Ummy Mwalimu aonya viongozi kuwadhalilisha wahudumu wa afya

Dodoma. Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amewataka viongozi wa Serikali kutowadhalilisha wataalamu wa kada hiyo akisema wanafanyakazi kubwa.

Ummy alisema hayo jana wakati wa kupitisha bajeti ya wizara yake ya Sh990.68 bilioni kwa mwaka wa fedha 2019/20. Alisema kutokana na uhaba uliopo, watumishi wa afya nchini wanafanyakazi kubwa hivyo wanahitaji kutiwa moyo badala ya kudhalilishwa.

“Mhudumu mmoja nchini anafanyakazi ya watu watano, tunapowadhalilisha tujue tunaowaumiza ni Watanzania maskini wanaowategemea kwani wenye hela wana mbadala. Wanapokosea wapelekwe kwenye mamlaka husika,” alisema.

Takwimu za Serikali zinaonyesha kuna watumishi 56,841 ambao ni sawa na asilimia 48 ya mahitaji.

Kauli ya Ummy haikutofautiana na ushauri uliotolewa na kambi rasmi ya upinzani iliyotahadharisha juu ya ongezeko la viongozi wa kisiasa kuingilia majukumu ya wataalamu hao hivyo kuzorotesha huduma kwa wananchi maskini.

Hata hivyo, licha ya kuunga mkono hoja hiyo, akisoma hotuba ya kambi hiyo, Mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Matiko alisema “majigambo ya Serikali kwamba imeboresha sekta ya afya nchini ni kujitafutia umaarufu wa kisiasa tu.”

Kauli hiyo ilijibiwa na waziri Ummy akisema asilimia 99 ya watoto chini ya miaka mitano sasa wanapata chanjo, wagonjwa wanapandikizwa figo na watoto wanapandikizwa vifaa vya usikivu huduma zilizokuwa hazipatikani awali.

“Nashangaza kusikia eti mafanikio yaliyopo ni kutafuta umaarufu wa kisiasa. Tutawasilisha muswada wa sheria ya bima ya afya Septemba. Hata hivyo, nikiri zipo changamoto ambazo tunaendelea kuzishughulikia,” alisema.

Licha ya maelezo hayo, Matiko alishika shilingi akiitaka Serikali kueleza mkakati wa kupunguza vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua ambavyo alisema vimeongezeka. Wizara ya Afya inatakiwa kutafuta majibu kwa maswali na hoja zilizoibuliwa na wabunge msisitizo mkubwa ukiwa kuhusu bima kwa wote na matunzo kwa wazee.

Wabunge waliochangia bajeti ya wizara hiyo walisisitiza utatuzi wa kero zinazozorotesha huduma kwa wananchi na kuitaka Serikali kuhakikisha wahudumu wanakuwapo kwenye vituo na uwepo wa dawa za uhakika.

Mbunge wa Nkenge (CCM), Dk Diodorus Kamala alisema juhudi za Serikali kujenga vituo vipya vya afya zimeleta changamoto mpya inayohiaji kushughulikiwa haraka iwezekanavyo.

“Mafanikio ni baba wa matatizo. Kadri vituo vya afya vinavyoongezeka ndivyo dawa na watumishi wanavyohitajika zaidi. Jimboni kwangu kuna uhaba,” alisema.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Azza Hamad alisema Ushetu ina upungufu wa watumishi 1,660 wa afya na vituo vipya 11 vilivyojengwa mkoani Shinyanga havijaanza kufanyakazi kutokana n kukosa vifaatiba hivyo wananchi kukosa huduma.

Mbunge wa Konde (CUF), Khatib Haji aliwasilisha kilio cha wagonjwa wa figo akisema alishawahi kuugua ugonjwa huo na kueleza kuwa gharama zake ni kubwa mno.

“Kwa siku, kusafisha damu inagharimu Sh180,000. Hizi ni gharama kubwa sana kwa mwananchi wa kawaida kumudu. Watanzania wengi wanakufa kwa kushindwa kuzimudu,” alisema Haji.

Alisema hata kwa wenye bima kuna changamoto kwa kuwa kuna maelekezo kwamba inatakiwa iwe imekaa kwa muda fulani kabla ya kutumika.

Ingawa Serikali inao mpango wa kuwatibu bure wazee, wabunge wamesema bado walengwa wengi hawajapewa vitambulisho wala kutungwa kwa sheria inayosimamia mkakati huo.

Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CUF), Vedasto Ngombale Mwiru alisema utekelezaji wa mpango huo unasuasua. “Wabunge tumechanjwa ugonjwa wa ini, nashauri chanjo hii itolewe kwa Watanzania wote,” alisema Vedasto.

Kuhusu miradi iliyoanzishwa, Mbunge wa Urambo (CCM), Margareth Sitta alisema jimboni kwake kuna jengo la upasuaji ambalo tangu lilipoanza kujengwa mwaka 2010 mpaka leo, halijakamilika.

“Urambo tuna upungufu wa wafanyakazi na hatuna (chumba cha wagonjwa mahututi) ICU, naomba Serikali ituangalie,” alisema Sitta.