Spika wa Bunge Eala apingwa mahakamani

Thursday March 14 2019

 

By Zephania Ubwani, Mwananchi [email protected]

Arusha. Burundi imefungua rasmi kesi katika Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) kupinga uchaguzi wa Spika wa sasa wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala).

Mwanasheria wa Burundi, Nestory Kayobera aliieleza mahakama hiyo Jumanne iliyopita kwamba uchaguzi ulifanyika kwa kukiuka mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Alisema uchaguzi ulifanyika bila kuwepo kwa wawakilishi kutoka Burundi na Tanzania, jambo ambalo ni kinyume na kanuni za Eala na mkataba wa jumuiya hiyo.

Kesi hiyo ilifikishwa mbele ya Jaji Monica Mugenyi kama jaji kiongozi na majaji wengine; Dk Faustin Ntezilyayao, Fakihi Jundi, Charles Nyawello na Charles Nyachae.

Kayobera aliieleza mahakama kuwa uchaguzi wa Spika unaongozwa na mkataba wa EAC na sheria na taratibu zake na kwamba uchaguzi huo uliofanyika Desemba 19 mwaka jana ubatilishwe kwa sababu haukufuata vigezo vinavyotakiwa.

Katika uchaguzi huo, Martin Karoli Ngoga, mbunge wa Eala kutoka Rwanda alichaguliwa kuwa spika wa tano wa Eala akichukua nafasi ya Daniel Kidega kutoka Uganda ambaye alitumikia nafasi hiyo tangu Desemba 2014.

Burundi na Tanzania pia zilisimamisha wagombea wao kila mmoja kwenye uchaguzi huo wa Spika.

Baadaye wabunge kutoka nchi hizo mbili waligomea uchaguzi huo baada ya majina ya wagombea wao kufutwa.

Kwa mujibu wa mwanasheria huyo, akidi ya bunge hilo au kamati ya bunge zima inatakiwa kuwa nusu ya wabunge wote waliochaguliwa endapo kuna uchaguzi kama huo.

Akidi hiyo inatakiwa kuwa na angalau theluthi moja ya wabunge wa kuchaguliwa kutoka katika kila nchini mwanachama wa EAC.

Kayobera aliieleza mahakama Ibara ya 23 ya Mkataba wa EAC inatoa mamlaka kwa mahakama, kama chombo ndani ya jumuiya, kuhakikisha sheria zinafuatwa na mkataba unazingatiwa.

Aliitaka Mahakama ya Afrika Mashariki kuitisha uchaguzi mpya wa Spika kwa mujibu wa mkataba na kanuni za bunge hilo.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa EAC, Dk Anthony Kafumbe alisema uchaguzi ulifanyika kwa mujibu wa Sehemu ya III ya kanuni za mwongozo wa Bunge.

“Baada ya wabunge wote kupiga kura, karani (wa bunge) kwa maoni ya wabunge waliopo, atatoa kura zote kwenye masanduku na kuanza kuhesabu kura zilizokuwemo ndani yake,” alisema.

Alisema suala la akidi halihusiki kabisa na kwamba hiyo inatumika pale bunge linapokuwa limeundwa.

Aliongeza hakukuwa na ukiukwaji wowote wa taratibu kwenye uchaguzi wa Spika, na kwamba Spika alichaguliwa kwa mujibu wa vifungu vya kanuni za Bunge hilo.

Kafumbe alisema wabunge wamemkubali Spika na kwa hiyo haitakuwa na tija kufuta uchaguzi huo na kuitisha uchaguzi mpya.

Mahakama itatoa uamuzi juu ya suala hilo baada ya kuzisikiliza pande mbili za mlalamikaji na mlalamikiwa.

Advertisement