Matokeo ya miradi ndio yatakayozibeba asasi za kiraia

Friday March 22 2019

Meneja uwezeshaji wa Mfuko wa Asasi za Kiraia

Meneja uwezeshaji wa Mfuko wa Asasi za Kiraia (FCS), Edna Chilimo 

By Elizabeth Edward, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Asasi za kiraia zimetakiwa kutumia kwa usahihi fedha za miradi zinazotolewa kwa wahisani kuhakikisha malengo ya mradi husika yanafikiwa.

Wito huo umetolewa jana Machi 21, 2019 na meneja uwezeshaji wa Mfuko wa Asasi za Kiraia (FCS), Edna Chilimo, wakati wa kuhitimisha ufadhili wa serikali ya Ufaransa kupitia mashirika yake ya PISCCA na DEFI  kwa asasi 12  nchini ambao umedumu kwa miaka miwili.

Chilimo amesema kama asasi itapewa fedha na kushindwa kuonyesha matokeo chanya kwenye mradi wake itakuwa ngumu kwa wafadhili kuendelea kuwekeza katika eneo hilo.

“Siku hizi fedha za mradi matokeo yake yanatakiwa kuonekana kuanzia chini kabisa kwa wananchi ambao ndio walengwa kinyume na hapo inakuwa ngumu kuwashawishi watoe tena fedha.

“Wenzetu serikali ya Ufaransa walifadhili miradi ya asasi 12 na tumeona kumekuwa na matokeo chanya na leo muda wa ufadhili ndio unamalizika sasa ni jukumu letu kukaa na kuangalia tulifanikiwa wapi na kitu gani bado ni changamoto ili hata akitokea mfadhili mwingine tuwe na sehemu nzuri ya kuanzia,” amesema.

Chilimo amesema miongoni mwa miradi iliyofanikiwa kwa kiasi kikubwa ni uliojikita kuelimisha jamii kuhusu athari za ndoa na mimba za utotoni na elimu ya afya ya uzazi.

Advertisement

Akiwakilisha asasi ya Msichana Initiative ambayo ni miongoni mwa wanufaika wa mradi huo, Lightness Njau ameeleza kuwa kwa kiasi kikubwa walizifikia shule za sekondari na kutengeza vikundi vya kutoa elimu kwa wanafunzi.

“Lengo letu ni kuelimisha kuhusu ndoa za utotoni na kwa kiasi kikubwa kupitia ufadhili huu tumefanikiwa kuwafikia mabinti wengi waliopo shuleni na jamii zao,” amesema Njau.

Advertisement