VIDEO: Simulizi ya mwandishi jinsi meneja mawasiliano wa TFS alivyofia mbele ya waandishi wa habari

Muktasari:

Hakuna ajuaye siku wala saa. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya meneja mawasiliano wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Glory Mziray kufariki dunia leo mchana Jumanne Februari 19, 2019

Dar es Salaam. Hakuna ajuaye siku wala saa. Ndivyo unavyoweza kuelezea jinsi meneja mawasiliano na uhusiano wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Glory Mziray alivyo maliza safari yake ya mwisho duniani jana mchana.

Glory alifikwa na mauti jana akiwa ofisini kwake jengo la Mpingo (zamani Wizara ya Maliasili na Utalii).

Jana, TFS iliitisha mkutano na waandishi wa habari na mzungumzaji alikuwa Glory ambaye aliingia ukumbini akiwa amevalia suruali na blauzi nyeusi, koti jekundu, viatu vya rangi ya kahawia na kichwani akiwa amesuka nywele za mtindo wa Afro King za kuachia.

Alionekana akiwa amejiandaa vilivyo kutekeleza jukumu lake, lakini Mungu alikuwa na makusudi mengine kwake.

Mwandishi Wetu, Elizabeth Edward alipowasili katika ukumbi wa mkutano alimkuta marehemu akiwa tayari ameketi kwa ajili ya kuanza kuzungumza.

“Tukasalimiana na utani wa hapa na pale akionekana mwenye bashasha na afya njema,” amesema Elizabeth.

“Punde akaanza kuzungumza kwa kusoma taarifa aliyoiandaa akielezea kupandishwa hadhi kwa misitu saba. Haikumchukua zaidi ya dakika 15 alimaliza kusoma maelezo yote na kushukuru kwa kusikilizwa.”

Baada ya kumaliza kuzungumza ulifika muda wa maswali na mwandishi wetu alikuwa miongoni mwa waliotaka kuuliza.

“Lakini kabla hajaruhusu akatokea mwandishi mwingine wa televisheni akamtaka aseme jina lake na cheo chake kwa kuwa alianza kuzungumza bila kufanya hivyo,” alisema mwandishi wetu.

“Wakati anatamka jina lake na cheo chake ghafla sauti ilianza kubadilika na akaonekana kama mwenye shida. Tulipomsogelea kumpa msaada alikuwa amepoteza fahamu. Akatolewa nje kwa ajili ya kupata hewa huku wengine wakimpepea,” alisema mwandishi wetu.

Alieleza kuwa baadaye alichukuliwa na kumpeleka hospitali ya TMJ Chang’ombe na aliwekwa kiti cha nyuma cha gari.

“Muda wote kichwa chake (cha Glory) kililazwa kwenye mapaja yangu,” alisema mwandishi wetu Elizabeth.

“Haikuchukua dakika 10 alifikishwa hospitali na kupelekwa chumba maalumu kwa ajili ya uchunguzi wa kitabibu. Baada ya kumfanyia uchunguzi madaktari wakaeleza kuwa alishafariki dunia kabla ya kufikishwa hospitalini hapo,” alisema.

Daktari aliyempokea, Dk Chris Peterson alieleza kuwa kwa taarifa alizozipata kuhusu historia ya mgonjwa kutoka kwa familia yake, Glory alikuwa na tatizo la shinikizo la damu.

Upandishaji hadhi misitu

Taarifa iliyosomwa na Glory ilieleza kuwa Serikali imeipandisha hadhi misitu saba ambayo ni Itulu, Rondo, Pinndiro, Kalambo, Mwambesi, Aghondi na Kilinga.

Alisema TFS inaendelea na mazungumzo na serikali za vijiji zinaridhia kuhifadhi misitu yao ambayo kwa kiwango kikubwa imeharibiwa.

Lengo la jitihada hizo ni kuirudishia misitu hadhi yake ili kufanya hifadhi kwa faida ya sasa na kizazi kijacho. Pia aligusia suala la ufugaji nyuki na kuhamasisha wafugaji kufuga kibiashara kwa kuwa TFS inaendelea kuwatafutia masoko ndani na nje ya nchi.