VITA YA KAGERA: Mwalimu Nyerere ahamasisha wapiganaji - 7

Muktasari:

  • Jana tuliona habari za ushindi wa kuitwaa Kagera zilivyomfariji Mwalimu Nyerere, lakini inasemekana, hakufurahishwa na habari za mauaji yaliyofanywa na jeshi lake. Baadaye Nyerere alitoa amri ya maandishi kwa jeshi lake litofautishe jeshi na raia na mali zao. Vyovyote iwavyo, ushindi wa kwanza ukawa umepatikana kwa kuikomboa Mutukula. Siku JWTZ ilipovuka mpaka, Serikali ya Uganda ilitangaza kuwa wanajeshi zaidi ya 1,000 wa Tanzania wameingia maili 100 ndani ya Uganda na kuteka miji mitatu ya Kyotera, Kakuto na Kalisizo.

Miezi miwili ya mwanzo wa vita ilikuwa ni ya kuongeza idadi ya wanajeshi jeshini. Katika lile juma la kwanza vikundi vya wanamgambo vilianza kufanya mazoezi baada ya saa za kazi.

Miongoni mwa wanamgambo hawa walikuwamo wakulima wadogo na wale ambao hawakuwa na ajira. Jeshi la Polisi lilichangia askari wake kiasi cha 2,000.

Juma moja baada ya uvamizi wa Uganda wakuu wa mikoa yote 20 ya Tanzania walikutana mjini Dodoma kujadiliana kuhusu uandikishaji wa wapiganaji. Kila mkoa ulipewa idadi ya kikomo cha wapiganaji 2,000 na wakuu hao walipewa maelekezo ya kuwapokea wale tu ambao walikuwa wamehitimu mafunzo ya mgambo.

Pamoja na hayo, mkuu wa Mkoa wa Mara alipotangaza mkoani mwake kuwa yeyote ambaye anataka kujiunga na jeshi ajitokeze, wananchi wengi walimiminika kwenye vituo vya kuandikishwa. Vituo vya kijeshi mkoani Mara vilielemewa na idadi kubwa ya waombaji, mwishowe Rais Nyerere alikwenda mwenyewe mkoani humo kulikabili tatizo hilo.

Hatimaye mkoa huo ulikubaliwa kuandikisha wapiganaji 4,000 badala ya 2,000 wa kikomo waliokubaliwa awali, ilimradi tu hawakuwa na tatizo la akili, wana elimu ya angalau darasa la saba na ni wanachama wa CCM.

Kwa kutumia utaratibu huo wanamgambo 40,000 waliingizwa jeshini na kufanya idadi ya wapiganaji kufikia 75,000—au zaidi. Hatimaye wapiganaji 45,000 wa Tanzania wakaingia Uganda.

Ingawa wanamgambo wanawake nao walipata mafunzo ya kijeshi sawasawa na wale wa wanaume, hakuna mgambo mwanamke aliyeingia jeshini kupigana vita isipokuwa tu wale waliotumika kama wauguzi.

Mara baada ya uvamizi wa Kagera, Tanzania ilianza kuwahamasisha Waganda waliompinga Idi Amin kupigana dhidi ya Idi Amin. Kufikia hatua hii, mkataba wa Mogadishu— ambao ulilitaka jeshi letu kukaa umbali wa kilomita 16 au zaidi kutoka kwenye mpaka wa Uganda—ukawa umekufa rasmi.

Mkataba huo ulioitwa ‘Mazungumzo ya Mogadishu’ uliafikiwa nchini Somalia Alhamisi ya Oktoba 5, 1972. Ulikuwa ni sehemu ya usuluhishi wa mgogoro kati ya Tanzania na Uganda. Somalia iliepusha vita kati ya Tanzania na Uganda kwa miaka sita tangu 1972 hadi ilipokuja kuzuka baadaye mwaka 1978 na sasa, wakati vita inaendelea, ukawa hauna kazi tena.

Walioshiriki katika mazungumzo hayo ni mawaziri wa mambo ya nje ambao ni John Samuel Malecela (Tanzania), Joshua Wanume Kibedi (Uganda) na Umar Arteh Ghalib au Omer Carte Qalib (Somalia). Mwingine aliyeshiriki ni Katibu Mkuu wa OAU, Nzo Ekangaki.

