Mrema ahofia CUF kufuata njia za NCCR, amuonya Seif

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema anahofia kuwa CUF inaweza kuwa inapitia njia ambayo aliipitia, huku akimuona Maalim Seif Sharif Hamad kuwa asidhani amepata ufumbuzi.

Mrema, aliyeondoka CCM na kupokewa kwa nguvu na wapinzani na baadaye kupewa fursa ya kugombea urais mwaka 1995, pia alisema masuala ya siasa kupeleka mahakamani yanaua vyama.

Maalim Seif, ambaye amekuwa katibu wa CUF tangu mwanzoni mwa miaka ya tisini, alitangaza kuhamia ACT Wazalendo mapema wiki hii baada ya Mahakama Kuu kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti wa chama hicho.

“CUF wanapitia njia ileile niliyopitia. Nilipokuwa NCCR nilizushiwa mambo na kupewa sifa mbaya kuwa mimi ni kibaraka wa CCM, matokeo yake tukapotezeana imani, tukashindwa kuaminiana nikaamua niondoke,” alisema.

Mrema, aliyekuwa mbunge wa Vunjo mkoani Kilimanjaro na Temeke jijini Dar es Salaam kwa nyakati tofauti, alisema Watanzania watarajie kuiona CUF ikipitia vipindi tofauti, ikiwamo kupoteza nguvu kutokana na mpasuko huo.

“Hata kwa Maalim Seif asijidanganye kuwa amepatata ufumbuzi. Kwenda ACT si mwarobaini wa changamoto za kisiasa katika vyama vyetu,” alisema Mrema, ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na baadaye kuhamishiwa Wizara ya Kazi kabla ya kutofautiana na mawaziri wenzake na hivyo kuonekana ameshindwa kuheshimu kanuni ya uwajibikaji wa pamoja.

“Tujifunze kutatua changamoto zetu. Tusijidanganye kuwa mahakama ni kila kitu, hivyo kufikishana huko hata kwa jambo dogo.”

Akiwa mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Mrema alilazimika kukihama chama hicho na wafuasi wake mwaka 1999, baada ya kuingia mgogoro dhidi ya Kamati Kuu iliyokuwa ikiungwa mkono na Mabere Marando, aliyekuwa katibu mkuu.

Akiungwa mkono na wajumbe wa Halmashauri Kuu, Mrema aliitisha mkutano wa kumfukuza Marando na wajumbe wengine wa Kamati Kuu, lakini walikwenda mahakamani na kurejeshwa madarakani.

Katika mkutano wa Halmashauri Kuu uliofanyika hoteli ya Bwawani Zanzibar, Mrema na wafuasi waliondoka wakati wa mapumziko ya chakula cha mchana na baadaye wakajiunga na TLP.