UCHOKOZI WA EDO: Dar inavyoipelekesha puta Tanzania

Tuesday January 29 2019Edo  Kumwembe

Edo  Kumwembe 

Wakati mwingine nawaza. Dar es Salaam ni Tanzania au Tanzania ni sehemu ya Dar es salaam. Kipi kikubwa kati ya viwili hivyo? Usidhani nimewaza kijinga, hapana. Nimefikiria mbali sana. Nimefikiria jinsi watu wa Dar es Salaam wanavyowapa shida wenzao wa mikoani.

Kwa mfano, tafsiri ya maendeleo makubwa yanayofanyika nchini kwa sasa asilimia kubwa ni yale mambo makubwa yanayofanyika Dar es Salaam. Kuna barabara ya hewani pale Tazara. Kuna barabara ya hewani nyingine nadhani inakuja Ubungo. Muda si mrefu unaweza kusikia kuna barabara ya hewani pale Mwenge.

Kuna madege makubwa yananunuliwa yanatua Dar es Salaam, kuna daraja la Kigamboni, kuna barabara nane zinazotarajiwa kujengwa kuanzia Dar es Salaam hadi mkoani Pwani pale Kibaha. Ni maendeleo makubwa.

Hizi ni silaha nzuri wakati wa uchaguzi, lakini wakati mwingine unawaza wananchi wa Njombe na Newala watashawishiwa vipi kwamba hayo maendeleo makubwa ya barabara za hewani Dar es Salaam yanawagusa na wao? Pengo la Dar es Salaam na wengine ni kubwa kuliko pengo la Maputo na Nampula.

Tuachane na siasa. Mitandaoni sasa kuna watu wanaibuka na umaarufu ambao hata watu wa mikoani hawauelewi. Kwa mfano kuna jamaa mlevi anaitwa Pierre. Jamaa mfupi hivi. Ameingia katika umaarufu mkubwa mitandaoni kwa sababu ya ulevi. Inaelekea watu wa mikoani wanateseka sana kutaka kumuona. Mikoani kuna walevi wengi kuliko yeye lakini yeye amekuzwa kutokana na umaarufu wa Dar es Salaam mitandaoni.

Jiulize kuhusu usumbufu wa Dokta Shika. Ghafla watu wa Dar es Salaam wakamtia umaarufu mkubwa mitandaoni kwa kuharibu mnada wa nyumba za kifahari. Watu wangapi wanaharibu minada mikoani?

Advertisement

Imefikia wakati sasa watu wa Dar es Salaam wanataka mkuu wa mkoa wa Tabora, Agrey Mwanri ahamishiwe Dar. Hawaamini mtu wa aina yake, mwenye burudani za namna yake, anastahili kuwa mkazi wa Tabora.

Kutoka katika nguvu ya mitandao ya kijamii hadi maendeleo makubwa tunayojaribu kufanya, inaonekana kama vile Dar es Salaam inaleta tafsiri ya Tanzania. Sawa, ndilo jiji kubwa zaidi, lakini hata hivyo taswira tuliyotengeneza kwamba Dar es Salaam ndio Tanzania ni kubwa sana.

Advertisement