Mabilioni ya Barrick kulipwa mwezi ujao

Rais John Magufuli akiagana na Ofisa Mwendeshaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation anayeshughulikia Afrika na Mashariki ya Kati , Dk Willem Jacobs baada ya  kukutana na kufanya naye mazungumzo Ikulu jijini Dar es Salaam jana. Picha na Ikulu

Muktasari:

Zile fedha zilizoibua mjadala mkubwa kiasi cha kufikia wananchi kutafsiri kuwa zingewezesha kila Mtanzania kuwa na gari moja aina ya Toyota Noah, sasa zinakuja.

Dar es Salaam. Zile fedha zilizoibua mjadala mkubwa kiasi cha kufikia wananchi kutafsiri kuwa zingewezesha kila Mtanzania kuwa na gari moja aina ya Toyota Noah, sasa zinakuja.

Mbali na tafsiri hiyo, baadhi walisema si rahisi kwa kampuni ya Barrick Gold kulipa kiwango hicho cha fedha kilichoafikiwa katika mazungumzo baina ya timu ya Tanzania na ya Barrick Gold.

Lakini kampuni hiyo kubwa katika uchimbaji madini duniani, sasa iko tayari kulipa fedha hizo, Sh682 bilioni ambazo Barrick Gold ilisema ingelipa kuonyesha nia njema ya kufidia fedha zilizotokana na upotevu wa mapato katika biashara zinazoendeshwa na kampuni ya Acacia.

Barrick, ambayo ni mwanahisa mkubwa wa Acacia, imeahidi kulipa fedha hizo Machi.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu jana inaeleza kuwa ofisa mwendeshaji mkuu wa Barrick anayeshughulikia Afrika Mashariki na Kati, Dk Willem Jacob alieleza hayo alipokutaka na Rais John Magufuli.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi aliiyeongoza timu ya Serikali katika majadiliano hayo, amesema nyaraka za makubaliano hayo zimekamilika.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kinachosubiriwa ni utekelezaji wa makubaliano hayo unaotarajiwa kukamilika ifikapo mwisho wa Machi, mwaka huu.

“Baada ya muungano wao, hii sasa ni timu mpya na tumewaona ni watu ambao sasa wapo tayari kutekeleza yale yote yaliyokubaliwa. Na sasa ni kwa kila upande kwenda kwenye vyombo vyake vinavyohusika kufanya maamuzi ya mwisho ili utekelezaji ufanyike,” taarifa hiyo inamnukuu Waziri Kabudi.

Oktoba, 2017 Barrick ilikubali kuilipa Serikali hisa ya asilimia 16 na mgawo wa asilimia 50 ya mauzo ya dhahabu kutoka katika migodi mitatu inayoimiliki, sambamba na kutoa dola 300 milioni za Kimarekani kama malipo ya nia njema.

Taarifa iliyotolewa jana na mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa inaeleza kuwa, Jacobs aliyeongozana na washauri wa Barrick Gold Corporation, Rich Haddock, Duncan Bullivant na Wicus du Preez wamemhakikishia Magufuli kuwa makubaliano yaliyofikiwa watayatekeleza kikamilifu.

“Hasa baada ya kampuni kubwa ya uchimbaji dhahabu ya Rand Gold ya Afrika Kusini kuungana na Barrick Gold Corporation katika umiliki, uwekezaji na menejimenti,” inaeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo inamnukuu Jacobs akibainisha kuwa hakuna kitakachokuwa tofauti na makubaliano yaliyofikiwa awali ambayo yaliongozwa na mwenyekiti mtendaji wa Barrick Gold Corporation, Profesa John Thornton.

“Ikiwemo Barrick Gold Corporation kuilipa Serikali ya Tanzania kifuta machozi cha Dola 300 milioni za Marekani (Sh682.5bilioni), kuendelea na uwekezaji kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Barrick Gold na mgawanyo wa mapato ya kiuchumi kwa uwiano wa asilimia 50 kwa 50 kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya Barrick Gold.

Sakata la Acacia lilianza wakati Rais Magufuli alipopiga marufuku usafirishwaji wa mchanga wa madini nje ya nchi kwa ajili ya kuyeyusha kupata masalia.

Baadaye, Rais aliunda kamati iliyochunguza biashara ya madini na kutoka na matokeo yaliyoonyesha udhaifu katika sheria, mikataba na utendaji wa watumishi wa Serikali uliosababisha nchi kutonufaika na rasilimali hizo.

Kamati hiyo pia ilibaini kuwa Acacia ilikuwa ikifanya kazi bila usajili rasmi na baadaye Mamlaka ya Mapato (TRA) ikabaini kuwa Acacia haikulipa kodi iliyofikia dola 190 bilioni za Kimarekani, ikichanganywa na riba.