Ulaji wa bamia kwa mwenye kisukari na faida zake

Fahamu kuwa bamia linaweza kukutoa katika hatari ya kupata ugonjwa wa kisukari kwa sababu ya uwezo wake wa kusaidia kuyeyusha au kumeng’enya sukari.

Pia, huweka sawa mfumo wa sukari mwilini. Bamia ni aina ya yenye utajiri wa makapimlo ambayo ni muhimu sana katika mwili hasa katika usagaji wa chakula.

Mara nyingi tumekuwa tukichukulia bamia kama mboga ya kimaskini pasipo kujua ni tunda mboga lenye faida nyingi sana.

Moja wapo ya faida ambayo ni muhimu ni kusaidia kumeng’enya sukari mwili au kuweka sawa mfumo wa sukari mwilini na pia tatizo la kukosa choo ni tatizo la kawaida kwa wagonjwa wa Kisukari.

Bamia ikiliwa mara kwa mara inasaidia kurekebisha mfumo wa umeng’enya chakula na sukari mwilini.

Maji maji yanayotoka katika bamia yana uwezo wa kuondoa lehemu katika mishipa ya damu kwenye mwili.

Lehemu ni aina ya mafuta yanayopatikana kwenye mishipa damu, endapo mafuta haya yakazidi huweza husababisha maradhi ya shinikizo la damu.

Mgonjwa wa kisukari mwenye shida ya lehemu muhimu kula bamia mara kwa mara.

Tukiachana na kisukari, bamia huongeza na uboresha kinga ya mwili hasa kwa watu ambao kinga yao ya mwili imeshuka kama watu wenye maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU).

Wataalamu lishe wanasema watu wengi wamekuwa wakila bamia kwa kuidharau ila huzuia magonjwa ya moyo kwa kuisaidia mishipa ya damu kufanya kazi vizuri.

Watu wenye matatizo ya vidonda vya tumbo, bamia huwasaidia kupunguza uwezekano wa kupata saratani ya tumbo na huongeza kiwango cha damu mwilini. Wengine wanatumia bamia kama dawa ya kuongeza kinga ya mwili kwa kutafuna zikiwa mbichi au kuzichemsha.

Angalizo kwa wagonjwa wa kisukari, msiache dawa zenu na kuanza kutumia bamia kama dawa. Tumia bamia mara kwa mara kama tunda mboga linalosaidia kumeng’esha sukari mwilini na kuimarisha kinga ya mwili wako.

Mwandishi wa makala haya anaishi na kisukari, muelimishaji na mshauri lishe kwa wagonjwa wa kisukari