Mifugo 5,000 yaugua magonjwa ya kupe kila mwaka

Monday March 25 2013

 

By Joseph Lyimo, Mwananchi

Yadaiwa magonjwa yote yanaambukizwa na kupe kutokana na kukosa majosho.

Hanang’. Zaidi ya  mifugo 5,000 huugua na 600 kati ya hiyo  hufa kila mwaka kutokana na maradhi yaletwayo na kupe, ilielezwa.

Baadhi ya madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo walisema hayo kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo, yaliyoandaliwa na asasi isiyo ya kiserikali ya nchini Uholanzi ya (SNV) na Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi.

Madiwani hao waliazimia kutoa msukumo kwa jamii,ili majosho yaliyoharibika wayatumie pindi yakitengenezwa,kwani kati ya majosho 21 ni sita yaliyo na hali nzuri, 10 yanahitaji matengenezo na manne yanahitaji kujengwa upya.

Madiwani hao walidai kuwa wenyewe ndiyo wanapitisha bajeti ya halmashauri ya wilaya hiyo, hivyo wapo tayari kuidhinisha kwenye bajeti zao fedha za kuboresha majosho na ununuzi wa dawa za kuogeshea mifugo.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ Felix Mabula alisema wilaya hiyo ni miongoni mwa wilaya zenye mifugo mingi mkoani Manyara na inaingiza mapato mengi hivyo ni wajibu kuijengea mazingira bora.

“Kwa vile madiwani wamejengewa uwezo wa kutambua madhara ya kutoogesha mifugo, naamini wataufikisha ujumbe huu kwa jamii ya maeneo yao ili zoezi la kuogesha mifugo lianze kwenye majosho yote,” alisema Mabula.  

Kwa upande wake, Ofisa mifugo na uvuvi wa halmashauri ya wilaya hiyo, Dk Tom Maeda alisema majosho yanayofanya kazi yapo kwenye Vijiji vya Dirma, Dawar, Gitting, Mureru na Gendabi.

Advertisement