Mwenyekiti Tadea aitetea CCM

Thursday May 16 2019

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Haji Ussi Gavu akiwasilisha kwenye kikao cha Baraza la Wawakilishi makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2019/2020, mjini Unguja, Zanzibar jana. Picha na Haji Mtumwa 

By Haji Mtumwa, Mwananchi [email protected]

Unguja. Waziri asiye na Wizara Maalumu wa Serikali ya Zanzibar, Juma Ali Khatib amesema kama kuna mtu ana nia ya kutaka kuiondoa CCM madarakani ajiandae kuondoka mwenyewe.

Khatib ambaye pia ni mwenyekiti wa Chama cha Ada-Tadea alitoa kauli hiyo juzi akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Ofisi ya Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa mwaka wa 2019/20.

Alisema kuna watu wana dhana potofu ya kutaka kuiondoa CCM madarakani na kwamba haina nguvu.

Mpinzani huyo ambaye aliteuliwa na Rais Dk Ali Mohamed Shein kuwa mwakilishi kisha waziri asiye na wizara maalumu, alisema kutokana na utendaji na utekelezaji wa maendeleo wa Dk Shein, hakuna mtu hata mmoja asiyemkubali.

Khatib alisema anashangazwa wanapojitokeza watu kana kwamba hawaoni kazi hiyo wakitaka kufanya mabadiliko ya chama tawala, hivyo anawaona wana mtizamo finyu.

Naye mwakilishi wa kuteuliwa, Said Soud Said aliwataka wananchi kutokubali maneno ya baadhi ya wanasiasa ambao hawana nia njema na nchi.

Alisema kuna baadhi ya wanasiasa kazi yao kubwa ni kuharibu mafanikio yaliyopatikana chini ya CCM, huku wakisahau uwapo wao hapo unatokana na msaada mkubwa wa chama hicho.

Bajeti ya Sh11 bilioni

Awali, akiwasilisha hotuba hiyo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Haji Ussi (Gavu), aliliomba Baraza la Wawakilishi kuidhinisha Sh11.726 bilioni kwa ajili ya mishahara, matumizi ya kawaida na maendeleo katika mwaka wa fedha 2019/20.

Katika kiwango hicho, Sh9.72 bilioni ni matumizi ya kawaida na Sh2 bilioni za maendeleo.

Gavu alitaja vipaumbele vya bajeti hiyo kuwa ni kuratibu shughuli na kusimamia huduma za Rais, kufuatilia na kutathmini utekelezaji shughuli za wizara, idara, taasisi na uamuzi wa Serikali.

Pia, kuratibu ushiriki wa watendaji wa Serikali katika vikao vya mtangamano wa jumuiya za kikanda na kusimamia majukumu ya kikatiba na kisheria ya Baraza la Mapinduzi, kuratibu ushirikiano wa kikanda, mashirika ya kimataifa na Wazanzibari wanaoishi nje.

Advertisement