kesi hii itakaposajiliwa rasmi. Kama itawapendeza, nitawaomba mtakaopata nafasi kuhudhuria mahakamani, kwa niaba yangu, wakati wote itakapokuwa inaendelea,” alisema.

Advertisement