Waziri afagilia NSSF, ataka waongeze nguvu kuongeza wanachama

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa baraza la wafanyakazi la Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), muda mfupi baada ya kuzindua baraza hilo, mwishoni mwa wiki mjini Morogoro.

Muktasari:

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama ameipongeza Bodi ya wadhamini na menejimenti ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jami (NSSF) huku akiitaka kuongeza nguvu katika kuandikisha wanachama kwa sababu sekta binafsi ina wanachama wengi wanaotakiwa wajiunge katika shirika hilo.

Morogoro. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, ameipongeza Bodi ya Wadhamini na Menejimenti ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kufanya mabadiliko ndani ya muda mfupi ikiwemo kuboresha uendeshaji wa shirika hilo.

Jenista ameyasema hayo mwishoni mwa wiki, wakati akifungua mkutano wa baraza la 45 la wafanyakazi wa NSSF lililofanyika mkoani Morogoro.

Amesema bodi ya wadhamini na menejimenti imeboresha uendeshaji wa Shirika kwa kujiunga na mifumo ya kielektroniki kama mfumo wa malipo wa serikali wa kielektroniki (GePG), ambapo waajiri wanatumia mfumo huo kuwasilisha michango NSSF.

Amesema mfumo wa kielektroniki wa uhasibu (Orcale Financial System) ni kati ya mifumo ambayo imeboresha utendaji wa Shirika katika kipindi kifupi.

Amesema faida za mifumo hiyo ni kusaidia kupunguza malalamimo ya wanachama ikiwa ni pamoja na kupata malipo yao kwa wakati.

Pia, alisisitiza uwajibikaji kwa watendaji wa shirika hilo kwa kutumia mabaraza hayo kwa sababu yapo kisheria.

“Menejimenti, mheshimiwa mwenyekiti wa bodi (Balozi Siwa) mmenifariji sana. Lakini nimeona mmetengeneza mfumo wa kielektroni wa kihasibu, hongereni mmefanyakazi nzuri," amesema Jenista.

Waziri Jenista ameitaka menejimenti kuongeza nguvu katika kuandikisha wanachama kwa sababu sekta binafsi ina wanachama wengi wanaotakiwa wajiunge katika Shirika hilo.

Alisema hatavumilia kwa mtendaji yoyote ambaye hatafikia malengo waliyojiwekea katika shirika hilo.

Waziri Jenista amesisitiza kampuni binafsi kujiunga na NSSF, kwa mujibu wa mabadiliko ya sheria ya mwaka 2018.

Amewataka wafanyakazi wa Shirika hilo kuacha kukaa ofisini na badala yake waende kuandikisha wanachama wapya.