Wabunge Chadema ‘wamshughulikia’ Mtulia wa CCM hadi amekubali yaishe

Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia akifuta kauli bungeni iliyowakwaza wabunge wa kambi ya upinzani, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Wabunge wa Chadema wamemshukia mbunge wa Kinondoni kutokana na kauli yake, lakini mbunge huyo ameifuta

Dodoma. Wabunge wa Chadema wamemshukia mbunge wa Kinondoni (CCM), Maulid Mtulia kutokana na kauli yake kuwa baadhi ya wabunge wa chama hicho walipatikana kwa aibu.

Kelele nyingi zimeibuka ndani ya Bunge jijini Dodoma Tanzania leo Ijumaa Aprili 12,2019 wakimtaka Mtulia kuthibitisha jambo hilo au vinginevyo alitakiwa kufuta kauli yake.

Mtulia amekutana na maswahibu hayo kutokana na taarifa aliyoitoa wakati mbunge wa Viti maalumu (Chadema), Grace Kihwelu alipokuwa akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa wizara zilizo chini ya ofisi ya Rais (Tamisemi, Utumishi na Utawala Bora)

Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko akiomba mwongozo wa Mwnyekiti wa Bunge kufuatia Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia kutoa kauli iliyowakwaza wabunge wa kambi ya upinzani, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Mbunge wa Tarime mjini (Chadema), Esther Matiko ameomba mwongozo wa Spika kwa kutumia kanuni ya 64 kuhusu utaratibu ambapo amemtaka Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge kumweleza Mtulia athibitishe aibu gani wanayoifanya Chadema hata kupata ubunge.

"Mheshimiwa mwenyekiti, sisi sote humu ndani tunaingia kwa kupigiwa kura na wananchi na kufuata utaratibu, naomba mbunge atuambie aibu gani walifanya wabunge wa upande huu hata wakapata ubunge," amesema Matiko

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Grace Kiwelu akichangia bungeni mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais (Tamisemi) na Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Wakati mbunge huyo akitoa taarifa yake, wabunge wengi walikuwa wakipiga kelele na baadhi kuzomea jambo lililowafanya wabunge wa CCM kusimama akiwemo Magreth Sitta waliokuwa wakimtaka Mtulia kufuta kauli yake.

Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge akizungumza bungeni alipokuwa akiongoza kikao cha tisa cha mkutano wa Bunge la Bajeti, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Chenge alimpa nafasi Mtulia kuchagua kama anaweza kufuta kauli au anaweza kuthibitisha kauli yake lakini alichagua kuifuta

Akitoa mchango wake Kihwelu alimtuhumu Mtulia na kutoa maneno yaliyoonyesha kumchongea kwa wapiga kura wake wa kike katika jimbo la Kinondoni.