Waziri akerwa ubambikiaji kesi

Waziri wa Katiba na Sheria,Dk Augustine Mahiga akizungumza wakati wa kongamano la watoa huduma za Msaada wa Kisheria jijini Arusha jana,kushoto ni Msajili wa Watoa Huduma za Msaada wa Kisheria,Felister Mushi,Katibu Mkuu wa Wizara ya Sheria na Katiba,Profesa Sifuni Mchome na kulia ni Katibu Tawala Msaidizi mkoa wa Arusha,Hegnery Chitukulo.Picha na Filbert Rweyemamu

Arusha.Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Augustine Mahiga amesema moja ya changamoto inayoikabili Serikali katika kuhakikisha kunakuwapo na utawala wa sheria na wananchi kuifurahia Serikali yao ni kukomesha matukio ya kuwabambikia kesi.

“Nakumbuka hivi karibuni Waziri Mkuu alituita Dodoma kwa ajili ya maandalizi ya kikao cha bajeti, tukiwa tumeshamaliza nikiwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alikuja mama mmoja akatuambia mnapaswa kumaliza kero ya watu kubambikiwa kesi,” alisema Dk Mahiga jana wakati akifungua kongamano la kwanza la watoa huduma za kisheria mjini hapa.

Alisema uwepo wa watu hao umesaidia kupunguza vitendo vya uonevu wanavyofanyiwa baadhi ya wananchi ambao hawawezi kumudu gharama za mawakili.

Waziri huyo alisema dhamira ya Serikali ni kuwahudumia wananchi vizuri hasa katika eneo la kisheria na ndio maana iliona umuhimu wa kuwa na Sheria ya Watoa Huduma za Msaada wa Kisheria ya mwaka 2017 baada ya kubaini kuwapo kwa wananchi wanaodhulumiwa mali au kufungwa gerezani kwa kutofahamu sheria.

Alisema katika kipindi kifupi tangu kuanza matumizi ya sheria hiyo, wizara yake haijafikia malengo waliyojiwekea lakini kumekuwapo na mafanikio yanayoendelea kuigusa jamii.

Dk Mahiga alisema Serikali inatambua kuwapo kwa washtakiwa mahakamani ambao hawawezi kuelewa maana ya mashtaka wanayosomewa na wengine wanakiri makosa ambayo hawakutenda kwa kutojua nini cha kusema na namna ya kukisema.

Awali, katibu mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome aliwataka wasaidizi wa kisheria kutofautisha kazi yao na ya wanaharakati ili kuwawezesha wananchi wasio na uwezo kupata huduma inayostahili.

Alisema kazi ya watoa huduma za msaada wa kisheria ni kuwawezesha wananchi wasio na uelewa na ambao kwa namna moja ama nyingine wapo hatarini kudhulumiwa haki zao, na kwamba jukumu lao ni kuwatetea.

Msajili wa Watoa Huduma za Msaada wa Kisheria, Felister Mushi alisema lengo la kongamano hilo ni kuwaleta pamoja watoa huduma hao kuielewa sheria na namna ya kutekeleza wajibu wao bila kukinzana na sheria.