Wanafunzi warahisishiwa kusoma vitabu vya fasihi kwa njia ya maigizo

Mwandishi wa Mwananchi Nasra Abdallah (kulia) akifanya mahojiano na Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza.

Muktasari:

Wanafunzi shule ya Sekondari wamerahisishiwa usomaji wa vitabu vya fasihi kwa kuwekwa katika sanaa ya kuigiza

Dar es Salaam. Hivi sasa wanafunzi wa Shule za Sekondari huenda wakapata afueni ya kuelewa vitabu vya fasihi  baada ya kuwekwa katika sanaa ya maonyesho ya jukwaani yale yaliyoandikwa ndani yake.

Hayo yamebainika katika Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu katika ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), ambapo jana Jumatatu Machi 11, 2019 wanafunzi kutoka shule mbalimbali waliangalia maigizo ya kitabu cha 'Passed like a Shadow na 'Kilio Chetu' kutoka kwa waigizaji wa  kikundi cha 'Ngao Art'.

 

Akifungua Jukwaa hilo, Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza amesema maonyesho hayo mbali na kusaidia wanafunzi kuvielewa vitabu hivyo, pia itasaidia kuzalisha wasanii na wataalam katika fani ya sanaa.

 

Mngereza amesema ni ukweli usiopingika mwanafunzi hushika jambo kirahisi pale linapofanyika kivitendo ukilinganisha na kusoma kwa nadharia.

 

"Kama Basata katika jukwaa hili tunakutana na watu mbalimbali na kama mnavyojua moja ya kazi ya sanaa ni pamoja na kutoa elimu, hivyo jukwaa leo (jana) limeona liwalete wanafunzi waweze kujifunza fasihi wanayoisoma darasani kwa njia ya maigizo," amesema.

 

Naye Mkurugenzi wa kikundi cha 'Ngao Art', Ali Mohammed, alisema kupitia mradi wao wa Tanzania Art Education Theatre(TET)',  wamelenga kufikisha elimu kupitia vitabu vya fasihi kwa wanafunzi.

 

Mohammed alisema tayari  wameshakutana na shule mbalimbali katika Mkoa wa Dar es Salaam huku mpango wao ukiwa ni kufikia nchi nzima.

 

Kwa upande wao wanafunzi akiwemo Moses Japhet kutoka shule ya Benjamin Mkapa na Maria Jacob kutoka Kibasila, walisema maigizo hayo ni vema yakawepo mara kwa mara kwani wao ndio mara yao ya kwanza kuyaona.

Wakati mwalimu wa fasihi, Naomi Modest wa shule ya Sekondari Uhuru Mchanganyiko, alisema wamekuwa wakikumbana na changamoto ya uhaba wa vitabu katika kuwafundisha wanafunzi somo la fasihi, ambapo kitabu kimoja hutumiwa na wanafunzi saba na hivyo kupunguza kazi ya uelewa.

Kupitia njia hiyo ya maigizo Naomi amesema itasaidia kupunguza changamoto hizo na kushauri  wasanii kuboresha kwa kuyaweka katika njia za video ili kufikia wanafunzi wengi zaidi.