Mtoto aliyetekwa Dar awapa wakati mgumu wenzake

Idrissa Ally (13) alitekwa

Muktasari:

  • Idrissa Ally (13) alitekwa 'kimafia' Septemba 26, maeneo ya Tegeta jijini Dar es Salaam tukio ambalo limewafanya wanafunzi wenzake kuanza kupoteza matumaini ya mwenzao kupatikana na kurejea shule.

Dar es Salaam. Mussa Idrissa, mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Princes Gate anayesoma Idrissa Ally (13) aliyetekwa ‘kimafia’ amesema wanafunzi wa shule hiyo wameanza kupoteza matumaini ya kumuona rafiki yao akirejea shuleni hapo.

Akizungumza na Mwananchi jana, Mwalimu Mussa alisema wanaendelea kuwapa moyo wanafunzi hao kwamba Idrissa atarejea kwa sababu wanaendelea kumuomba Mungu na vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kumtafuta.

Idrissa, ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tano katika shule hiyo hadi jana ametimiza mwezi mmoja na siku moja bila kuonekana baada ya kutekwa Septemba 26 saa 11 jioni akiwa anacheza na wenzake eneo la Tegeta Masaiti, wilayani Kinondoni Dar es Salaam.

Mtoto huyo anadaiwa kuchukuliwa na dereva mmoja mwanaume aliyekuwa katika gari aina ya Toyota IST, ambaye baada ya kuwafukuza marafiki wa Idrissa, alitoa kichupa kidogo kinachodhaniwa ni ‘spray’ na kumpulizia mtoto huyo na kumuingiza mlango wa nyuma wa gari lake kisha kuondoka.

Akizungumza kwa upole jana, Mwalimu Mussa alisema wanafunzi wenzake na Idrissa walikuwa na matumaini makubwa kuwa rafiki yao angerudi na kujiunga nao kwa siku za awali, lakini kadiri muda unavyozidi kwenda wanavunjika moyo.

“Nikiwa ofisi kwa nyakati tofauti hufika na kuniuliza vipi mwalimu Idrissa anarudi lini? Mbona siku zinaenda sisi tulidhani kapotea kwa wiki moja tu,” aliwanukuu wanafunzi wengine.

Hata hivyo, alisema huwa anajitahidi kuwapatia majibu ya kutowakatisha tamaa.

“Nikiwajibu bado, ghafla wanakosa raha na nyuso zao huonekana zenye huzuni,” alisema.

Mwalimu huyo alisema juzi walikuwa na kikao cha walimu wakuu wa shule za kata ya Kunduchi na wao waliulizia hatima ya mtoto huyo.

“Tukiwa katikati ya kikao, waliniuliza vipi kijana wetu amepatikana? Nikawajibu bado hatujafanikiwa, wakasema tuendelee kumuomba Mungu,” alisema Mussa.

Mama mzazi wa Idrissa, Leila Kombe alisema bado mwanaye hajapatikana, lakini polisi wamewahakikishia kuwa upelelezi dhidi ya suala hilo unaendelea na wana imani atapatikana.

Hivi karibuni Ally Idd, baba mzazi wa Idrissa alisema nguvu kubwa iliyotumika kumpata mfanyabiashara maarufu nchini Mohammed Dewji aliyetekwa kisha kupatikana, ihamishiwe kwa watu wengine akiwamo mwanaye.

Idd mwenye watoto wawili Idrissa na Ishac alisema, “Sina mengi ya kuzungumza bali naviomba vyombo vya dola hasa polisi, nguvu iliyotumika kumpata Mo Dewji itumike pia kwa watoto wetu waliopotea na kutekwa.

“Binadamu wote ni sawa, bado tunaliamini jeshi letu kwa kazi inayofanya, lakini itusaidie na sisi, ni muda sasa mwanangu sijamuona,” alisema baba yake Idrissa.

Hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alisema Serikali inafuatilia matukio ya utekaji na kupotea ndiyo maana wengine wanapatikana.

Kwa mujibu wa Lugola, mwaka 2017 watu 273 walitekwa na polisi walifanikiwa kuwapata 22 wakiwa hai na wawili wakiwa wamekufa na watatu hawakupatikana.

Katika utekaji wa watoto alisema kati ya mwaka 2016 hadi 2018, watoto 18 miongoni mwao wa kiume sita na wakike 12 walikumbwa na adha hiyo.