VIDEO: ‘Mwanafunzi aliyepigwa risasi alitaka kumuua Rais Kenyatta’

Muktasari:

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta (JKUAT) aliyepigwa risasi amedai nia yake ilikuwa ni ‘kumuua’ Rais Uhuru Kenyatta.


Nairobi. Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta (JKUAT) aliyepigwa risasi amedai nia yake ilikuwa ni ‘kumuua’ Rais Uhuru Kenyatta.

Akiwa amejihami kwa kisu, Brian Kibet Bera (25), ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tano anayesomea uhandisi wa mashine chuoni JKUAT, alikuwa amepanga kumvamia Rais kwa muda, lakini vitisho vyake vikachukuliwa kama mzaha.

Msemaji wa Ikulu, Kanze Dena alithibitisha kuwa Bera alivamia Ikulu Jumatatu jioni kwa kuruka ukuta, na akapigwa risasi bega la kushoto na walinzi, alipokataa kusimama na badala yake akawatishia kwa kisu.

Tangu Ijumaa iliyopita, Bera alikuwa akitoa vitisho dhidi ya Rais Kenyatta kwenye akaunti yake ya mtandao wa Facebook.

Alitoa vitisho vya mwisho Jumapili saa tatu na dakika 15 usiku ambapo alisema: “Kesho (Jumatatu) nitavamia Ikulu. Mungu amenituma kutekeleza hukumu dhidi ya kila mwizi na washirika wa wezi.”

Alitangaza vita dhidi ya Rais Kenyatta na sekta ya mabenki anayodai ndiyo inashawishi maamuzi ya utawala wa Jubilee, na akapuuza baadhi ya watu walioeleza hofu kwamba huenda ana matatizo ya kiakili.