Benki ya kichina yazinduliwa Tanzania, yaahidi kuongeza mtaji

Thursday November 29 2018

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (wa

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (wa pili kutoka kushoto), Balozi wa China nchini, wang Ke, Mwenyekiti wa Kituo cha huduma kwa wachina nchini, Zhu Jinfeng (wa pili kushoto), Meneja Idara ya Usimamizi wa Mabenki wa Benki ya Kuu ya Tanzania (BOT), Sadati Musa (wa kwanza kulia) na  Mwenyekiti wa China Dasheng Bank Limited, Yu Jia Qin (wa pili  kulia), wakikata utepe kuashiria uzinduzi wa benki ya China Dasheng Bank Limited jijini Dar es Salaam. Picha na Anthony Siame 

By Kalunde Jamal, Mwananchi [email protected]

Wakati sekta ya fedha ikianza kuimarika, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeipa leseni China Dasheng Bank iliyoanza kutoa huduma Jumatatu ya wiki hii jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa uzinduzi mwishoni mwa wiki iliyopita, mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya benki hiyo, Yu Jiaqin alisema wataanza na tawi moja na kutanuka kadri mazingira yatakavyoruhusu.

Benki hiyo inamilikiwa na kampuni sita za Kichina zikiwamo nne za sekta binafsi kutoka Mji wa Shanghai na Jiangsu na za umma.

“Tunaanza na mtaji wa Dola 40 milioni za Marekani ambazo ni sawa na Sh93 bilioni. Tunalenga kutoa huduma kwa kampuni kubwa za kichina zinayofanya miradi mbalimbali nchini na kuwahudumia Watanzania wanaofanya biashara na China ikizingatia,” alisema.

Kwa upande wake, naibu ofisa mtendaji mkuu wa benki hiyo, Nunu Saghaf alisema shughuli zao zitalenga kuisaidia Serikali kufanikisha malengo ya kuwa na uchumi wa kati unaotegemea viwanda ifikapo mwaka 2025.

“Hii ni benki inayomilikiwa na Wachina lakini imeanzishwa Tanzania. Hapa ndipo yalipo makao makuu yake ingawa ipo mipango ya kuwa na matawi hapo baadaye,” alisema Nunu.

Balozi wa China nchini, Wang Ke alisema kufunguliwa kwa benki hiyo ni ishara ya ushirikiano madhubuti na wa muda mrefu baina ya nchi hizi mbili. Benki hiyo, alisema itaboresha huduma za fedha na kuwa na manufaa kwa wafanyabiashara kutoka China na Tanzania.

“China imefanya mageuzi makubwa ya kiuchumi ikitoka kwenye umasikini na kuwa ya pili kwa uchumi mkubwa duniani. Hili linawezekana pia kwa Tanzania,” alisema Balozi Ke.

Benki hiyo imepewa leseni baada ya benki saba kufungwa ndani ya miaka miwili iliyopita. Zilizofungwa kuanzia mwaka 2016 mpaka sasa Benki za Wananchi Mbinga, Njombe na Meru, Efatha, Benki ya Wakulima Kagera na Benki ya Convenant.

Wakati benki hizo zikifungwa kutokana na kutokidhi masharti ya BoT hasa upungufu wa mtaji, Twiga Bancorp ililazimika kuungana na Benki ya Posta Tanzania (TPB) huku Benki M ikiwa chini ya usimamizi wa BoT.

Kwa mtaji ilionao China Desheng Bank, ni mkubwa kuliko wa benki sita zilizofungwa.

Mchumi na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (KIU), Dk Bravious Kahyoza anasema ni jambo jema kukaribisha wawekezaji wenye mtaji mkubwa kama benki hii.

“Tatizo tulilonalo kwa muda mrefu ni menejimenti na mtaji. Takwimu zinaonyesha sekta ya huduma zikiwamo za fedha inachangia takriban asilimia 50 ya pato la Taifa kwa nchini nyingi Afrika,” anasema.

endapo Tanzania itakopa au kuomba msaada kutoka China kwa ajili ya kutekeleza mradi wowote utakaosimamiwa na kampuni ya Kichina itakayoitumia benki hii: “Tutakuwa na uchumi hewa.”

Anasema China ikitoa fedha ambazo zitapitia benki hiyo ambayo inakusudia kuzihudumia zaidi kampuni za Kichina zenye miradi nchini, maana yake fedha hizo hazitaingia kwenye mzunguko nchini.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliyekuwa mgeni rasmi wa uzinduzi wa benki hiyo alisema anafuraha kubwa kuona benki yenye mtaji mkubwa inafunguliwa kwani itaongeza mtaji kwa wawekezaji na wafanyabiashara wa Kitanzania.

Alisema mkoa utatoa ushirikiano unaotakiwa.

“Mimi binafsi nimeenda China, dhana kuwa ni wajanja kibiashara ni potofu cha msingi ni kushirikiana nao kwa manufaa ya nchi zetu,” alisema Makonda.

Katika kuimairisha ushirikiano na jamii ya Wachina, Makonda alidokeza kuwa mkoa utaandaa mkutano wa kubaini changamoto wanazokutana nazo wafanyabiashara ili kuzitatua.


Advertisement