Kufikia hatua hii Rais Nyerere alisema waziwazi kuwa anaunga mkono wanaompinga Idi Amin na kwamba angetoa mafunzo, silaha na fedha kwa Waganda wowote ambao wangekuwa tayari kwenda Uganda kumpiga.

Wito huo uliitikwa na makundi mbalimbali. Wengine walikuwa wanaishi nchini Tanzania, Kenya, Zambia, nchi za Ulaya na Amerika pamoja na Waganda waliokuwa ndani ya Uganda kwenyewe.

Baadhi ya hawa hawakuwa wapiganaji. Wengine walikuwa wafanyabiashara, walimu au waandishi wa habari. Kwa hiyo hawakuwahi kubeba silaha wakati wowote.

Sehemu kubwa ya hawa ilitokea Tanzania, hususan kwenye kambi ya wakimbizi ya Tabora.

Wengi wao walikuwa katika jeshi la Obote, lakini tangu waliposhindwa katika jaribio lao la mwaka 1972 la kumwangusha Idi Amin hawakuendelea tena kupata mafunzo ya kijeshi.

Baadhi ya wengine hawangeweza tena kuingia kwenye mapambano ya kivita kwa sababu ya uzee.

Hata hivyo, siku chache baada ya uvamizi wa Idi Amin, Obote ambaye alikuwa amekwenda Zambia, alirejea Tanzania haraka na kuanza kuwakusanya makomandoo wa kijeshi kutoka Dar es Salaam na kwingineko.

Wanajeshi wote wa zamani wa Uganda walitakiwa kukutana Tabora kwa mkakati maalumu dhidi ya Idi Amin. Ndani ya wiki moja tu ya wito huo wakakutana 800 chini ya Kanali Tito Okello, ambaye ndiye alikuwa kamanda wa lile jaribio la mapinduzi la mwaka 1972.

Kufikia katikati ya Novemba 1978 kiasi cha wapiganaji 300 miongoni mwao wakawa wamepewa sare za kijeshi na kupelekwa Mwanza ambako walikutana na wenzao wengine ili wapelekwe vitani Uganda.

Mwalimu Nyerere alitaka kikosi cha Waganda hao kiende vitani haraka iwezekanavyo, lakini Obote akapinga akidai kikosi chake cha Tabora kimeganyika na kilihitaji muda kuwekwa sawa. Lakini wengine walisema Obote alihisi kikosi hicho kinamtii zaidi Kanali Okello kuliko yeye.

Okello na wapiganaji wengi walikuwa wa kabila la Acholi na ingawa wakati mmoja Obote alidai kuwa watu hao wa Tabora walikuwa watiifu kwake, wakimbizi wengi wa kabila la Acholi waliona kuwa Obote aliwapuuza wakati wa utawala wake kabla ya kupinduliwa na Idi Amin mwaka 1971.

Wengi wao walikuwa wakidai kuwa wakati Obote akiwa madarakani aliwapendelea watu wa kabila lake la Langi kwa kuwapa ajira na fursa nyingine ambazo wao walinyimwa.

Hata hivyo Nyerere alimsikiliza sana Obote na hivyo aliamuru wapiganaji 300 waliokuwa wameshawasili Mwanza warudi Tabora ambako Obote na Okello wangekubaliana kuwa hao wawe kwenye batalioni moja. Kwa mujibu wa kitabu cha War in Uganda, Tanzania iliwapatia silaha na makamanda wa Uganda wakaanza kutoa mafunzo mara moja.

Wakati huohuo, Nyerere alianzisha kambi ya mafunzo ya Uganda huko Tarime karibu na Musoma. Ilikuwa na uwezo wa kutoa mafunzo kwa wapiganaji 1,200. Nyerere aliwataka Waganda wengine, akiwamo Robert Serumaga na Roger Makasa.

Wengine ni Andrew Adimola wa chama cha Ugandan Redemption and Reconciliation Union. Robert Bellarmino Serumaga ambaye alikuwa mwandishi, aliukimbia utawala wa Idi Amin mwaka 1977. Adimola alikuwa waziri kabla hajakimbia. Mwingine ni Aleker Ejalu. Nyerere aliwasihi wote hawa wahamasishe wapiganaji.

Itaendelea kesho