Viwanda vya dawa vyatangaziwa ‘dili’

Thursday December 6 2018

 

By Kalunde Jamal, Mwananchi [email protected]

Serikali hutumia dola milioni 100 za Marekani (takribani Sh220 bilioni) kuagiza dawa nje ya nchi kila mwaka.

Hatua hiyo inatokana na viwanda vya ndani vya dawa kutokuwa na uwezo wa kuzalisha bidhaa za kutosheleza mahitaji ya nchi.

Pamoja na changamoto zilizopo, juhudi za Serikali kuendeleza sekta hiyo zinatajwa kuzaa matunda baada ya kuelezwa kuwa soko la dawa la Tanzania linatarajiwa kukua kwa dola 250 milioni (Sh572.6 bilioni) katika miaka minne ijayo.

Dk Jude Benjamin kutoka Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji akizungumza wakati wa mkutano wa mnyororo wa ugavi wa dawa nchini ulioandaliwa na taasisi ya Tanzania Health Summit (HSC), anasema ukiaji huo ni ishara njema kwa soko hilo.

Alisema uchambuzi wa masuala ya uchumi, viwanda na masoko ya fedha (BMI) unaonyesha, soko hilo litafikia dola milioni 700 (Sh1.6 trilioni) mwaka 2021 kutoka dola 450 milioni (Sh1.03 trilioni) mwaka 2017 ikiwa ni ongezeko la dola 250 milioni sawa na Sh 572.6 bilioni.

Dk Benjamin anasema vyanzo vya kimataifa likiwamo Shirika la Afya Duniani (WHO), vinaonyesha kuwa soko hilo katika kipindi cha miaka 10 limekuwa kutoka dola 107 milioni (Sh245.1 bilioni) mwaka 2007 mpaka dola 450 milioni (Sh1.03 trilioni) mwaka 2017.

Anasema sekta hiyo kwa ujumla inatarajiwa kukua kutoka dola 47 milioni (Sh107.6 bilioni) mpaka dola 497 milioni (Sh1.14 trilioni).

Dk Benjamin anasema: “Ukuaji wa soko hilo unatokana na jitihada za serikali za kuchochea ukuaji wa viwanda nchini na kuongeza ufanisi wa mkakati wa nchi kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025”.

Anasema mapato yanayotokana na viwanda vya dawa yataongezeka kama uwekezaji katika sekta hiyo utaongezeka na kuwapo kwa msisitizo wa kutumia dawa na vifaa tiba vilivyozalishwa nchini.

“Serikali ina mikakati mingi kufanikisha hilo ikiwamo utekelezaji wa mpango wa maendeleo endelevu ya viwanda (SIDP) ambapo kutakuwa na kiwango kikubwa cha mazingira rafiki ya biashara,” anasema.

Anasema kati ya mwaka 2012 na 2025, Serikali itatekeleza Mpango wa Maendeleo ya Viwanda (IIDP) wenye malengo mbalimbali ikiwamo kuboresha sekta ya viwanda, kuongeza mchango kwa pato la taifa, mapato na thamani ya fedha kutokana na uwepo wa wigo mpana wa kuuza bidhaa nje ya nchi.

Anaeleza kuwa mchango wa sekta ya viwanda utaongezeka kutoka asilimia 6.59 hadi asilimia 23 kufikia mwaka 2025, huku sekta hiyo ikitarajiwa kukua kutoka asilimia 8.4 hadi 15 kila mwaka.

“Thamani ya bidhaa zinazotolewa kutoka sekta hiyo zitazalisha dola 16.8 bilioni za Marekani (Sh38.49 trilioni) mwaka 2025 na mauzo ya bidhaa za nje yatachangia dola 6.6 bilioni (Sh16.12 trilioni) ifikapo mwaka 2025,” anasema. Anabainisha kuwa kwa sasa nchi ina viwanda 14 vinavyozalisha dawa za binadamu na mifugo ingawa uzalishaji wake bado uko chini.

Aliorodhesha baadhi ya vifaa tiba na dawa ambazo fursa yake ipo wazi kwa wawekezaji ni maboksi ya kuhifadhia sindano zilizotumika, ya kuhifadhia dawa, bahasha za kuhifadhia dawa, fomu za kuandikia dawa (A5), mipira ya kutandika kwenye vitanda vya wagonjwa na madaftari ya kuorodhesha majina ya wagonjwa.

Kwa upande wa Irinei Kiria Mkurugenzi wa taasisi inayojishughulisha na masuala ya afya ya Sikika, anasema suluhisho la changamoto kubwa inayoikabili sekta ya dawa ni bajeti finyu inayosababisha baadhi ya dawa kukosekana hospitalini. Anasema licha ya Sh270 bilioni kutengwa kwa ajili ya ununuzi wa dawa, lakini hazitolewi zote na hazifiki kwa wakati

Advertisement