Vigogo tisa kula Krismasi mahabusu

Sunday December 16 2018

 

By Hadija Jumanne, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Huenda vigogo tisa wanaokabiliwa na kesi zilizo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakasherehekea sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya wakiwa rumande kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya upelelezi kutokamilika.

Lakini wengine kesi zao hazina dhamana na wengine wamefutiwa dhamana.

Miongoni mwa vigogo hao ni pamoja na Harry Kitilya na maofisa wa zamani wa benki ya Stanbic; Shose Sinare na Sioi Solomon wanaosota rumande kwa takribani miaka miwili na miezi minane kutokana na upelelezi wa shauri lao la utakatishaji fedha kutokamilika. Wote walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Aprili Mosi, 2016.

Kitilya, ambaye ni mwenyekiti wa kampuni ya Uwekezaji wa Mitaji na Dhamana (Egma), pia aliwahi kuwa kamishna mkuu wa TRA. Mbali ya Kitilya wamo pia mkurugenzi mkuu wa zamani wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (Rahco), Benhadard Tito; mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe; wafanyabiashara Habinder Seth na James Rugemarila.

Wengine ni Yusuf Ali maarufu kama Shehe au Mpemba, Mohamed Mustafa Yusufali, Dk Ringo Tenga na mkurugenzi wa uthaminishaji almasi na vito Tanzania (Tansort), Archard Kalugendo.

Vigogo wa Rahco

Mkurugenzi mkuu wa zamani wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (Rahco), Tito na wenzake wawili; mwanasheria wa Rahco, Emmanuel Massawe na mfanyabiashara na mwakilishi wa Kampuni ya Rothschild (South Afrika) Proprietary Ltd, Kanji Mwinyijuma wanakabiliwa na mashtaka manane. Walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Machi 14, 2016 kujibu mashtaka hayo ikiwemo kuisababishia hasara Serikali, lakini hadi sasa upelelezi haujakamilika. Kesi yao itatajwa tena Desemba 27, 2018.

Viongozi wa Chadema

Uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumfutia dhamana mwenyekiti wa Chadema, Mbowe na mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko kutokana na kukiuka masharti huenda ukasababisha wawili hao kula Krismasi mahabusu.

Seth na Rugemarila

Wafanyabiashara Seth na Rugemarila wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na wanaendelea kusota rumande kutokana na upelelezi wa shauri hilo kutokamilika. Walifikishwa Kisutu Juni 19, 2017 kujibu mashtaka 12 yakiwemo ya utakatishaji fedha. Kesi yao itatajwa tena Desemba 20.

‘Mpemba’ wa Magufuli

Yusuf Ali maarufu kama Shehe au Mpemba aliyewahi kutajwa na Rais John Magufuli kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo na wenzake watano wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi. Wengine ni Charles Mrutu, Benedict Kungwa, Jumanne Chima, Ahmed Nyagongo na Pius Kulagwa ambao walifikishwa mahakamani hapo Novemba 16, 2016. Upelelezi wa kesi yao haujakamilika na itatajwa tena Desemba 18.

Kesi ya wizi wa Sh7 milioni kwa dakika

Kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili wafanyabiashara watano; Mohamed Mustafa Yusufali, Alloyscious Gonzaga Mandago, Isaac Wilfred Kasanga, Taherali Sujjauddin Taherali na Mohamed Seif Kabla.

Yusufali aliwahi kutajwa na Rais Magufuli kuwa ana mashine inayotoa risiti za kielektroniki (EFD) nje ya mfumo wa TRA na huzisambaza kwa wafanyabiashara wengine, hivyo kujiingizia Sh7 milioni kwa dakika. Wote walifikishwa Kisutu Julai 2016 na kesi yao itatajwa tena Desemba 19.

Dk Tenga na wenzake

Vigogo wa kampuni ya mawasiliano ya Six Telecoms Limited akiwemo wakili maarufu Dk Tenga wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi. Wengine ni mhandisi Hafidhi Shamte au Rashidi Shamte; mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo, Peter Noni; mkuu wa fedha, Noel Chacha na Six Telecoms yenyewe. Wanakabiliwa na mashtaka sita na walifikishwa mahakamani hapo Novemba 20, 2017. Upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na itatajwa tena Desemba 21.

Shauri jingine mahakamani hapo linawahusu mkurugenzi wa uthaminishaji almasi na vito Tanzania (Tansort), Kalugendo na mthamini wa almasi, Edward Rweyemamu ambao ni waajiriwa wa Serikali wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara. Kesi hiyo itatajwa tena Desemba 17.

Advertisement