Mawakili watoana jasho kesi ya mume, ndugu kugombea maiti

Ndugu wa marehemu Fatuma Kileo,wakitoka katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi  Moshi mjini jana baada ya kesi ya ndugu yao kuhairishwa. Picha na Dionis Nyato.

Muktasari:

Mkoa huo umekuwa ukiteswa na mambo mbalimbali ya kimaisha, uchumi na kiafya; wadau wazungumzia mustakabali wa hali iliyopo

Moshi. Mawakili wa pande mbili katika kesi ya kugombea maiti ya Fatuma Kileo (56) mkazi wa Himo, jana walionyeshana ‘ubabe’ wa kisheria mahakamani wakati wa usikilizwaji wa pingamizi la awali.

Juzi familia ikiongozwa na Ausen Nkya, waliwasilisha pingamizi la awali wakitaka maombi ya mume wa marehemu, Zuberi Shango ya kutaka aruhusiwe kumzika mkewe yatupwe.

Akiwasilisha hoja za kisheria kuhusu pingamizi hilo, wakili Godwin Sandi anayewatetea wajibu maombi alidai Shango amewasilisha kortini maombi madogo badala ya kufungua shauri la msingi.

Wakili Sandi katika hoja zake alizozitoa jana mchana, alisema maombi hayo yamefunguliwa kimakosa na kwamba vifungu vya sheria vilivyotumika havikustahili kutumika katika kufungua kesi hiyo.

Wakili huyo alieleza haikupaswa kufunguliwa kwa maombi madogo, bali ilipaswa kufunguliwa kama kesi ya kawaida ya madai, hivyo akaiomba mahakama hiyo itupilie mbali maombi hayo.

Katika hoja yake, wakili huyo alisema hati ya kuitwa kwa shauri linalosikilizwa chemba inaonyesha ni maombi madogo kwamba, muombaji amezuiwa na wajibu maombi kumzika mkewe.

Wakili Sandi alieleza shauri hilo lilipaswa lifunguliwe kama la madai na kuiomba mahakama itupe maombi hayo na wateja wake waruhusiwe kwenda kuzika.

“Naiomba mahakama yako itupilie mbali maombi haya na kuruhusu twende (kuzika). Kulingana na vifungu walivyovitumia kesi hii inakosa sifa ya kuendelea kuwa mahakamani,” alisisitiza wakili huyo.

Alisema kifungu cha 66 (e) na 95, alivyovitumia mleta maombi haviipi mahakama uwezo wa kusikiliza au kutoa amri zinazoombwa kwa vile kwa dosari hizo, kesi hiyo inakosa sifa ya kuwa mahakamani.

Wakili Sandi alieleza kuwa ili mahakama iweze kutoa uamuzi juu ya kesi hiyo, ni lazima kuwe na kesi ya msingi na kwamba kuifungua kama maombi madogo inakosa sifa kwa mujibu wa sheria.

Akizungumzia kifungu cha 95 cha sheria ya muongozo wa mashauri ya madai, kilichotumiwa na watoa maombi, alisema pia hakiipi mahakama uwezo wa kusikiliza kesi hiyo.

Akihitimisha hoja yake, wakili Sandi aliiambia mahakama kuwa kwa kuwa maombi yamewasilishwa kinyume cha sheria, wanaomba kesi hiyo itupiliwe mbali.

Akijibu hoja za pingamizi hilo, Wakili Tumaini Materu ambaye ni mmoja wa mawakili wanne wanaomwakilisha mume wa marehemu, Shango, alidai pingamizi lililowekwa halina mashiko kisheria.

Wakili huyo alieleza kuwa hakuna sheria ambayo inakataza maombi kuletwa kwa namna walivyopeleka na kwamba zipo kesi za mfano ambazo zinaruhusu uamuzi wa maombi kutolewa bila kesi ya msingi.

“Tunasema maombi madogo yanaruhusiwa bila hata ya kuwa na kesi ya msingi, hivyo pingamizi hilo litupiliwe mbali kwa kuwa lililenga kuzuia ombi hili ambalo lililetwa kwa haraka,”alisema.

Wakili huyo alisisitiza kuwa maombi yao yaliwasilishwa kisheria, na inaruhusu mahakama kuyasikiliza na kuweza kutenda haki kwani hata kifungu cha 95 walichotumia ni sahihi.

Wakili mwingine katika jopo hilo, Elia Kiwia alipinga maelezo ya Sandi kuhusiana na kifungu cha 68(e) akisema hakueleza nini cha kufanya na kudai hiyo inaonyesha yalikuwa ni mawazo yake.

“Maombi yetu yaliyoko mezani tupo sahihi. Tupo sahihi kutumia kifungu hicho ndio maana tunaiomba mahakama itoe muongozo na kutupa maelekezo juu ya mazishi ya mke wa mwombaji,” alisema.

“Kifungu pekee kinachoweza kutibu kesi yetu ni cha 95 na hakuna kifungu kingine cha sheria kinachoweza kutumika katika kesi hii.” Alisema wakili wa wajibu maombi endapo aliona mahakama haikuelezwa sawasawa, akiwa kama ofisa wa mahakama alipaswa kuelekeza ni kifungu kipi sahihi ambacho ilipaswa kukitumia.

Kwa upande wake, wakili Wilhad Kitaly alisema mapingamizi yaliyowasilishwa mahakamani hayana msingi kwa kuwa taratibu zilizotumika kufungua kesi hiyo ni sahihi kwa mujibu wa sheria.

Aliiambia mahakama kuwa kifungu cha 68,(e) kiko sahihi mbele ya macho ya mahakama kwa kuwa kinaipa mamlaka ya kutoa uamuzi kama haki inakwenda kupotezwa.

Alifafanuwa kuwa Ibara ya 47(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaitaka mahakama pale inapokwenda kutenda haki, isifungwe na ufundi wa kisheria kama uliojitokeza katika kesi hiyo.

“Haki katika shauri hili ni ya kuzika mwili ambao upo mochwari. Ombi letu ni kuwa isifungwe na ufundi wa kisheria, bali iende ikatende haki na ni maombi yetu pingamizi hili litupiliwe mbali,” alisema.

Wakili Mussa Mziray aliiomba mahakama kutupilia mbali pingamizi lilizowasilishwa na kusikiliza kesi ili kupunguza muda wa mwili wa marehemu kukaa mochwari. Baada ya kusikiliza hoja za pande mbili, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Moshi, Bernadetha Maziku aliahirisha kesi hiyo saa 9:45 alasiri hadi saa 11:30 jioni atakapotoa uamuzi juu ya pingamizi hilo.

Sababu za mume kumzika mkewe

Kwa mujibu wa maombi namba 24 ya 2018 yaliyowasilishwa mahakamani hapo, mume wa marehemu anadai alifunga ndoa na Fatuma Julai 20, 2005 huko Tunduma mkoa wa Mbeya.

Wawili hao walifunga ndoa ya Kiislamu na hati ya ndoa namba 6306 ilitolewa na Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Mbeya na kusimamiwa na Sheikh Idrisa Adeny.

Katika hati ya kiapo kinzani walichokiwasilisha mahakamani jana, wajibu maombi wawili, Ausen Nkya na Lodrick Kileo, wanasisitiza kuwa marehemu hakuwahi kuolewa wala hakufia hospitali ya Kilema isipokuwa alifia Himo na mwili wake kupelekwa Hospitali ya Kilema.