Msajili atishia kuifuta ACT-Wazalendo

Muktasari:

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeeleza nia yake ya kukifutia usajili chama cha ACT-Wazalendo na imekipa siku 14 kuanzia jana kuwasilisha maelezo kwa nini kisichukuliwe hatua.

Dar/Unguja. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeeleza nia yake ya kukifutia usajili chama cha ACT-Wazalendo na imekipa siku 14 kuanzia jana kuwasilisha maelezo kwa nini kisichukuliwe hatua.

Hatua hiyo inakuja ikiwa ni takriban wiki moja baada ya chama hicho kumpokea aliyekuwa katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad aliyekihama chama hicho akiwa na wafuasi wake.

Maalim Seif alihama baada ya Mahakama Kuu kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti halali wa CUF.

Baada ya hatua hiyo, wafuasi wengi wa CUF walimfuata Maalim Seif huku wakishusha bendera za chama hicho na kupandisha za ACT, na pia baadhi ya ofisi kubadilishwa rangi na matumizi.

Vitendo hivyo vimeisukuma ofisi ya msajili kukiandikia chama hicho barua iliyosainiwa jana na msajili msaidizi, Sisty Nyahoza ikieleza nia hiyo na kutoa siku 14 kielekeze kwa nini kisifutwe.

Nyahoza alipoulizwa na Mwananchi kuhusu barua hiyo alijibu kwa kifupi kupitia ujumbe wa maandishi “ni kweli barua inatoka kwetu”, na alipoulizwa zaidi kuhusu maudhui yake alijibu kuwa “barua inajieleza”.

Barua hiyo inaeleza kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 19 cha Sheria ya Vyama vya Siasa, msajili anapotaka kufuta usajili wa chama cha siasa anapaswa kutoa taarifa ya maandishi kwa chama hicho.

“Taarifa hiyo ya maandishi ieleze ukiukwaji wa sheria uliofanyika au ukosefu wa sifa za usajili uliopo na nia yake ya kufuta usajili wa chama hicho, ili kukipa chama husika fursa ya kuelewa kosa lake na kujitetea,” inasema barua hiyo ya kurasa mbili.

Tuhuma zilizomo

Barua hiyo imeyataja mambo yanayodaiwa kukiukwa na chama hicho kuwa ni vitendo vya uvunjifu wa sheria ikiwamo kuchoma moto bendera za CUF baada ya mahakama kutoa hukumu katika kesi namba 23 ya 2016.

Barua ilieleza kuwa vitendo hivyo vinafanywa na “mashabiki wa Maalim Seif, ambao wanadai sasa ni wanachama wa ACT Wazalendo.”

“Kitendo cha kuchoma bendera ya chama cha siasa ni kukiuka kifungu cha 11C cha sheria ya vyama vya siasa,” ilisema sehemu ya barua hiyo ambayo Mwananchi limeona nakala yake.

Vilevile, chama hicho kimetuhumiwa kutumia dini katika siasa zake baada ya mashabiki kuonekana katika mitandao wakipandisha bendera ya ACT-Wazalendo kwa kutumia tamko takatifu la dini ya Kiislamu (Takbira), kitendo kinachokiuka kifungu cha 9 (1)(C) cha sheria hiyo.

Nyahoza alisema licha ya msajili kukemea vitendo hivyo Machi 19 na kusema kuwa anayafanyia kazi matendo hayo, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na chama hicho ikiwa ni pamoja na kutokemea tabia hiyo.

“Kutokana na hilo, inaonekana chama chenu kiliafiki au kuelekeza vitendo hivyo kufanyika,” inasema sehemu ya barua hiyo.

Mbali na hatua hizo, ofisi ya msajili imesema chama hicho kilichopata usajili wa kudumu Mei 5, 2015 kinakabiliwa na adhabu nyingine ya kutowasilisha hesabu za ukaguzi za 2013/2014.

Barua hiyo imenukuu barua ya Mei 22, 2018 kwenda chama hicho iliyokuwa inasitisha ruzuku sambamba na kuhitaji hesabu za miaka mitatu ya 2013/14, 2015/16 na 2017/17 lakini kilipojibu kilitoa hesabu za miaka miwili bila kuweza za 2013/2014.

Alisema kutowasilisha hesabu za mwaka wa fedha wa 2013/14 kinakuwa bado hakijakidhi matakwa ya barua ya msajili wa vyama vya siasa, hivyo kinakuwa kimekiuka sheria ya vyama vya siasa sura ya 258.

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alipoulizwa kuhusu barua hiyo alisema “sielewi unazungumzia barua ipi, mpigie katibu mkuu.”

Katibu mkuu wa chama hicho, Dorothy Temu alipoulizwa alisema, “nipe saa moja naingia kwenye mahojiano nikitoka nitakwenda ofisini kuangalia kama imefika, kwa sasa sijui chochote.”

Pamoja na barua hiyo, Ofisi ya Msajili Zanzibar nayo imetoa tamko ikiwatahadharisha wafuasi wa ACT-Wazalendo ambao wametokea CUF kuacha kufanya vitendo ilivyoviita vya uvunjifu wa amani la sivyo wataishia jela.

Naibu msajili wa Vyama vya Siasa Zanzibar, Mohamed Ali Ameir alisema hayo jana wakati akizungumza na wanahabari ofisini kwake Mbweni.

Katika hatua nyingine, mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa CUF, Mussa Haji Kombo alisaini hati ya kiapo cha mashtaka dhidi ya ACT – Wazalendo katika Mahakama Kuu Zanzibar ikidai wanachama wa chama hicho wameharibu mali za CUF na kuhatarisha amani.