Tozo zasababisha wafanyabiashara kurejesha leseni

Thursday May 16 2019

 

By Peter Elias, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wafanyabiashara zaidi ya 100 wamelalamikia tozo mbalimbali za halmashauri ya Manispaa ya Mtwara-Mikindani.

Wamesema kutokana na hali hiyo, wameamua kufunga biashara na kurejesha leseni za biashara walizokata kwa manispaa hiyo.

Kutokana na sababu hiyo, wafanyabiashara hao wamedai kwamba wameamua kufunga biashara zao na kurudisha leseni ofisi za manispaa hiyo wakidai kwamba mzigo huo umekuwa mkubwa huku mzunguko wa biashara ukiwa mdogo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani, Emmanuel Mwaigobeko alikiri kuwapo kwa changamoto hiyo lakini alisisitiza kwamba kodi nyingine siyo za manispaa, bali ni za mamlaka nyingine za serikali.

Mfanyabiashara mmoja wa Mtwara-Mikindani, Mkuruma Suma aliliambia Mwananchi jana kuwa licha ya tozo hizo, pia kumekuwa na mdororo wa biashara, hali inayowafanya wakose fedha na kile wanachokipata kinaishia kwenye kulipa tozo hizo.

“Biashara hakuna, unaweza ukakaa siku tatu hujauza au ukauza Sh15,000 tu. Hapo hapo unatakiwa kulipa kodi ya pango ya Sh100,000 kwa mwezi, kuna tozo ya zimamoto, leseni ya biashara na bidhaa nyingine tofauti,” alidai Suma.

Advertisement

Alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) nayo inawakadiria kodi bila kujua hali ya biashara ikoje, jambo ambalo linawapa ugumu wa kufanya biashara zao. Pia, alisema makadirio hayo yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka.

Mwenyekiti wa ushirika wa wafanyabiashara Soko Kuu la Mtwara, Ramadhan Mtumba alisema pamoja na tozo mbalimbali, pia biashara katika eneo hilo imekuwa mbaya kutokana na kuhamishwa kwa stendi kuu ya mabasi kwenda Chibukuta.

“Tangu stendi kuu ilipohamishwa mzunguko wa biashara umekuwa mdogo. Tunaomba Serikali iruhusu daladala ziweze kushusha abiria katika stendi kuu ya zamani ili na sisi wafanyabiashara tupate wateja,” alisema Mtumba.

Kuhusu tozo, Mwaigobeko alisema Manispaa ya Mtwara-Mikindani inazo mbili tu ambazo ni leseni ya biashara na ushuru wa huduma (service levy).

Alisema mkurugenzi hana mamlaka juu ya tozo za taasisi nyingine.

“Nilishapata malalamiko ya wafanyabiashara ya samaki ambao kodi yao ni kubwa. Wanatakiwa kulipa Sh6 milioni ya leseni ya uvuvi. Tume ya Mionzi nayo inawatoza Dola za Marekani 2.5 kwa kila kilo moja ya samaki,” alisema Mwaigobeko.

Alisema “nimewasiliana na mkuu wa mkoa ili aweze kushughulikia hili kwa ngazi ya juu, mimi kama mkurugenzi sina mamlaka hayo.”

Mwananchi lilipomtafuta Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa azungumzie hilo, alijibu kuwa hana taarifa juu ya hilo.

Advertisement