Ziara ya Liquid bungeni yaibua mjadala

Mbunge wa kuteuliwa, Mama Salma Kikwete akiwa   na Peter Moller maarufu,  Pierre katika viwanja Bunge jijini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi

Dar es Salaam. Wakati Bunge likiazimia kutofanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), chombo hicho cha kutunga sheria kimeibua na mijadala mitatu, ukiwemo unaomuhusu Pierre Liquid ambaye ameibukia kuwa maarufu jijini Dar es Salaam.

Jana asubuhi, kulikuwa na video katika mitandao ya kijamii inayomuonyesha Spika Job Ndugai , Liquid, ambaye jina lake halisi ni Peter Mollel, Naibu Spika Tulia Ackson na watu wengine wakifurahia jambo katika viwanja vya Bunge.

Picha nyingine zilimuonyesha Liquid akiwa eneo la wageni katika ukumbi wa Bunge. Haikufahamika kama Spika Ndugai alimkaribisha au alikuwa katika moja ya ziara ambazo amekuwa akizifanya tangu achomoze kuwa maarufu.

Mbali na tukio hilo, Spika Ndugai alikaririwa akisema baadhi ya wabunge wanakabiliwa na msongo, akimtaja mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema kuwa ana mkopo wa Sh419 milioni kati ya Sh644milioni.

Pia Spika amesema kuwa ana ujumbe wa malalamiko kutoka kwa baadhi ya wanawake kuwa baadhi ya wabunge wametelekeza watoto wao.

Masuala hayo yamepokewa kwa mitazamo tofauti na wachambuzi.

“Ni kweli (suala la Liquid) linaweza kuathiri mjadala wa CAG, lakini siyo kwa kundi la watu makini,” alisema Dk Richard Mbunda kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM).

“Watu wanajadili sasa kwa kuhusisha na issue (suala) ya CAG. Wanasema kwa utani Bunge limekataa kufanya kazi na CAG na badala yake litafanya kazi na Konki Liquid.

“Huo ni utani lakini bado wanajaribu kukumbuka sakata la CAG. Pengine labda inategemea na mitandao ya kijamii inayotumika katika mjadala huu,” alisema.

“Lakini kwa watu makini bado wanajadili na kuhoji maswali ambayo hayajapatiwa majibu.”

Ziara ya Liquid, ambaye amejipatia umaarufu kutokana na video zinazomuonyesha akiwa baa, pia ilipingwa na baadhi ya wabunge.

“Leo Bunge lipo kwa ajili ya maswali na majibu na linaahirishwa, ila unampa mtu dakika tano kumtambulisha Pierre? Natambua mchango wake, lakini hatukupaswa kupoteza muda wa Bunge,” alisema mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Matiko.

Mbunge wa Manonga (CCM), Seif Gulamali alisema, “Unajua hili ni Bunge la Watanzania , wananchi wote wana haki kuja kujifunza.”